PDA

View Full Version : Jaji Mkuu atoa madai mazito



mwanakijiji
12-14-2008, 02:30 AM
Jaji Mkuu: Baadhi ya mawakili ni matapeli(Nipashe)

2008-12-13 13:47:27
Na Joseph Mwendapole na Hellen Mwango

Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, amesema baadhi ya mawakili ni matapeli na wamekuwa wakiwatapeli wateja wao kwa kula njama na upande wa wapinzani wa wateja wao.

Kadhalika, amewataka mawakili kutowatetea wateja wao ambao hukiri kutenda makosa yanayowakabili mahakamani.

Akizungumza jana kwenye hafla ya kuwapa vyeti mawakili wapya 64 wa kujitegemea, Jaji Ramadhani alisema baadhi ya mawakili wamekuwa ndumila kuwili na kwamba huo ni usaliti na utapeli.

``Hapa kuna suala la uaminifu kuhusu fedha za wateja wenu... Yapo malalamiko kuwa mawakili wachache wanajinufaisha kwa fedha za wateja wao na bila kumung`unya maneno natamka kuwa huo ni wizi,`` alisema.

Alisema mawakili wana wajibu kwa wateja wao na inawapasa wawe waaminifu kwao.

Kuhusu washtakiwa wanaokiri makosa, Jaji Ramadhani alisema kama mshtakiwa anakiri kosa, wakili anapaswa kujaribu kupata afueni ya adhabu na ni mwiko kusimama kidete na kudai kuwa mteja wake hana hatia.

Alisema wakili anao wajibu kwa dhamira yake na kama anaona dhamira yake haimruhusu kushiriki katika kesi fulani basi asijilazimishe bali aiache hata kama itamkosesha donge nono.

Alisema Tanzania kwa sasa ina mawakili 1,133 lakini mawakili ambao wanafanya kazi ni 761 tu ambao wamehuisha leseni zao mwaka huu.

Alisema Jiji la Dar es Salaam lina mawakili 704 na kati ya hao mawakili 102 hawajahuisha leseni zao na kwamba mawakili 31 wamepeleka maombi kwa Jaji Mkuu ya kuruhusiwa kuhuisha leseni zao.

Aidha, alisema ni aibu kuona mawakili 71 bado hawajapeleka hata maombi ya kuruhusiwa kuhuisha leseni zao.

``Hivi wakili ambaye anakuwa mzembe kuhuisha leseni yake ambayo ndiyo inampatia maslahi atakuwa makini kuhusu maslahi ya mteja wake?`` Alihoji Jaji Ramadhani.

Alisema kwa mwaka ujao wakili atakayechelewa kuhuisha leseni yake ataachwa asote mwaka mzima kabla ya kibali cha Jaji Mkuu kupatikana.

Miongoni mwa mawakili wa kujitegemea walioapishwa jana na Jaji Mkuu ni pamoja na Joseph Holle wa Takukuru aliyewasomea mashitaka mawaziri wandamizi, Basil Mramba na Daniel Yona.

Mawaziri hao wa zamani walisomewa mashitaka 13 ya kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 11.7 kwa kutumia vibaya madaraka yao.

Wengine walikuwa waendesha mashitaka wa serikali na askari polisi kadhaa.

Ach-F
12-14-2008, 06:21 PM
Mahakama Tanzania zimekuwa mstari wa mbele katika kile ambacho tunakiona kuwaonea aibu watuhumiwa au kutokufuata sheria hasa watuhumiwa hao wakiwa kama Mramba, et al. Tuliona yaliyotokea kwa Dito lakini Mwenyezi Mungu si Athumani. malipo ni hapa hapa duniani majaji acheni mafisadi wafie jeli kwa nini mnawaonea huruna? Siku yenu inakuja.