PDA

View Full Version : CCM kutotumia Helikopta Mbeya



mwanakijiji
12-22-2008, 04:42 PM
Kamati Kuu yadai ni matumizi mabaya ya fedha


na Edward Kinabo (Tanzania Daima)


ZIKIWA zimebaki siku saba kabla ya kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Mbeya Vijijini kuanza, Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC), imepiga marufuku matumizi ya helikopta katika kampeni hizo kama ilivyokuwa katika Jimbo la Tarime.

Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya CC iliyokutana jana jijini Dar es Salaam chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilisema kuwa matumizi ya helikopta katika jimbo hilo lililokuwa chini ya Mbunge wa CCM, marehemu Richard Nyaulawa, aliyefariki dunia, ni matumizi mabaya ya fedha.

Kwa mujibu wa habari hizo, CCM imepanga kutumia zaidi ya sh milioni 700 lakini gharama zote zisizidi sh bilioni moja.

?Tarime CCM tulitumia zaidi ya sh bilioni mbili hadi kuagiza helikopta mbili siku za mwisho na bado tukashindwa, safari hii hatutaki tena kutumia gharama hiyo,? kilisema chanzo chetu cha habari kutoka ndani ya kikao hicho.

Suala la gharama za uchaguzi Tarime, liliwahi pia kuzungumziwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na kupendekeza namna nyingine bora ya kujaza nafasi zinazoachwa wazi na viongozi wa kuchaguliwa ili kuepuka gharama.

Katika hatua nyingine, CCM imetaja majina ya viongozi na makada wake watakaongoza kampeni katika uchaguzi huo.

Baadhi ya viongozi hao ni Makamu mwenyekiti mstaafu, John Samwel Malecela, Makamu Mwenyekiti wa sasa, Pius Msekwa, Mwenyekiti wa UVCCM, Yusuf Masauni na makamu wake, Beno Malisa, Nape Nnauye na Luteni Yusuph Makamba, ambaye atatumika kama mshauri na si kiongozi wa kampeni hizo kama ilivyokuwa Tarime.

Katibu wa CCM wa itikadi na uenezi, John Chiligati, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho, jijini Dar es Salaam jana, alisema chama hicho kitanzindua kampeni zake Januari 4, 2009, katika uzinduzi utakaofanywa na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Ali Hassan Mwinyi.

Alisema baada ya uzinduzi huo, kampeni za kumnadi mgombea huyo zitakuwa zikiendeshwa na kamati ya siasa ya mkoa huo, na ofisi ya Katibu Mkuu wa chama, iliyo chini ya Makamba, itakwenda Mbeya kutekeleza wajibu wa kuziwezesha kampeni hizo, kwa kutoa ushauri utakaokihakikishia ushindi chama hicho.

Ufafanuzi huo wa Chiligati ulitokana na swali aliloulizwa kuhusu nini utakuwa wajibu wa Makamba katika kampeni hizo, hasa baada ya chama hicho kushindwa katika uchaguzi mdogo uliopita wa Jimbo la Tarime, ambapo alijibu kama ifuatavyo:

?Si kweli kwamba Makamba alisababisha CCM ishindwe Tarime. 2005 tulishindwa Tarime, Makamba alikuwepo? Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni. Kile kiti kilikuwa cha CHADEMA sisi tulikuwa tunajaribu tu lakini hatukufanikiwa, tutakwenda tena uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, labda watakuwa wamebadili mawazo watatuunga mkono.

?Kampeni ya uchaguzi Mbeya itafanywa na kamati ya siasa ya mkoa ?wilaya na sisi kutoka makao makuu tutakwenda kule kuwa kama ?facilitators? (wawezeshaji), jukumu letu kubwa litakuwa ni kushauri hapa na pale na kuangalia mwenendo wa kampeni?mikakati ili tushinde.?

Alipoulizwa kwanini kampeni hizo ziendeshwe na kamati ya siasa na Makamba awe mshauri tu, wakati katika uchaguzi mdogo wa Tarime Makamba alikuwa kinara wa kumnadi mgombea wa CCM licha ya kuwepo kamati ya siasa ya Mkoa wa Mara, alisema:

?Siyo kwamba hatakwenda Mbeya?hapana, atakwenda Mbeya. Yeye ndiye Katibu Mkuu. Kwa katiba yetu yeye ndiye mkurugenzi wa uchaguzi, kwa hiyo hawezi kuacha kwenda Mbeya kwa sababu kampeni zote zipo chini yake. Lakini nimesema yeye atakuwa ni facilitator (mwezeshaji), ambaye atakuwa akishauri na kuhakikisha mambo yote yanakwenda sawa ili tupate ushindi. Kamati ya siasa ndiyo itafanya kampeni zote na tayari wameshajipanga, kuanzia kwenye nyumba kumi kumi na matawi.?

Akimtangaza mgombea wa CCM kwa ajili ya uchaguzi huo, alisema CC ya chama hicho, imemteua Luckson Ndaga Mwanjale (58), kuwa mgombea wa kiti hicho, baada ya kupitia sifa za wagombea wote tisa walioomba kuteuliwa.

Alielezea sifa zilizomfanya Mwanjale kuteuliwa na chama hicho kwamba ni kuwa na stashahada ya elimu ya ufundi, ameshika nafasi mbalimbali katika uongozi wa CCM, ni katibu wa dhehebu lake la Uinjilisti na ameongoza katika kura za maoni.

Alisema, Mwanjale aliyepata kura 435, aliwashinda wagombea wengine wanane, akiwamo, Allan Mwaigaga, aliyepata kura 259, Andrea Sayile (229), Generali Robert Mboma (164), Diovita Diyame (162), Petro Mwashusha (28), Flora Mwalyambi (26), Michael Mponzi (23) na Maria Mwambanga aliyepata kura 19.

Alipoulizwa kwanini CCM imempitisha mgombea huyo ambaye kumbukumbu zinaonyesha kuwa alishaomba kuteuliwa na chama hicho kuwania nafasi hiyo hiyo mara tatu, lakini hakuteuliwa kwa kuwa hana sifa za kuwa mbunge, alisema kuwa katika chaguzi zilizopita ukiwemo uchaguzi wa mwaka 2005, mgombea huyo alijitokeza lakini hakupitishwa kwa sababu alikuwa hajakomaa na ndiyo maana kura zake hazikutosha.

Alisema kwa sasa wanaamini kuwa mgombea huyo ameshakomaa na ndiyo maana kura zake zimetosha, kwa kuweza kuwazidi wanachama wengine wanane wa CCM walioomba kuteuliwa kuwania kiti hicho.

Katika mkutano huo, Chiligati pia alitoa taarifa kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (CCM), Mkoa wa Tabora, baada ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho kilichoketi Novemba 11, 2008 kuagiza nafasi hiyo itangazwe upya kutokana na kubakia mgombea mmoja tu.

Alisema baada ya nafasi hiyo kutangazwa upya walijitokeza wanachama wanne, ambapo kati yao, walioteuliwa kugombea nafasi hiyo ni Mwasiti Badru Ngesi, Tatu Mussa Ntimizi na Lucy Kayanda Sekasua.

Aidha, alisema kamati kuu imempongeza Yusufu Hamad Masauni kwa kuchaguliwa na mkutano mkuu wa taifa wa UVCCM uliofanyika Dodoma hivi karibuni kuwa mwenyekiti mpya wa taifa wa jumuiya hiyo, na Beno Malisa kuwa Makamu Mwenyekiti wake.

Uchaguzi mdogo wa Mbeya Vijijini, unatarajiwa kufanyika Junuari 25 mwakani.

Mpita Njia
12-22-2008, 06:07 PM
Nashindwa kukielewa anachotaka kusema Chiligati-kwamba matumizi ya helikopta ni ufujaji fedha au hawazipeleki helikopta Mbeya kwa sababu hazikuwasaidia Tarime? Najiuliza hivi kwa sababu kama sababu ingekuwa ni ufujaji wa fedha, wangelielewa hili tangu baada ya uchaguzi wa Kiteto, lakini walipoenda tarime walitumia helikopta! Oh! labda kwa sababu JK alikemea baada ya uchaguzi wa Tarime ndio wameghairi kupeleka Mbeya? Au kwa sababu wana uhakika wa kushinda Mbeya hata wasipotumia helikopta?

mwanakijiji
12-22-2008, 07:12 PM
Nashindwa kukielewa anachotaka kusema Chiligati-kwamba matumizi ya helikopta ni ufujaji fedha au hawazipeleki helikopta Mbeya kwa sababu hazikuwasaidia Tarime? Najiuliza hivi kwa sababu kama sababu ingekuwa ni ufujaji wa fedha, wangelielewa hili tangu baada ya uchaguzi wa Kiteto, lakini walipoenda tarime walitumia helikopta! Oh! labda kwa sababu JK alikemea baada ya uchaguzi wa Tarime ndio wameghairi kupeleka Mbeya? Au kwa sababu wana uhakika wa kushinda Mbeya hata wasipotumia helikopta?

sasa wakishindwa Mbeya Vijijini si Makamba anaweza kuwacheka na kusema "tungetumia helikopta na sisi"...