PDA

View Full Version : Ushindi wa Obama ni Somo kwa Tanzania



mwanakijiji
11-06-2008, 04:37 PM
USHINDI WA OBAMA NI SOMO KWA WATANZANIA!

Na. M. M. Mwanakijiji

Tukiuangalia ushindi wa Obama kama vile kutoka mbali, ni vigumu kuona jinsi gani ushindi huo unatoa somo kwa Watanzania. Lakini tukiusogelea kwa karibu na kuuchunguza kama Wanasayansi katika maabara tunaweza kuona vile vilivyofichika ambacho vinakuwa dhahiri kama vilivyokuzwa kwa darubini.

Kwa ushindi wake dhidi ya Seneta John McCain Rais Mteule Obama anakuwa ni Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kushika wadhifa wa juu kabisa katika utawala wa serikali ya nchi hiyo tangu taifa hilo liundwe zaidi ya miaka 230 iliyopita. Na kwa kufanya hivyo ameashiria mwanzo mpya wa mahusiano kati ya watu weupe na weusi wa nchi hiyo na bila ya shaka kuwafungulia milango watu weusi katika nchi nyingine ambapo wanajitahidi bado kukubalika na kupokelewa kama raia kweli wa nchi hizo.

Bila ya shaka watu wengi leo wataandika kwa kirefu maana ya ushindi huo kwa Wamarekani na ni kwa jinsi gani ushindi huo umemletea mtu mweusi hadhi na heshima anayostahili. Lakini tukitulia chini na kuanza kuangalia kwa karibu tunaweza kuona mambo yafuatayo kuhusu ushindi wa Obama na hasa tukiangalia mwelekeo wa kisiasa wa taifa letu la Tanzania. Kuangalia ushindi wa Obama na kutotumia mwanga wa siasa za nchi yetu kutatufanya tukose ujumbe ulio dhahiri wa ushindi huo.

Kwanza, Obama asingeweza kushinda bila kura ya watu weupe. Kuweza kuelewa hili nitatumia ushindi wa Nelson Mandela Afrika kusini mwaka 1994 alipochaguliwa kuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya kusini. Kule Afrika ya Kusini Mandela hakuhitaji hata kura moja ya mtu mweupe kushinda (ingawa najua alizipata nyingi tu) kwani watu weusi ni wengi zaidi kuliko weupe. Hata wazungu wote wangekubaliana kutompigia kura Mandela bado angeshinda.

Hilo lisingewezekana kwa Obama. Hata kama watu wote weusi wa Marekani wangempigia kura ya ndiyo Obama na watu weupe wakasema hapana Obama asingeweza kushinda (kwani watu weusi ni kama asilimia 12 tu ya wananchi wa Taifa hilo. Obama ameshinda uchaguzi huo kwa sababu watu weupe nao wamemkubali na kumuamini kuliongoza Taifa lao. Ni imani ambayo waliwanyima viongozi wengine weusi waliojaribu kusafiri njia hiyo. Waliwanyima kina Mch. Jesse Jackson, Mch. Al Sharpton na Dr. Alan Keyes. Hawakuwabali hao kimsingi kutokana na kuwaona kuwa hawakubaliki sana na siasa zao hazikuvuka mipaka ya kutosha kuwafikia watu weupe.

Hivyo, ushindi wa Obama umeonesha kuwa kuna kizazi cha Wamarekani ambao hatimaye wamefanya kile ambacho marehemu Dr. Martin Luther King Jr alikisema kuwa siku moja anayoiotoea njozi itakuja ambapo wana na mabinti wa Kimarekani ?watahukumiwa siyo kutokana na rangi yao bali kilichomo katika tabia zao?. Wamarekani walimuona Obama kuwa ni mtu mweusi (licha ya kwamba amechangia) lakini hawakumhukumu kutokana na rangi yake, kanisa alilokwenda, jina la kati la baba yake (Hussein), au kwa kitu kingine chochote ambacho Obama hakuwa na uchaguzi nacho. Walipiga kura wakimhukumu kwa kile ?kilichomo katika tabia yake?.

Jambo la pili ambalo tunaweza kuliona na kwa hakika ndicho kiini cha sherehe na furaha kwa watu weusi duniani kote ni ukweli kuwa Marekani ni Taifa ambalo limetoka katika historia ya utumwa, unyanyasaji wa mtu mweusi na hata hivi tunavyoandika bado kuna watu katika Taifa hilo ambalo hawaamini kuwa mtu mweusi ana hadhi, utu, na thamani kama binadamu mwingine yeyote yule.

Kuweza kuelewa hili ni kuona kile ambacho pia kulitokea Afrika ya Kusini ambapo watu weupe ilibidi baada ya Mandela kuchaguliwa wajikuta wakimpigia mtu mweusi saluti, na kusimama akiingia kwenye ofisi na kutoa heshima kwa Rais. Kuna watu wa Afrika ya Kusini ambao hata leo hii bado hawakubali kabisa kuwa watu weusi wa Afrika Kusini ni binadamu kama wengine.

Hivyo ushindi wa Obama unakata kama upanga mkali na kutuma ujumbe mzito kwa wale wote wanaohukumu watu kwa sababu ya rangi yao au kutokana na asili ya uzao wao. Obama anahusiana na Wamarekani weusi kwa rangi zaidi kuliko historia yao. Baba yake Obama hakuwa uzao wa kizazi cha watumwa waliopelekwa Marekani bali ni uzao wa baba wa Mkenya ambaye alienda huko masomoni na kumpenda mwanamke mzungu. Na ndiyo maana mwanzoni mwa kampeni zake watu weusi wengi walikuwa wanasita sita kumuunga mkono kwa kile walichokuwa wakidai kuwa Obama hakuwahi kuwa ?sehemu ya mapambano? (wakimaanisha mapambano ya kutafuta haki za watu weusi za miaka ya sitini)

Lakini pole pole Obama alianza kuzikosha nyoyo za watu mbalimbali na hasa waliokuwa wakosoaji wake. Aliwafanya wamkubali, wampokee kama mwenzao na hatimaye kumkumbatia kama mtoto wa Taifa lao kweli na zao la historia yao. Niliangalia jinsi Mch. Jesse Jackson akitiririka machozi usiku wa Jumanne akishuhudia kile ambacho wengi wao hawakutarajia kukioana katika maisha yao yaani mtu mweusi kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani. Ilikuwa ni uchungu (kwamba hakupata nafasi hiyo) lakini pia ni fahari kuwa anashuhudia kitu ambacho kilionekana hakitowezekana kwa karne moja ijayo!

Lakini jambo la tatu ambalo naamini linatokana na hayo mawili ya kwanza ni kuwa ushindi wa Obama unatuma ujumbe kwa mataifa mbalimbali duniani hasa yale yenye raia wenye asili ya uzao wa nchi nyingine au bara jingine. Ni hiki ndicho ninachoona Watanzania hatuna budi kujipima kweli kweli kama tunaweza kufanya kilichofanywa na watu weupe wa Marekani kwa wao kumchagua mtu mweusi.

Hivi unaweza kujiona ukiwa tayari kumpigia kura Mtanzania mwenye asili ya Kiasia ambaye amejidhihirisha kuwa anaipenda Tanzania kweli na anafanya kila liwezalo kuitumikia nchi yake (siyo kuitumia kutengeneza utajiri tu)? Je tuko tayari kumpigia kura Mtanzania mwenye asili ya Uarabuni ambaye tumemkubali kweli kuwa ni mzalendo halisi? Katika hapa unaweza kupata kigugumizi.

Ni rahisi kwa wengi wetu kufurahia walichofanya wazungu kwa kumchagua mtu mweusi ambaye wamemhukumu kwa tabia yake kuliko sisi wenyewe kuangalia kama tunaweza kumchagua mtu ambaye ana asili ya bara jingine au amechangia damu (kama Obama) kuliongoza Taifa letu. Wengi wetu ndani yetu tunaweza kujisikia kigugumizi kwa sababu hatuko tayari kuona ?Mhindi? au ?Mwarabu? anapata nafasi ya kuliongoza Taifa letu kwa sababu moja tu nayo ni rangi yake.

(inaendelea chini)

mwanakijiji
11-06-2008, 04:38 PM
Toka Juu

Tunaposhangilia ushindi wa Obama hatuna budi kujipepeleza mioyoni mwetu kwamba tunaweza kushinda unafiki wetu, woga wetu, hukumu zetu n.k na kumpa Mtanzania yeyote yule (awe Mwekundu, Mweupe, wa Bluu wau Mweusi) nafasi sawa ya kuitumikia nchi yake.

Ninalisema hili nikiwa na kumbukumbu nzuri ya jinsi gani ndani ya CCM ulichezwa mchafu wa kumnyima nafasi Dr. Salim kwa kitu kimoja tu nacho ni ?Upemba? wake na wengine walitumia viapo kusema kuwa ?Mwarabu? hatotawala Tanzania. Wengi wetu tunakumbuka kwa fahari utumishi wa Dr. Salim kwa Taifa lake lakini pale ilipotokea apate nafasi ya kugombea uongozi wa yake tulimkana kwa kuangalia vitu ambavyo hana uwezo wa kuvibadilisha hata kama akitaka. Tuliangalia rangi yake, nywele zake na asili yake na kusema ?si mwenzetu?.

Lakini ni sisi hawa hawa ambao leo hii na sehemu nyingine mwishoni mwa juma tutaandaa tafrija za kufurahia watu weupe kumchagua mtu mweusi lakini tunaona hatupigi kelele tunapoona vitendo vya kibaguzi vikitokea dhidi ya Watanzania wenzetu kwa sababu tu tunaona kama wanastahili vile.

Leo hii Tanzania tumepewa somo, ni somo ambalo kwa hakika hatuna budi kulifuzu. Wananchi wa Botswana walimchagua Rais wao ambaye mama yake ni mzungu na wanaishi na kuendelea kusonga mbele. Je Tanzania tuko tayari kuchagua Mtanzania ambaye amechangia damu na watu wa mabara mengine? Je tutaendelea kuwaona Watanzania wenzetu wenye mapenzi ya kweli kwa Taifa letu kuwa ni wageni bado kwa sababu tu ya rangi yao?

Lakini pia ujumbe mkubwa zaidi unawaendea Watanzania ambao wana asili ya mabara mengine au ambao wamechangia damu na watu wa mabara wengine. Hamuwezi kuishia kuwa mashabiki wa michezo tu na kutoa misaada ya michezo. Haiwezekani muendelee kuegemea chama tawala tu kwa sababu ya kile ambacho mnaamini wanawapatia. Hamuwezi kuendelea kukaa pembeni wakati wa raha na inapotokea shida mnakuwa wa kwanza kwenda ?Canada? au ?Uarabuni? mkisubiri mambo yatulie.

Wakati wenu umefika na ninyi watoto wenu wajiunge katika sekta nyingine za Taifa letu, sijui ni nani kati yenu yuko tayari kumpa nafasi mtoto wake kuwa Afisa wa Polisi akahenyeke kule CCP? NI wangapi watoto wenu wamesoma na kuelemika lakini hakuna anayetaka kuwa mpiganaji wa JWTZ au vikosi vingine?

Wakati wenu umefika wa kuanza kufanya mazungumzo katika sebule zenu na watoto wenu na kuwatia moyo kuitumikia nchi yao na kutokuwakatisha tamaa pale watakapotaka kuwa katika nafasi na kazi ambazo mnaziona ?siyo zenu?. Muwatie moyo watoto wenu kuipenda Tanzania na kudai kwa haki kabisa kuwa hapa ndipo nchini mwenu.

Na ndio maana binafsi nilichukuzwa na kukerwa wakati maneno ya kibaguzi yaliporushwa na baadhi ya watu ambao leo wanamshabikia Obama dhidi ya Ritchie yule binti mwenye asili ya Uhindi aliyeshinda Umiss Tanzania. Nakumbuka jinsi watu walivyosema kuwa ?hastahili kuwa Miss Tanzania? kwa vile tu alikuwa na rangi tofauti. Kile kiliniuma sana kwa sababu najua na sisi tunaweza kuwa zaidi ya hofu zetu na woga wetu. Tunaweza kusimama na kufanya kile ambacho ni cha kibinadamu kweli na siyo cha ?kizungu?.

Ndugu zangu, wakati umefika wa kuamini kuwa kama kweli tunataka kufika kwenye ile nchi ya ahadi, kama kweli tunataka kujenga Taifa la watu walio huru kweli na sawa, hatuna budi kuweka pembeni visingizio vyetu, woga wetu, chuki zetu, na hisia zetu kinyume dhidi ya watu wengine kwa sababu ya rangi zao au asili yao. Tuwe tayari kuwapa nafasi ya kuwasikiliza hoja zao na kuwapima kwa matendo yao.

Tukifanya hivyo kweli tutaweza kusema kama alivyosema Baba wa Taifa miaka ile ?Sisi hatutukuzi rangi bwana, tunatukuza mtu?. Leo hii hata hivyo naamini tunatukuza vyote viwili. Leo hii tunaona fahari kuwa mtu mweusi ameheshimika. Tunaona fahari kuwa mtu mweusi amepewa nafasi. Tunaona fahari kuwa mtu mweusi naye anaweza! Tunaona fahari kuwa katika ulimwengu wetu huu, tutafanikiwa pamoja au pamoja tutaangamia.

Tunaposherehekea na kufurahia ushindi wa Obama, tujiulize, je itakapotokea Tanzania kwa kiongozi mwenye asili ya nje ya bara hili au aliyechangia damu na watu wa nje ya bara hili, tuko tayari kumpa nafasi hiyo mtu huyo au tutaongozwa na woga wetu, chuki zetu, husuda zetu, au visingizio vyetu? Tukiweza kusema kuwa ?tuko tayari kushinda vitu hivyo na kumpa mtu huyo nafasi? basi na sisi tutaweza kweli siku moja kufurahia kwa pamoja utu wetu, umoja wetu, udugu wetu , na kwa hakika hatima ya pamoja ya Taifa letu tulipendalo.

Ndiyo tunaweza, Yes We Can!

Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com

Ach-F
11-07-2008, 11:14 PM
Waliomkana Salim ni Wa-zanzibar kwani kwao wako karibu zaidi na waarabu kuliko Waafrika lakini hawakawii kukimbilia nchi kama UK, USA na kwingineko hawataki kukimbilia uarabuni kisa Sharia Law hawaiwezi lakini hawaishi kuchokonoa chokonoa kila kukicha. Utafikiri wamesahau jinsi Falasha's walivyohamishwa kwenda Israel na kugundua kwamba hawakubaliki. Je wao watakimbilia wapi kama siyo Western world ambayo kila uchwao wanaisaga?

Hata SA ni tatizo hilo hilo tu Zuma ambaye ni Mzulu pamoja na kuvurunda wakati akiwa makamu wa rais bado anaitingisha nchi wakati uwezo wa kuendesha nchi hana. Je, ni nini itakuwa hatma ya SA. Another Zimbabwe?