PDA

View Full Version : Haya Mafuriko Dar yana mwisho kweli?



mwanakijiji
11-06-2008, 04:57 PM
Theopista Nsanzugwanko
Daily News; Wednesday,November 05, 2008 @21:15

Mvua kubwa iliyonyesha jana alfajiri Dar es Salaam, imesababisha maafa mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakazi wa maeneo ya Mbagala kuchelewa kufika katikati ya mji baada ya daraja la Mzinga kujaa maji.

Wakazi wa maeneo hayo na wale wa maeneo ya Kongowe na kwingineko wanaotumia Barabara ya Kilwa kufika katikati ya mji, walilazimika kuzunguka hadi Kigamboni na kuvuka kwa pantoni.

Kutokana na hali hiyo, kulikuwa na msongamano mkubwa wa magari na abiria katika kivuko cha Kigamboni na kusababisha foleni kubwa kwa waliokuwa wanawahi kufika mjini.

Mkazi wa Mbagala, Hassan Kiloi, aliyekuwa miongoni mwa wamiliki wa magari yaliyokwama aliitaka serikali kuihimiza kampuni inayojenga Barabara ya Kilwa kumalizia daraja jipya la Mzinga mapema ili kuwahakikishia usafiri wakazi wanaoishi wa maeneo hayo.

Alisema bila kufanya hivyo hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu kutokana na kwamba daraja hilo limeshaelemewa na mvua ndiyo kwanza inaanza. “Hatuna budi hatua za haraka zichukuliwe mapema kutokana na kuwa mvua hizi za vuli ndiyo zinaanza na daraja lile tayari limeelemewa bila hivyo sisi wakazi wa Mbagala tutaendelea kuchelewa makazini kila siku,” alisema.

Hadi kufikia jana mchana, magari yalikuwa yakigoma kwenda maeneo ya Mbagala kwa kuhofia kushindwa kurudi kwa kupitia njia hiyo ikiwa mvua ingenyesha na daraja hilo kujaa maji. Wakati wakazi hao wakichelewa kufika katikati ya mji, ukuta wa nyumba moja umebomoka huku nyumba nyingine nne zikiwa kwenye hatari ya kubomoka katika eneo la Mbagala Misheni.

Jana, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilisisitiza tena onyo lake kwa wakazi wa mikoa ya pwani kwamba wajihadhari na mvua hizo za vuli, kwani utabiri unaonyesha kuwa kutakuwapo na mafuriko kutokana na mvua kutegemewa kwa kiwango cha juu.


Ikinyesha mvua kidogo tu Dar basi inakuwa balaa. Miaka nenda miaka rudi kuna mafuriko ya kushangaza yanatokea kila inaponyesha mvua kubwa na kuonesha jinsi gani miundo mbinu yetu ya kusafirisha maji machafu (drainage system) bado ni dhaifu na hakuna dalili ya dhati ya kukabiliana na tatizo hilo. Je kuna njia kweli ya kuweza kubadilisha hili au ndio tukubali yaishe?

http://www.globalpublisherstz.com/uploads/posts/thumbs/1225891004_mvua2.jpg