PDA

View Full Version : Tunda hili mimi sili



mwanakijiji
11-06-2008, 06:15 PM
Ninaapa kwa mababu, na mizimu ya kikwetu,
Natoa leo sababu, roho yangu iwe kwatu,
Ni hili lilonisibu, kunifedhehesha utu,
Walilokula wengine, tunda hili mimi sili!

Nimepewa tunda hili, la bure sikununua,
Ni moja siyo mawili, hilo nililichukua,
Nina hamu kwelikweli, alonipa kang'amua,
Walilokula wengine, tunda hili mimi sili!

Alonipa kasifia, kasema tunda ni tamu,
Kanipa kaniambia, wengine wanalo hamu,
Hakuna alowahia, kulila tunda adhimu,
Walilokula wengine, tunda hili mimi sili!

Ndipo nikashangilia, wakijiji nina ngeke,
Tunda nililoshikia, kama vile libeneke,
Hamu nikalishakia, nyumba hima nifike,
Walilokula wengine, tunda hili mimi sili.

Kufika pale nyumbani, sahani nikaandaa,
Kulitoa mfukoni, na kisu kukiandaa,
Nikapigwa tafurani, nikabaki kushangaa,
Walilokula wengine, tunda hili mimi sili!

Tayari limeshang'atwa, upande huu na ule,
Kwa kisu lilishakatwa, ati na miye nilile,
Wanadhani wa kuletwa, kumbe nami yule yule,
Walilokula wengine, tunda hili mimi sili!

Tunda hili sasa chungu, kuonja miye sitaki,
Nataka lililolangu, si tunda la kinafiki,
La kwangu la peke yangu, lenye utamu wa haki,
Walilokula wengine tunda hili mimi sili!

M. M. Mwanakijiji (Sauti ya Kijiji)

Mama
11-07-2008, 10:38 PM
Hodi hodi uwanjani, polepole naingia
mliopo kina nani, nyumbani nakaribia
Naomba nipokeeni, kwa vifijo shangilia
Hongera Mwanakijiji, Forum kufungulia

Wasema tunda hulili, wenzio wamepitia
Tunda hilo si asili, mwenyewe walihofia
si tamu kama asali, wengine wamepitia
sijihini nafsiyo, kama hutaki usile.

Mpita Njia
11-09-2008, 10:55 AM
He mama, kumbe na wewe wamo, hongera sana

magoma
11-26-2008, 05:19 PM
Tunda hili Chungwa au chenza?? kama Chenza sawa lakini kama in Chungwa NOMA:

mwanakijiji
09-26-2009, 08:19 PM
Tunda hili Chungwa au chenza?? kama Chenza sawa lakini kama in Chungwa NOMA:

umenichekesha kweli