PDA

View Full Version : News Alert: Wakamatwa wakitafuta viungo vya Albino



mwanakijiji
12-16-2008, 11:08 PM
Watumishi wawili wa kampuni ya Madini ya Burega Mineral and Export ya JIjini Dar wamekamatwa mkoani Rukwa wakiwa katika jitihada za kutafuta viungo vya Albino. Watumishi hao Bw. Chacha Samwel na ndugu yake Joseph Chacha wamekamatwa baada ya wananchi waliochoshwa na vitendo vya mauaji ya Albino kutoa taarifa Polisi mara ndugu hao wawili walipoanza kuulizia jinsi ya kupata viungo hivyo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa Bw. Isuto Mantage watumishi hao walikuwa wakitafuta viungo hivyo kwa kile walichodai kutekeleza maagizo ya Mkurugenzi wa Kampuni hiyo ambaye jina lake halikutajwa ili kutoharibu uchunguzi.

Watumishi hao waliingia Rukwa Jumamosi wakiwa wanatokea Dodoma.

Karibu mwaka mmoja na zaidi kumeibuka wimbi la mauaji ya watu wenye matatizo ya rangi ya ngozi (Maalbino) kwa kile kinachotajwa kuwa ni kutokana na imani za kishirikina. Inadaiwa kuwa waganga wa kienyeji wamekuwa wakitaka viungo vya albino kama mojawapo ya vitu vinavyotakiwa ili kuweza kumfanikisha mtu kwenye biashara yake ya madini.

Hadi hivi sasa Maalbino zaidi ya 30 wameuawa na viungo vyao kunyofolewa ili kukidhi biashara hiyo haramu ya viungo vya binadamu.