PDA

View Full Version : CWT kushiriki mgomo wa wafanyakazi wote!



mwanakijiji
03-17-2010, 07:19 PM
Felix Mwagara (mwananchi)

CHAMA Cha Walimu nchini (CWT) kimesema kitashiriki kikamilifu kwenye mgomo wa nchi nzima uliotangazwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta).

Tucta imetangaza kuwa wafanyakazi nchi nzima watafanya mgomo kuanzia Mei 5 wakipinga mambo mbalimbali na kwamba wameishaitaarifu serikali juu ya kusudio la mgomo wao kama sheria inavyoeleza kuwa taarifa ya mgomo inatakiwa kuwa ya siku 90 kabla ya tarehe ya kufanyika.

Rais wa CWT, Gratian Mukoba aliiambia Mwananchi jana kuwa chama hicho ni kati ya vyama 14 vilivyo ndani ya Tucta na kwa maana hiyo kauli ya shirikisho hilo inaheshimiwa na CWT, ambayo ina nguvu zaidi ndani ya Tucta kulinganisha na vyama vingine.

Alisema kama rais wa CWT haba budi kutoa taarifa kwa walimu wote nchini na ili wafahamu kuwa chama chao kimeitikia wito wa kushiriki kwenye mgomo wa kudai mambo mbalimbali ambayo serikali imeyadharau kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa viongozi wa vyama vyote wamekubaliana kuwatangazia wanachama wao kuhusu mgomo huo ili washirikiane kudai haki zao chini ya mwavuli wa Tucta.

"Baada ya Tucta kutangaza na sisi tunatoa tamko kwa walimu wote kushiriki katika kudai haki zetu ambazo nasi zinatugusa," alisema Mukoba.

"Madai hayo ni pamoja na mishahara duni isiyokidhi mahitaji, mafao duni ya wastaafu kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na ulipishwaji wa kodi kubwa kwenye mishahara midogo wanayopata wafanyakazi," alisema.

Alisema hivyo ndivyo vitu vitatu vikubwa watakavyovidai kwenye mgomo huo na kwamba watatumia sherehe za Mei Mosi kuhamasishana na kufahamishana jinsi ya kufanya mgomo huo Mei 5.

Aliongeza kuwa serikali imeshindwa kuwaongezea mishahara tangu walipotoa mapendekezo yao ya kiasi cha Sh315,000 kwa kima cha chini ambacho wanadai kilipuuzwa na serikali ambayo sasa inalipa Sh104,000 kwa kima chini.

Mukoba alisema mapendekezo hayo waliyapeleka serikalini tangu miaka mitano iliyopita, lakini bado wanaona kimya hivyo basi muda umefika sasa kuhakikisha wanapata haki zao wafanyakazi wote.

Siku kadhaa zilizopita rais wa Tucta, Omary Ayubu alitangaza rasmi mgomo wa siku nne wa wafanyakazi kwa ajili ya kuishinikiza serikali kuchukua hatua madhubuti dhidi ya ufisadi uliokithiri pamoja na kuongeza mishahara ya wafanyakazi.

Ayubu alitoa tamko hilo wakati wa kikao cha 18 cha baraza kuu la Tucta kilichofanyika mjini Morogoro na kueleza kuwa mgomo huo ni halali na kuwatahadharisha wafanyakazi dhidi ya vitisho vyovyote kutoka kwa waajiri.

Ayubu alisema awali katika kikao cha kazi kilichofanyika Oktoba 2009, shirikisho lilitoa tamko kwa serikali la kudai kutekelezwa na kurekebishwa kwa madai ya muda mrefu ya wafanyakazi, lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika zaidi ya ahadi za kila mara.

Alitaja madai ya muda mrefu yaliyotakiwa kutekelezwa kuwa ni pamoja na hoja ya kuongeza mishahara ambayo kwa sasa ni duni, kuongeza mafao ya wastaafu kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii, kupunguza kodi inayotozwa kwenye mishahara ya wafanyakazi, serikali na waajiri kutoheshimu sheria za kazi na mgawanyo mbaya wa pato la taifa.

Ayubu pia alisema Tucta haitamwalika rais wala waziri mkuu katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu kwa kuwa inataka sherehe hizo ziwe za wafanyakazi kujadili mambo yao.

Walidaikuwa hawawezi kuwaalika kwa vile rais ameshindwa kughulikia matatizo yao hivyo hawaoni sababu za kuwa mgeni rasmi badala yake Rais wa chama hicho ndiye atakuwa mgeni rasmi.

Hata hivyo, siku chache baada ya kauli hiyo ya Tucta, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma kapuya alisema anashangazwa na uamuzi huo kwa vile Rais Kikwete na serikali yake amekuwa mstari wa mbele kutatua kero za wafanyakazi kupita wizara yake.