PDA

View Full Version : Wameshindwa miaka 25 wataweza miaka 5?



mwanakijiji
09-16-2010, 10:59 PM
Na. M. M. Mwanakijiji

Baada ya Baba wa Taifa Mwalimu J. K. Nyerere kusoma alama za nyakati na kuelewa kuwa kwa uwezo wake wa kibinadamu aliweza kuwafikisha Watanzania mahali alipowafikisha aliamua kuachia "ngazi" au kama tulivyoita wakati ule aliamua kung'atuka. Shujaa wangu alitambua kuwa uongozi una kikomo chake cha uwezo wa mwanadamu na vyovyote vile ilivyo alitambua kuwa Tanzania ni lazima itakuja kutawaliwa na watu wengine nje ya yeye mwenyewe.

Hivyo, akaliandaa Taifa kuwa na viongozi wengine na akamuachia Mzee Ali Hassan Mwinyi kushika usukani. Mwinyi akaingia na Ruksa kwa miaka kumi ya kile ambacho kinajulikana kama ufunguaji wa uchumi wetu kwa sekta binafsi. Hii iliaminika kuwa ingekuwa dawa ya kulileta taifa letu katika mafanikio ya mtu mmoja mmoja. Naye alipomaliza miaka yake kumi akamuachia Mkapa ambaye naye aliingia kwa kubinafsisha taasisi na makampuni mbalimbali yaliyokuwa ya umma kwa nguvu kubwa. Mkapa akawa mtu aliyefungua uchumi wetu kwa wawekezaji wa ng'ambo kwa kiasi kikubwa akisimamia upitishwaji wa baadhi ya sheria mbovu kabisa kuwahi kutungwa na watu huru.

Alipomaliza naye miaka yake kumi ya majaribio ambayo iliisha kwa mlolongo wa kashfa ambazo hazijawahi kutoka katika taifa hili akamuachia usukani Rais Kikwete ambaye naye aliahidi kuendeleza "mazuri" yaliyofanywa na serikali zilizopita na kuleta mapya kwa kile alichokiita "kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya". Kikwete alipoingia aliingia kwa kujumlisha yale ya Mwinyi (Ruksa) na yale ya Mkapa (Ubinafsishaji) kwa nguvu zaidi lakini akaongeza na ya kwake ambayo ameyasimamia miaka hii mitano inayoisha. Yeye kaja na Uchumi wa Wawekezaji akiamini kabisa kuwa bila ya wawekezaji wa kigeni Tanzania haiwezi kuendelea na hivyo akitumia nadharia ya ruksa (ya Mwinyi) amezidi kufungua sekta na sehemu mbalimbali za uchumi wetu kwa wawekezaji wa kigeni hata katika mambo ambayo ukiyakodolea kwa karibu yanashangaza (kama uchimbaji wa vyoo vya shule!)!

Kikwete naye kama Mkapa kabla yake amesimamia serikali iliyogubikwa na mlolongo wa kashfa ambazo kuzirudia tena kunaweza kuwa ni kashfa vile vile.

Miaka ishirini na mitano ya watawala watatu ilitarajiwa ingeweza kufuta na kurekebisha matokeo ya utawala wa Rais mmoja aliyekuwa madarakani kwa karibu miaka 24 hivi. Lakini nusu karne ya watawala watatu mbalimbali wakiwa na faida ya ulimwengu wa kisasa, uliotulia kutoka katika vita baridi, chini ya Afrika iliyo na amani zaidi na mahusiano ya kimataifa ambayo yametengemaa kuliko wakati wowote ule katika historia yetu. Watawala hawa watoto wamekuja na kila mpango na miradi ya "maendeleo" ambayo wameijaribisha. Kuanzia mipango ya "kufufua uchumi" ya miaka ya themanini na mipangao ya MTUKUTA, MKURABITA na MMEM n.k ya miaka ya 2000!.

Kusema kweli wamejaribu. Wamejaribu kutawala na kufanya yote yaliyo ndani ya uwezo wao. WAmejaribu kurekebisha muundo wa serikali, wamejaribu kupigana na rushwa, wamejaribu kubadilisha elimu ya msingi, sekondari na ya juu, wamejaribu kuleta utawala bora. Naam! Wamejaribu saana kama timu ambayo licha ya jezi nzuri, na makocha wazuri imeendelea kufungwa katika mechi zake mbalimbali hata zile ambazo walitarajiwa angalau kutoka sare. Wamejaribu kuliongoza taifa kwa miaka 25. Na wamefanikiwa katika kujaribu.

Wamefanikiwa kujaribu kuongeza vitu mbalimbali na ni kweli chini yao idadi ya vitu mbalimbali imeongezeka. Ukiwasikiliza kwa makini utaona wanasifia idadi zaidi kuliko ubora. Kwao wao maendeleo ni kuongezeka kwa idadi. Watasema wameongeza idadi ya vyuo, walimu, shule, majengo, n.k Wameanza kuwa kama Korea ya Kaskazini! Wanajivuna katik akuongeza idadi. Lakini macho yetu yanatufanya tuwe mashuhuda wa kushindwa katika majaribio yao.

Bado jiji la Dar ni miongoni mwa majini machafu kabisa, bado elimu ya juu ina matatizo makubwa katika ubora na upatikanaji wake, hospitali zetu bado hazijafikia kiwango cha kisasa zikiendelea kuwa mlundikano mkubwa wagonjwa, mipango yetu ya uokoaji bado ni mibovu kabisa kama tulivyoshuhudia juzi mtu aliyekuwa kwenye mtaro kwa masaa ishirini na nne akiojaribiwa kuokolewa kwa njia za enzi za ujima! Katika miaka yao ya robo karne bado kuna watoto wetu vijijini na mijini ambao wanasoma kwa kukalia matofali huku madara yao yakiwa yameezekwa nyasi wakati mtu mmoja anajengenewa jumba analo"stahili" kwa bilioni 3, huku wao wakijigawia bilioni karibu thelathini kila mwaka kwa ajili ya samani na chai huku wakiahidi kuleta bajaji kupeleka mabinti, mama na dada zetu hospitali wakati wa kujifungua!

Wamejaribu ndugu zangu. Kwa miaka 25 wamejaribu kushindwa na kwa hakika wameonesha jinsi wanavyozidi kushindwa. Kinachoshangaza ni kuwa wanataka miaka mingine mitano ya majaribio mengine makubwa. Yaani wanataka kujaribu kutuahidi kuwa yale ambayo wameshindwa kuyafanya kwa miaka 25 wataweza kuyafanya kwa miaka mitano kwa kutumia viongozi wale wale, wenye sera zile zile wakiongoza na itikadi ile ile ya "majaribio".

Kumbe swali kubwa ambalo wapiga kura wa Tanzania wanakabiliwa nalo na ndilo kubwa litakalotakiwa kuwaongoza kupiga kura katika uchaguzi huu mkuu ni hili: Je, wanaamini utawala wa CCM uliodumu kwa miaka 25 katika majaribio yaliyoshindwa unaweza kufanikiwa katika miaka mitano? Je, kama wameshindwa kuboresha shule za msingi kwa miaka 25 wataweza kweli kufanya hivyo kwa miaka mitano? Kama wameshindwa kutafuta namna nzuri ya kutoa elimu ya juu kwa miaka 25 ya uliberali wa kiuchumi wataweza kweli kufanya hivyo kwa miaka mingine mitano? Je wananchi wa Dar ambao wanaishi katika mojawapo ya majiji yaliyopangwa vibaya zaidi, machafu na yenye changamoto za kudumu za maji, umeme na usalama kwa miaka 25 kweli wanatarajia kuwa maisha yao yatakuwa tofauti na hali zao kuinuliwa kwa miaka mitano ijayo? Kweli wakazi wa Dar wanaamini chini ya watawala wale wale hospitali ya Mwananyamala, Temeke na Muhimbili zitakuwa bora zaidi miaka mitano ijayo kuliko miaka 25 iliyopita?

Naam, wapo wanaomini kuwa inawezekana. Naam ni imani tu. Na wengine wataapia kabisa kuwa inawezekana. Lakini msingi wa imani hiyo ni nini isipokuwa njozi kama za Alinacha? Wale wale walioshindwa miaka ishirini na mitano wataweza kweli miaka mitano?
Waliokataa kufanya marekebisho makubwa ya Katiba miaka ishirini na mitano wataweza kuleta mabadiliko miaka mitano bila mabadiliko makubwa ya Katiba? Walioshindwa kutunga sheria nzuri za uwekezaji na sera nzuri za misaada ya kigeni kwa miaka ishirini na mitano wataweza kweli kuleta mabadiliko katika miaka mitano ijayo?

Ndugu zangu, tunapoendelea kutafakari ujio wa uchaguzi mkuu ni lazima tujiulize katika dhamira zetu kama tunataka mabadiliko makubwa miaka mitano chini ya uongozi mpya, wenye sera tofauti na za sasa na wenye maono makubwa zaidi au kuendelea kwa kujaribisha watu wale wale ambao tunajua tayari wameshatuonesha kuwa wanashindwa?

Kama tumekuwa kwenye basi ambalo dereva wake amekuwa akipata ajali za mara kwa mara na kusababisha maafa na majeruhi miaka 25 tuendelee kumchagua dereva yule yule kwa vile ati tumemzoea na kwa vile tayari tunajua kuwa anaweza kupata ajali nyingine au tuamue kumpatia dereva mwingine ambaye anakuja na gari jingine na utaalamu mwingine wa uendeshaji wa gari hilo?

Katika uchaguzi huu wapo watakaoingia kwenye gari la kwanza kwa vile wamelizoea na wanajua kuwa hata ajali ikitokea wanaweza wasidhurike. Lakini ni majasiri wale wanaotaka kuingia kwenye gari jipya chini ya dereva mpya. Hapo pana tofauti kati ya wenye hofu na majasiri. Kutokana na mazoea wengine watapanda gari la kwanza na hatuwezi kuwashangaa kwani ndilo gari pekee lililokuwepo kijijini kwa muda mrefu, lakini nuru mpya na mwanga mpya umeanza kuangaza, gari jipya lipo kijijini, dereva mpya kashika usukani, anasema twende!

Waliozoea gari la zamani lenye ajali za mara kwa mara na waende kulipanda kwa furaha, lakini wanaotaka kutafuta njia mbadala wanalazimika kutafuta usafiri mwingine. Kwani, gari lililoshindwa kupanda mlima kwa miaka 25 litaweza vipi kupanda kwa miaka mitano likiwa na dereva yule yule, makonda wale wale na ubovu ule ule? Labda kuna wakati inabidi hata tutumie pikipiki!

MAHESABU
09-18-2010, 05:13 PM
ASANTE MWANAKIJIJI kwa hoja ndefu na yenye mantiki katika kipindi tulichonacho cha uchaguzi mkuu, lakini nipende kueleza kuwa UMEGUSA ZAIDI UPANDE MMOJA...bado hujauelezea upande mwingine ambao kwa MUDA WA MIAKA ZAIDI YA 15 WAMESHINDWA KUCHUKUA HATA ROBO YA SIFA(VITI) YA UDEREVA WA KUENDESHA GARI LETU ILI WATUFIKISHE WAENDAKO....tulichoshudia kwa magari haya kumbe ni"MAGARI YA KICHINA/magari ya JABA" ambayo unalinunua kabla ya kufika uendako linakuwa limekongoroka....!
Kwa mara nyingine tena tumeona magari na madereva hao pamoja na makonda wao wakiwa wamejaa dhuluma,matusi,kejeli, pasipo na ufumbuzi makini kwa abiria isipokuwa madereva wachache walioonyesha UMAKINI.....sishindwi kumtaja mtu kama NDESAMBURO ambaye amekuwa akitumia juhudi binafsi kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo aliyoyaahidi...WALIOBAKI NI MABINGWA WA POROJO....!

edo
10-22-2010, 08:49 AM
Ahsante MM kwa post yako na ninakubaliana na wewe.Kwamba watawala wetu wa sasa wameshindwa,hilo halina ubishi kwa mtu yeyote mwenye fikra sahihi.Sidhani kama ni sahihi kuwalaumu hao madereva mbadala kama alivyosema bwana mahesabu hapo juu kwa sababu fursa walizo nazo wao si sawa na hizo za watawala.Nionavyo mimi,uwanja usio sawa wa mapambano ndo chanzo cha hao jamaa kushindwa kupata hivyo viti.Kwa vyovyote vile,hawastahili kupewa muda mwingine kwani wameshindwa!!

Max Shimba
12-27-2010, 09:45 PM
Viongozi wetu hawana maono. Wanacho juwa wao ni kwenda ofisini kufungua faili, nikimaanisha, kufuata upepo na kumfurahisha aliye wapa ulaji, yaani Mkuu JK.

Ach-F
12-28-2010, 11:43 PM
Viongozi wetu hawana maono. Wanacho juwa wao ni kwenda ofisini kufungua faili, nikimaanisha, kufuata upepo na kumfurahisha aliye wapa ulaji, yaani Mkuu JK.

Hiyo ndio culture inayotakiwa kubadilishwa. Angalia Jeshi la polisi yaani ni kubwa sana kiasi kwamba uwajibikaji ni zero, wanafuata upepo tu Tanzania haiwezi kuendelea kwa mfumo uliopitwa we need changes now!

Max Shimba
12-29-2010, 12:06 AM
Hiyo ndio culture inayotakiwa kubadilishwa. Angalia Jeshi la polisi yaani ni kubwa sana kiasi kwamba uwajibikaji ni zero, wanafuata upepo tu Tanzania haiwezi kuendelea kwa mfumo uliopitwa we need changes now!

Sasa yule S. Mwema si rafiki yake Mukulu JK. Unajuwa, wakati ule wa miaka ya tisini mwanzoni si ndio walianza urafiki? Sasa alipo kamata uraisi tu, akampa rafiki ulaji, hivi, S. Mwema wa pale kati ninaye mjuwa mimi kweli ndio mkuu wa Polisi! Dar imewashinda sasa wameigawa kuwa mikoa ya kipolisi mitatu! Nini Mwema amesha fanya? Ni wale wale wafuata mkumbo na upepo kwa mtaji wa wananchi.

Max Shimba
12-29-2010, 12:07 AM
Hiyo ndio culture inayotakiwa kubadilishwa. Angalia Jeshi la polisi yaani ni kubwa sana kiasi kwamba uwajibikaji ni zero, wanafuata upepo tu Tanzania haiwezi kuendelea kwa mfumo uliopitwa we need changes now!

Sasa yule S. Mwema si rafiki yake Mukulu JK. Unajuwa, wakati ule wa miaka ya tisini mwanzoni si ndio walianza urafiki? Sasa alipo kamata uraisi tu, akampa rafiki ulaji, hivi, S. Mwema wa pale kati ninaye mjuwa mimi kweli ndio mkuu wa Polisi! Dar imewashinda sasa wameigawa kuwa mikoa ya kipolisi mitatu! Nini Mwema amesha fanya? Ni wale wale wafuata mkumpo na upepo kwa mtaji wa wananchi.

Dua
01-14-2012, 03:44 PM
Inafurahisha kuona nchi za Afrika hususan Tanzania kuwa kimya wakati nchi za ulaya wanawadhulumu Watanzania (waafrika) katika exchange rate mechanism, na kuendelea kukumbatia dollar na Eu currencies ambazo hazina thamani.

gfsonwin
05-17-2012, 06:12 PM
unajua kwa system ya tz ilivyo,watu wanategemea sana wizi na pesa za haraka, kimsingi watawala wetu siyo wzuri kwani wana uchu wa kujilimbikizia mali na kugain popularity. But uwajibikaji wa dhati haupo kabisa miongoni mwao. Binafsi huwa naumia sana kwani wawajubikaji wakubwa katika taifa hili ni wale wasio na madaraka na ammbao wanapata kipato kidogo sana ambacho kinawavunja moyo.