PDA

View Full Version : Mechi ya Brazil na Tanzania jinsi siasa inavyoharibu soka!



mwanakijiji
06-08-2010, 07:19 PM
Kama kuna mechi ambayo ingetakiwa kujaza uwanja wetu mpya wa Taifa wenye uwezo wa kuchukua watu wapatao 60,000 ilikuwa ni mechi hii ya kuwaleta Brazil nchini siku chache kabla ya timu hiyo maarufu zaidi duniani kuanza kushiriki kinyang'anyiro cha Kombe la Dunia. Mechi hiyo ilitakiwa ioneshe jinsi gani Tanzania ni wapenzi wa soka na kuwa timu hiyo ya Brazil inapendwa nchini na ingetumika hata kama siyo kutangaza utalii bali kutangaza timu yetu na vipaji vyetu tulivyonavyo. Kwa sababu tusizozijua mechi hiyo ilikuwa tupu uwanjani; washangiliaji walikuwa wachache na hata uchezaji wa timu yetu ya taifa yenyewe ukiondoa mengine ulikuwa wa kiusindikizaji na hata siyo kujaribu kuwa burudani. Ni kama tulitarajia kufungwa na Brazil na tukajiandaa kufungwa kama vile kupewa ujiko!

Ninaamini kwa upande wangu baada ya kuangalia maandalizi ya mechi na hatimaye kuangalia "live" mechi yenyewe (unaweza kuona clips kwenye forums hapa) naweza kusema pasipo shaka kuwa Watanzania na watawala wetu tunapenda makubwa bila kutaka kulipa gharama yake. Tunataka kuwa na timu za kimataifa, uwanja wa kimataifa, maisha ya kisasa na kuonekana na sisi tupo duniani lakini wakati huo huo hatutaki au hatudhamirii kulipa gharama ya malipo ya ukubwa. Gharama hizo ni pamoja na uwazi, uwajibikaji, uadilifu, ukweli, umakini na uthubutu. Sisi hatutaki yote hayo kwani yanatusumbua na yatawafanya watu wengine waonekane wanajua "sana" au wana "kimbelembele".



Matokeo yake ndiyo haya tuliyoyaona. Mechi ya Brazil kwa maoni yangu ilitakiwa iwe ni ya bure kabisa kwa wote wanaotaka kuiona na serikali ingeingia tu gharama ya kuwaleta na kuwahudumia ikikubaliana kuweka pia matangazo yetu wenyewe kuzunguka uwanja badala ya matangazo "yao" pamoja na haki za kurusha mechi hiyo ndani ya nchi yetu.



Lakini watawala wetu pamoja na TFF wakiwa kama waliopigwa changa la macho hawakujadiliana kutafuta masharti mazuri ya kufanikisha mechi hiyo. Matokeo yake wakaigeuza kuwa ya kibiashara ili waone ni jinsi gani "Brazili ingewaingizia pesa nyingi". Ni matumaini yangu wamepata hasara ya kutosha kuwa funzo kwao. Wakajaribu kutafuta mbinu zao za kifisadi za kuona jinsi gani wangeweza kuwafyonza mbayuwayu wetu ili wapate fedha ya kutosha wakijua kuwa Brazil ni jina kubwa. Serikali ikawakubalia na wao wenyewe TFF wakafanya madudu yao ambayo sasa hivi tunaweza kusema wamehitimu katika kuyafanya.



Na kama kawaida yao hakuna atakayekubali makosa - kwani viongozi wa Tanzania hawakosei na watatafuta maelezo mengine yote isipokuwa ya uzembe na kutokuwajibika kuelezea kwanini wananchi hawakutaka kujazana kuangalia mechi. Watadai siku ilikuwa mbaya na kuwa labda viingilio tu vilikuwa vikubwa sana kitu ambacho mtoto yeyote wa mbayuwayu angeweza kukiona.



Kilichouudhi zaidi ni kuwa Rais wetu ambaye ni "shabiki mkubwa wa soka" hawezi kusimama na kuomba radhi kwa kuendekeza TFF hii na ubovu wake. Aliwapa kocha toka Brazil ambaye anapomaliza muda wake wa mkataba atakuwa amekomba zaidi ya shilingi za madafu milioni 600 na hapo bila kuongeza marupurupu na posha kibao! Katika wazimu wao wameenda kumkodisha kocha mwingine wa kigeni wakikataa kabisa kuwekeza fedha hizo kutoa scholarship kwa makocha wazalendo kusomea ukocha katika vyuo mbalimbali duniani na kuwaendeleza makocha wetu wenyewe siyo kwa visemina vya hapa na pale bali kwa elimu hasa ya mambo ya michezo.



Yote haya yamechangiwa na viongozi wa kisiasa wanapoingialia masuala ya soka kwa namna ambayo inasababisha iwepo ndoa isiyo takatatifu; yaani mahusiano ya kishikaji ambayo yanaweka kipaumbele katika kufurahishana, kubebena na kulindana.



Tulichoshuhudia jana tunaweza kukielezea kwa maneno machache tu kuwa ni kilele cha uzembe na kutokuwa na mikakati madhubuti ya kutumia fursa mbalimbalia ambazo zinawekwa mbele zetu aidha kwa sababu hatujiamini au kwa sababu tumekubali kuwa hatuna uwezo wa kufanya makuu. Na kwa vile sisi tuko vile vile tutawarudisha watu wale wale wamadarakani, wenye sifa zile zile, mwelekeo ule ule na mikakati ile ile ya kushindwa - TUKITARAJIA MATOKEO TOFAUTI!



Wenyewe wanaita huu ni 'wazimu'!

Matigari
06-17-2010, 06:09 PM
I just don't understand how you can screw up a football match in Tanzania, any football match let alone the Brazil team visiting. It the marketing principles Stupid.