View Full Version : Gavana kuwekwa kiti moto.. na Kamati ya Bunge
mwanakijiji
01-19-2010, 09:37 AM
Sadick Mtulya
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), imepanga keshokutwa kuwa siku ya kumwita gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu ajieleze kuhusu matumizi ya Sh 2.5bilioni kujenga nyumba mbili za kuishi.
Habari zilizolifikia gazeti hili jana na kuthibitishwa na Makamu Mwenyekiti wa POAC, Ester Kilasi zimeeleza kuwa Profesa Ndulu ataitwa katika kamati hiyo baada ya wajumbe wake kufanya ziara eneo la mradi kulikojengwa nyumba hizo.
Kilasi aliliambia gazeti hili jana kuwa ziara hiyo itafanyika kwa siku mbili; leo na kesho.
"POAC imemwita Profesa Ndulu Alhamisi hii (kesho kutwa) ili atupe maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa nyumba anayoishi na za manaibu gavana wake," alisema Kilasi na kuongeza:
"Lakini kabla ya kupata maelezo hayo kamati imeamua kufanya ziara ya kuzungukia na kuangalia hali halisi ya mradi wa ujenzi wa nyumba hizo tujiridhishe." alisema.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kwamba Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe ambaye yuko masomoni Ujerumani amelazimika kurudi nchini kusimamia sakata hilo.
Kamati hiyo itakutana na Profesa Ndulu siku chache baada ya Waziri wa Fedha na Uchumi Mustafa Mkulo kuunda kamati ya kuchunguza suala hilo.
Mkulo aliliambia gazeti hili Ijumaa iliyopita kuwa ripoti ya kamati hiyo imekwishawasilishwa kwake na yeye ameanza kuipitia kabla ya kuitoa hadharani.
"Nikitoka hapa ninakwenda kuisoma ripoti niliyoiagiza kuhusu matumizi ya fedha yaliyotumika katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya gavana na manaibu gavana," alisema Mkulo na kuongeza:
"Hizi tuhuma ni nzito na zinamhusu mtu nyeti wa serikali, hivyo itachukua muda kidogo kutoa majibu ya ripoti niliyonayo."
Mkulo alifafanua kuwa amechelewa kuitoa ripoti hiyo kutokana na kuhusika kwa vyombo vingine nyeti vya serikali katika uchunguzi wake.
"Nikimaliza kuisoma ripoti hii, nitalazimika nishauriane na washauri wangu na kisha nivishirikishe vyombo vingine nyeti vya serikali," alisema
Kwa mara ya kwanza taarifa ya matumizi ya fedha katika ujenzi wa nyumba hizo ziliripotiwa na gazeti hili, lakini baadaye BoT ilitoa ufafanuzi ikieleza kuwa nyumba hizo zilijengwa baada ya kufuatwa taratibu zote za zabuni.
Kabla BoT kujibu tuhuma hizo, Profesa Ndulu alikiri kutumika kwa kiasi hicho cha fedha, lakini akafafanua kuwa fedha ilitumika kujenga upya nyumba hizo na siyo kuzikarabati.
“Nyumba haijakarabatiwa, imejengwa from the ground (kutoka chini)... ni tofauti kukarabati na kujenga nyumba mpya huu, ni upotoshaji wa wazi na kujaribu kuchafua mema,” alilalamika gavana huyo.
My Take:
Hivi hawa watu wanafikiria wao ni kina nani hasa... yaani katika serikali yetu hakuna mtu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi tukamaliza jambo moja.
Ach-F
01-19-2010, 11:51 AM
Wachukue quantity surveyors na Civil Engineers kutathmini hizo gharama na kujua nini hasa kilitokea bila kumung'unya maneno.
mwanakijiji
01-22-2010, 09:07 PM
na Irene Mark na Deogratius Temba (Tanzania Daima)
KAMATI ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma, jana ilishindwa kumuhoji Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndullu kuhusu ukarabati wa nyumba yake na ile ya naibu wake ambazo zimegharimu zaidi ya sh bilioni mbili.
Mchanganuo wa namna fedha zilivyotumika katika ukarabati huo uliotolewa na Gavana Ndullu ulitosha kuwafunga midomo wabunge wa kamati hiyo ambao kwa takriban wiki moja walikuwa wakijigamba kulivalia njuga suala hilo linaloonekana kutumia fedha nyingi.
Gavana Ndullu alieleza kila shilingi ilivyotumika sambamba na kubainisha kwa kina sheria iliyotumika katika kuhakikisha yeye na naibu wake wanapata makazi bora yenye ulinzi wa kutosha.
Licha ya kuwabwaga kwa hoja na maelezo yenye utoshelevu, Gavana Ndullu aliwakebehi wanaodai kwamba alilazimisha kuwekewa bwawa la kuogelea (Swimming pool) kwa maelezo kuwa hana shida ya kuogelea kwa kuwa ameanza kuoga kwenye mito akiwa na miaka mitatu.
Katika hilo alisema: “Wameandika sana ila. Mimi ni Mndamba safi, nimeanza kuogelea nikiwa na miaka mitatu...sihitaji swimming pool. Nimezaliwa kijijini, nimeogelea sana kwenye mito, hata ikiondolewa sitakosa kitu.
“Nyumba zote nilizowahi kuishi hazina swimming pool hata ile niliyojenga mwenyewe ya Mbezi haina bwawa la kuogelea,” alisisitiza Gavana Ndullu kwa sauti ya juu huku akionyesha kutofurahia jambo hilo.
Gavana huyo aliyemrithi marehemu Daudi Ballali, alisema ujenzi wa nyumba hizo ulitokana na sheria ya mwaka 2006 iliyoagiza uongozi wa BoT uwe na magavana watatu ambapo kabla ya sheria hiyo walikuwepo wawili na kwamba iliagiza viongozi hao wapewe makazi.
“Baada ya sheria hiyo, mwaka 2007 mwanzoni BoT ilifanya uamuzi wa kupata wataalam waelekezi wa michoro kwa ajili ya makazi ya viongozi hao wa benki. Kwa kusimamia utaratibu wa ujenzi na sheria ya mwaka 2004 ya manunuzi ya umma, zabuni ilitangazwa. Mwenzetu mmoja alikwenda kuishi kwenye nyumba ya gavana aliyenitangulia (akimaanisha Ballali).
“Walipatikana wazabuni 12, kati yao 10 walishinda. Aliyekuwa na gharama ya chini alisema ujenzi ungegharimu sh 1,399,184,549 na yule wa juu ni sh 1,847,000,000. Hapo bodi ya zabuni ilikaa ikamteua mwenye gharama za chini.
“Baada ya negotiation (makubaliano) kati ya mzabuni na bodi wakakubaliana kuwa ujenzi wa nyumba moja yaani ile ya gavana ni sh bilioni 1.274 hapo waliingia mkataba wa bei isiyobadilika.
“Nyumba ya pili ambayo sasa ni ile ya naibu gavana, baada ya kutangazwa kwa zabuni walijitokeza wazabuni watano. Katika utaratibu kama wa awali, walikubaliana kwa sh bilioni 1.272. Ikumbukwe kwamba kila nyumba ilikuwa na mradi wa peke yake,” alisema Ndullu huku wabunge na waandishi wa habari wakimsikiliza kwa umakini.
Licha ya kuwa ni miradi miwili tofauti, lakini mchoro na kila kitu kwenye nyumba hiyo vilifanana, ambapo kuna nyumba ya vyumba vitano, nyumba ya watumishi yenye bafu na choo, sehemu ya mapokezi, kibanda cha walinzi chenye choo, bwawa la kuogelea, jenereta kubwa, vifaa vya tahadhari ya moto, mfumo wa umeme kwa ajili ya ulinzi, viyoyozi na vifaa vingine muhimu.
“Napenda kuweka wazi, ulinzi kwa gavana ni kitu muhimu sana. Leo nikitekwa mimi si jambo dogo…ndiyo maana ujenzi wa nyumba hizi ulizingatia sana ulinzi. Kwa wanaolifahamu eneo hili upande mmoja kuna ukuta mrefu wenye usalama,” alisema.
Kwa zaidi ya dakika 35 gavana huyo alikuwa akiieleza kamati hiyo ya Bunge chanzo na mchakato mzima wa matumizi ya fedha hizo, huku akisisitiza kwamba nyumba hizo ni mali ya BoT kwa ajili ya gavana yeyote atakayekuja, kabla ya kutaja gharama za bwawa la kuogelea kuwa ni sh milioni 40.
Aidha, gavana huyo alisema tayari nyumba hizo zimekabidhiwa kwa BoT na wameanza kuishi humo tangu Desemba mwaka jana na kwa mujibu wa mkataba huo, BoT imepewa muda wa miezi sita ya kuhakiki nyumba hizo na miezi 12 kwa ajili ya kufanya marekebisho ya kitu chochote kwenye nyumba hizo.
Hata hivyo, Ndullu alisema baada ya kuteuliwa kuwa naibu gavana mwaka 2007 alikuwa akiishi nyumbani kwake Mbezi na kwamba alihamishiwa Masaki kwenye nyumba ya kupanga miezi minane baadaye kutokana na foleni za njiani kutoka Mbezi hadi kazini kwake.
Alisema mwaka 2008 BoT ilimpatia nyumba ya kupanga ambapo kodi yake ilikuwa dola 7,000 kwa mwezi alipoishi kwa kipindi cha mwaka mmoja, hali iliyolazimu ukarabati wa nyumba hizo kuharakishwa ili kupunguza mzigo wa kodi.
“Jamani nyumba hizi ni mali ya benki, hivyo nikiondoka mimi atakuja gavana mwingine kuishi humo. Nyumba hizi zitaanza kujilipa baada ya miaka 12 na uwezo wake kuendelea kuwepo ni baada ya miaka 100,” alisisitiza Ndullu kabla ya kuhitimisha maelezo yake.
Baada ya mchanganuo huo, kwa ruhusa ya Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zitto Kabwe, Mbunge wa Ilemela, Antony Diallo alimpongeza gavana huyo kwa maelezo mazuri yenye utoshelevu licha ya kuwepo kwa maswali madogo mawili kutoka kwa wajumbe hao kinyume cha matarajio ya waandishi na baadhi ya wabunge wa kamati hiyo.
Akihitimisha mjadala huo, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliendeleza pongezi kwa gavana na kubainisha kwamba hesabu na gharama za ujenzi huo zitapitiwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa lengo la kukutana nazo kwenye hesabu zinazoishia Juni mwaka huu.
“Tunamuomba CAG afanye utaratibu wa kukagua gharama zilizotumika kama zinaendana na kilichopangwa kujengwa, ateue wataalamu huru wa majengo ambao hawataingiliwa na mamlaka nyingine.
“Sisi ni wanasiasa, tungependa kupata taarifa zaidi za kiutaalamu jinsi kazi ilivyofanyika, mchakato wa kutangaza zabuni na mambo yote yanayohusiana na mradi huo, kama mlivyoona hili ni suala lenye maslahi kwa jamii, hivyo kila kitu lazima kiwe wazi,” alisema Zitto.
mwanakijiji
01-25-2010, 08:41 AM
Ndulu: Gharama jumba la Gavana BoT ni halali (Nipashe)
Muhibu Said
Wakati Gavana wa Benki Kuu, Profesa Benno Ndulu, akitetea gharama ya ujenzi wa nyumba ya gavana iliyogharimu Sh. bilioni 1.4, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) imeagiza tathmini ya nyumba hiyo ifanyike haraka.
Hayo yalijitokeza jana wakati Profesa Ndulu alipofika mbele ya kamati hiyo kutoa maelezo juu ya ujenzi wake ambao katika siku za hivi karibuni kumekuwa na maneno mitaani kuwa ujenzi wake ni wa gharama kubwa mno.
Baada ya maelezo hayo mbele ya kamati jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliagizwa na kamati kumteua mthamini binafsi kwa ajili ya kuifanyia tathmini nyumba hiyo na kuwasilisha ripoti yake kabla ya mwisho wa mwezi ujao.
Lengo la tathmini hiyo ni kupata gharama halisi zilizotumika katika ujenzi wa nyumba hiyo, ambao unalalamikiwa kutumia gharama mara mbili zaidi ya bei ya kununulia nyumba hiyo.
Nyumba hiyo iliyoko Oysterbay eneo la Morogoro Stores, jirani na nyumbani kwa Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip Mangula, jijini Dar es Salaam, ilinunuliwa kwa dola za Marekani 400,000, ambazo ni takriban Sh. milioni 500, wakati ujenzi wake ulitumia zaidi ya Sh. bilioni 1.4 kufikia Desemba, mwaka jana.
Nyumba nyingine, ambazo POAC imeagiza kufanyiwa tathmini, ni zile wanazoishi manaibu gavana watatu. Zote zilijengwa katika mradi wa nyumba za vigogo wa BoT unaodaiwa kugharimu jumla ya zaidi ya Sh. bilioni 2. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa POAC, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kikao cha jana cha kamati yake, kilihusu kupitia hesabu za benki za mwaka unaoisha Juni, 2008 na kujadili ripoti ya CAG na kuongeza kuwa suala la nyumba hiyo lilipewa nafasi kwa vile linagusa maslahi ya umma.
Zitto ambaye jana aliongoza kikao cha POAC, alisema lengo la kutoa agizo hilo kwa CAG ni ili kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kamati kutoa maoni yake.
“Kamati imeridhia maelezo aliyoyatoa. Ombi ni kwamba CAG kwa kushirikiana na wataalamu afanye utaratibu wa kutathmini, sisi hapa ni wanasiasa, tunataka ushauri wa kitaalamu kabla ya kamati kutoa maoni yake,” alisema Zitto.
Awali, Profesa Ndulu ambaye jana aliongea mbele ya kamati hiyo kwa umakini na kwa kujiamini, alitetea gharama zilizotumika katika ujenzi wa nyumba hiyo, kwa kusema kwamba, ni sahihi. Alisema mbali ya ujenzi huo kuwa ni sahihi, pia wanaamini kuwa nyumba hiyo itadumu kwa zaidi ya miaka mia, watafaidika kwa vile hawatalipa kodi tena ya majengo.
“Nyaraka na gharama zote tunazo,” alisema Profesa Ndulu.
Profesa Ndulu alisema uamuzi wa kujenga nyumba hizo, ulifikiwa baada ya kutafakari kwamba, vigogo hao wa BoT waendelee kuishi nyumba za kupanga, ambazo gharama yake ilikuwa ni dola za Marekani 7,800 kwa mwezi, ambapo kwa mwaka ilikuwa ni dola 93,000 (Sh. milioni 113), au wajengewe nyumba mpya.
Alisema pia uamuzi huo ulifuata taratibu na sheria zote zinazohusika, ikiwamo ile ya kumpata mzabuni wa ujenzi na kwamba, nyumba hizo bado ni rasilimali ya BoT wakati wowote ama yeye (Profesa Ndulu) akiwapo au akiondoka.
Naye mjumbe wa kamati hiyo, ambaye ni Mbunge wa Ilemela, Anthony Diallo (CCM), aliunga mkono utetezi uliotolewa na Profesa Ndulu kwa kusema kuwa haoni kuwa ni ajabu gharama zilizotumika katika ukarabati wa nyumba hiyo kwa vile eneo lililoko, bei ya kiwanja peke yake ni zaidi ya Sh. milioni 500.
Tayari Profesa Ndulu ameshahamia na anaishi katika nyumba hiyo tangu Desemba mosi, mwaka jana.
Mbali na nyumba hiyo, nyumba nyingine zinazolalamikiwa kutumia gharama kubwa katika ukarabati wake, ni ya Naibu Gavana wa Kwanza, Juma Reli, iliyo Masaki, Mtaa wa Chole. Nyumba hiyo ilikuwa ikitumiwa na Gavana wa zamani, marehemu Daudi Ballali.
Nyumba nyingine iliyo kwenye malalamiko hayo ya ufujaji wa mamilioni ya walipa kodi, ni ile inayotumiwa na Naibu Gavana wa Pili, Enos Bukuku, iliyoko Oysterbay pamoja na ya Naibu Gavana wa Tatu, Nilla Mkila iliyoko Masaki.
NIPASHE
Ach-F
01-25-2010, 05:06 PM
Tanzania pole sana nyumba inanunuliwa kwa $400,000.00 then wanaikarabati kwa 1.4 billion. Kweli tuna shamba kubwa la bibi. je huu ni utetezi unaokubalika na mkuu wa Kaya?
Powered by vBulletin™ Version 4.0.2 Copyright © 2012 vBulletin Solutions, Inc. All rights reserved.