View Full Version : Mkapa aondolewe Kinga?
mwanakijiji
12-22-2008, 04:49 PM
Kama kuna kiongozi ambaye watu wangependa ajibu maswali kadha wa kadha kuhusu vitendo vya kifisadi ni aliyekuwa Rais wetu Bw. Benjamin Mkapa. Hata hivyo kujibu tu haitoshi isipokjuwa pawe pia na uwezekano wa kumfungulia mashtaka.
Hata hivyo kuna mjadala katika medani za kisheria kama Mkapa anaweza kufunguliwa mashtaka au la kutokana na kuwahi kuwa na kinga ya kutofunguliwa mashtaka alipokuwa Rais.
So, la kwanza kabla ya kufungua mashtaka ni lazima tujiulize kama upo ulazima wa kumvua kinga yake au tupate majibu yake bila ya tishio la mashtaka?
Ach-F
12-24-2008, 02:54 AM
Hawa wahujumu wa uchumi wanachekewa badala ya kuwachukulia hatua kali ili iwe fundisho kwa akina Jakaya na kundi lake.
Mpita Njia
12-24-2008, 03:08 PM
Hapana, asiondolewe wala asishitakiwe.
Kinga iliyopo ni ya kikatiba kwa mambo ambayo rais atayafanya chini ya mamlaka yake kama rais. nadhani walioiweka walitaka kumfanya rais asiwe na hofu wakati atakapokuwa anafanya maamuzi ambayo karibu yote yana madhara kwa upande mmoja au mwingine.
Lakini wapo wanaolijadili hili waki-base kwenye ushiriki wa Mkapa kwenye Kiwira. kwangu mimi hilo si suala la kuondoa kinga kwa sababu halihusiani kabisa na masuala ya kinga ya uraisi, aliyafanya maamuzi haka kama mtu binafsi, na ndio maana hata kwenye fomu akajaza kuwa yeye ni mjasiriamali. katika hilo pia sioni umuhimu wa kuiondoa kinga kwa sababu hiyo kinga haizuii yeye kushitakiwa kwa suala kama hilo
mwanakijiji
12-28-2008, 09:53 PM
Mussa Juma, Karatu (Mwananchi)
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willbrod Slaa amesema anajiandaa kuzungumzia suala la Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kushtakiwa kwa makosa anayodaiwa kufanya akiwa Ikulu katika bunge lijalo.
Dk Slaa aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa atafanya hiyo ili kuondoa upotoshaji wa suala hilo ambayo imeanza kufanywa na baadhi ya wasomi nchini.
Alisema baadhi ya wasomi nchini wameanza kupotosha jamii kuwa Mkapa hawezi kushtakiwa mpaka bunge limwondolee kinga.
Dk Slaa alisema Mkapa anaweza kushtakiwa bila ya kuondolewa kinga yake.
Alisema anashangaa wasomi nchini kuendelea kuipotosha jamii juu ya suala la kufunguliwa mashitaka Rais mstahafu, na anakusudia kuliweka bayana suala hilo tena katika bunge lijalo.
"Katika bunge lililopita katika hotuba ya Waziri Mkuu, niliwahi kulisema hili kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria na lazima tutofautishe mamlaka ya rais na mtu binafsi na hili nitalieleza tena bunge,"alisema Dk Slaa ambaye kitaaluma ni mwanasheria.
Alisema matendo ambayo Rais hawezi kufunguliwa kesi mpaka aondolewe kinga ni yale tu ambayo aliyafanyaka kama Rais, katika madaraka yake kisheria kama kuwaachia huru wafungwa, kuidhinisha sheria na masuala mengine yaliyoanishwa kwenye
katiba ya nchi.
Dk Slaa alisema masuala kama ya Rais Mkapa kufanya biashara akiwa Ikulu hayahitaji kuwa na kinga ili ashitakiwe kwani ameyafanya nje ya mamlaka ya rais aliyopewa.
"Watu wengi hawapendi kusoma, ni wavivu. Jambo hili lipo wazi kabisa na nashangaa wasomi wetu ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) kudai eti kumshitaki mkapa ni kuvunja katiba,"alisema Dk Slaa.
Alisema kinachoendelea hivi sasa hapa nchini ni kukosekana kwa usimamizi mzuri wa sheria na viongozi wenye kauli ya mwisho juu ya masuala yenye maslahi ya Taifa.
"Ni aibu Waziri Mkuu anazungumza kuwa hakuna aliye juu ya sheria, Takukuru wanadai hawamchunguzi Mkapa kwani mpaka aondolewe kinga, haya ni mambo ya ajabu,"alisema Dk Slaa.
Dk Slaa ambaye ndiye alikuwa wa kwanza kutoa hadharani tuhuma nzito dhidi ya Mkapa kwa kuanzisha kampuni akiwa Ikulu na kujiingiza katika biashara mbalimbali, alisema umefika wakati sheria kufuatwa bila kujali nafasi za wahusika.
Akizungumzia vita dhidi ya ufisadi, alisema Chadema itaendelea kushinikiza watuhumiwa wote kufikishwa mahakamani hadi wamalizike.
"Sisi ndio tumeanzisha huu mjadala hakuna wa kuufunga sio Makamba (Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf) wala Chiligati (Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, John) na tutapiga kelele hadi watuhumiwa wote wakamatwe,"alisema Dk Slaa.
Dk Slaa aliwataka Watanzania kwa ujumla wao kusimama kidete na kuliombea Taifa lao kwani wasipoamka na kutetea rasilimali zao nchi yao itamalizwa na mafisadi na siku zijazo hali itakuwa mbaya zaidi.
"Tukiendelea hivi taifa linaporomoka ni lazima tuungane tuwaondoe mafisadi na tunakwenda kwenye uchaguzi Mbeya Vijijini mshikamano wetu ni muhimu kuing?oa serikali ya CCM,"alisema Dk Slaa.
Akizungumzia kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda hivi karibuni kuhusu kuzuia magari ya kifahari, alisema jambo hili ni kuwadanyanga wananchi kwani serikali haina nia ya dhati kuacha kutumia magari hayo.
"Anasema wanazuia wakati kuna magari 700 wamenunua kweli hapa kuna umakini na thamani ya gari moja ni zaidi ya Sh100 milioni na tunaendelea kudai nchi ni masikini,"alisema Dk Slaa.
mwanakijiji
12-29-2008, 05:13 PM
Lipumba: Mkapa hana kinga (tanzania daima)
na Asha Bani, Masasi
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, hana kinga, hivyo anastahili kushtakiwa kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari walioko kwenye msafara wa ziara ya kukagua uhai wa chama chake mjini Masasi.
Profesa Lipumba alisema kutokana na kifungu namba 46(3) cha katiba ya nchi, Mkapa anastahili kushtakiwa kama ushahidi wa kosa litabainika.
Alisema maovu mengi yalifanyika wakati wa utawala wake, hivyo kuna haja ya kuangalia kwa makini na kufanya uchunguzi endapo itagundulika kuna mkomo wake katika kuliingizia taifa hasara kutokana na mikataba mibovu; na ubinafsishaji usiofuata taratibu, anastahili kushtakiwa.
Alisema kifungu hicho cha sheria kinasema kinga ya rais ni pale ambapo amefanya jambo lililofuata taratibu za nchi.
?Kwa mfano, kama sehemu ina fujo, halafu Rais ameamuru jeshi kwenda kutuliza na kuua, hapo rais hatashtakiwa, lakini si kuipa nchi hasara, kuliingiza taifa kwenye umaskini kwa kushiriki kwenye makosa ya ufisadi na rushwa inabidi ashtakiwe!
?Rais hayuko juu ya sheria na kinga yake ni sheria, hivyo naye achunguzwe endapo itabainika kama alihusika kwenye rushwa katika ununuzi wa rada ambao umeliingizia taifa hasara ya sh bilioni 40, basi hana budi kushtakiwa,? alisema.
Profesa Lipumba alisema hakuna haja ya kuumiza kichwa kwani katika utawala wa Mkapa wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ulifanyika kwa kuchota mabilioni ya fedha na kutafunwa na wachache.
Katika hatua nyingine, chama hicho kimesema Mkapa haheshimu haki za binadamu kama ilivyodaiwa na Askofu wa Kanisa la Anglikan, John Ramadhan, katika ujumbe wake wakati wa mkesha wa ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Mkunazini, mjini Zanzibar.
Taarifa iliyotolewa na Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani jana, ilisema kumbukumbu za utawala wa Rais Mkapa zinaonyesha kulitokea mauaji ya kutisha yaliofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama dhidi ya raia wasiokuwa na hatia visiwani Zanzibar.
?Wakati mauaji hayo yanafanyika si tu Rais Mkapa alikuwa ndio Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, bali pia alithubutu kuwapandisha vyeo askari waliohusika na mauaji hayo,? alisema Biman.
Alisema CUF haikubaliani na kauli ya askofu huyo kuwa Mkapa alikuwa kiongozi aliyeheshimu utu wa mtu wa kuishi kwa vile hakupitisha adhabu hata moja ya kifo katika utawala wake licha ya watu kadhaa kupatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.
Alisema kwamba wananchi wa Zanzibar kila Januari 26 na 27 wamekuwa wakiadhimisha kumbukumbu ya mauaji ya kutisha yaliofanywa na vikosi vya ulinzi na usalama chini ya amiri Jeshi Mkuu Benjamin Mkapa.
Akitoa mahubiri katika ibada ya mkesha wa sikukuu ya Krismasi katika Kanisa la Anglikana Mjini Zanzibar, Askofu alisema Rais Mstaafu, Mkapa, katika uongozi wake atakumbukwa kwa kuheshimu haki ya mtu ya kuishi kwa vile hakuidhinisha adhabu ya kifo licha ya watu kadhaa kupatikana na hatia wakati wa uongozi wake.
mwanakijiji
12-29-2008, 07:03 PM
Sitta: Nitapokea hoja binafsi dhidi ya Mkapa
Jackson Odoyo (Mwananchi)
SPIKA wa Bunge la Muungano, Samwel Sitta ameongeza chachu katika mjadala wa kumuondolea kinga Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, baada ya kueleza kuwa yuko tayari kupokea na kujadili hoja binafsi za wabunge ili ikiwezekana kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya tatu apandishwe kizimbani.
Tayari mawaziri wawili wa Mkapa, Basil Mramba na Daniel Yona, pamoja na katibu mkuu wa wizara, Gray Mgonja wameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia vibaya ofisi wakati wakiwa mawaziri, lakini bado baadhi ya watu wanataka rais huyo mstaafu apandishwe kizimbani kwa makosa aliyoyafanya akiwa Ikulu.
Mbunge wa Karatu, Dk Wilibrod Slaa ametangaza nia yake ya kuwasilisha hoja binafsi katika kikao kijacho cha Bunge la Muungano, kutaka Mkapa afikishwe mahakamani akidai kuwa suala hilo halihitaji kiongozi huyo wa zamani kuondolewa kinga kama wasomi walivyoshauri, huku kiongozi wa upinzani bungeni, Hamad Rashid akisema ameshaandaa hoja binafsi ya kumuondolea kinga Mkapa.
Na Spika Sitta alikuwa na maneno mazuri kwa wabunge hao wawili na watu wengine wanaoshinikiza kutekelezwa kwa suala hilo.
"Nitatilia maanani hoja yoyote inayomhusu Mkapa itakayofikishwa mezani kwangu na kuiruhusu ijadiliwe ndani ya Bunge," alisema Sitta.
"Bunge bado lina nafasi ya kujadili suala la Rais Mkapa na kulitolea maamuzi kama bunge... na wala mlango haujafungwa kuhusu hoja binafsi itakayotolewa, hivyo kama kuna mbunge yeyote mwenye hoja kuhusu suala hilo anaruhusiwa kuiwasilisha mezani kwangu siwezi kukataa kuipokea."
Lakini Spika Sitta akakumbusha utaratibu wa kuwasilisha hoja bungeni. "Kabla ya hoja hiyo kujadiliwa rasmi bungeni, kuna kamati ya uongozi ambayo hukutana na kuijadili na ikibainika kwamba hoja iliyowasilishwa imejitosheleza na inastahili kujadiliwa, hufikishwa mbele ya wabunge kwa ajili ya mjadala huo," alisema.
Spika Sitta alisema moja ya kanuni za bunge kuhusu hoja yoyote inasema kwamba "hoja lazima ijitosheleze na iwe na uhusiano na suala husika" na kama itajitosheleza kamwe hawezi kufungiwa mlango.
"Kwanza kabla ya mtoa hoja hajawasilisha hoja yake anatakiwa awe na mtandao na wabunge wenzake na wakubaliane ili iwe rahisi kwa hoja yake kuungwa mkono na wenzake bungeni na itakapobainika kwamba, hoja hiyo ina nguvu na imeungwa mkono na wabunge wengi, basi bunge linaweza kubadili katiba na hatimaye Rais huyo Mstaafu akashitakiwa kama raia yeyote ndani ya nchi,"alifafanua Sitta.
Spika Sitta aliongeza kuwa hatua ya pili ambayo mwasilisha hoja anatakiwa kuzingatia ni suala la kanuni za bunge, katiba ya nchi na sheria zilizopo na kwamba hayo yote yakitekelezwa na hoja ikajitosheleza kulishawishi bunge kufanya marekebisho ndani ya katiba yeye kama Spika ama mtu mwingine hawezi kupingana na maamuzi hayo ya bunge.
Alionya kuwa mtoa hoja asipozingatia mambo hayo badala yake akaamua kutoa hoja kwa jitihada zake binafsi huku akijiami kwamba, anaweza kulishawishi bunge kwa kutumia nguvu ya hoja zake, anaweza asifanikiwe hata kama kamati yake ya uongozi itaipitisha hoja hiyo.
Dk Slaa anasema suala la Mkapa kufikishwa mahakamani halihitaji kuondolewa kinga kwa maelezo kuwa tuhuma zinazomkabili za kufanya biashara akiwa Ikulu hazihusiani na nafasi yake kama rais bali mtu binafsi.
Lakini Rashid aliiambia Mwananchi jana kuwa ameshaandaa hoja hiyo na sasa anatafuta kuungwa mkono.
"Kwanza ninampongeza Dk Slaa kwa uamuzi wake wa kujiandaa kuwasilisha hoja hiyo... na mimi natarajia kwamba tutakapokutana na wabunge wenzangu, akiwemo Dk Slaa, tutajadiliana suala hilo ingawa nimeshamaliza kuandika hoja yangu kuhusu marekebisho ya katiba ili Mkapa aweze kushitakiwa pamoja mambo mengine ndani ya nchi kama vile marekebisho ya mikataba feki," alisema Rashid na kuongeza:
"Ili Rais ashtakiwe ama kuondolewa kinga, inabidi katiba ibadilishwe na hivyo ninaamini kwamba, kwa hoja zetu safari hii wabunge watazikubali hasa ikizingatiwa kwamba suala la Mkapa ni kilio cha wananchi cha muda mrefu."
Aliongeza kwamba katiba ina mapungufu mengi na moja ya mapungufu hayo ni kuwapa viongozi nguvu ya kutoshtakiwa na kwamba, katiba hiyo hiyo pia inajipinga yenyewe katika baadhi ya vipengele vyake.
Nziku
12-29-2008, 07:26 PM
Mimi si Mwanasheria ila kwa kuzingatia hoja za Dr. Slaa na Prof. Lipumba zinaleta maana na zinaeleweka zaidi kuliko PCCB na Wanasheria (wasomi wengine) waliolizungumzia suala hili. Hata hivyo sioni kama kunauwezekano wa kumshitaki Mkapa kutokana na kukosekana kwa nia dhabiti ya kupambana na ufisadi pamoja na mafisadi. Hata hii habari ya kupelekwa mahakamani akina Mramba, yona na mgonja unaweza kuona kama ni kujisafisha tu. Unajua katika mapambano lazima awepo kiongozi. sasa katika vita dhidi ya ufisadi inayoendelea sasa inaongozwa na nani? Endapo Mhe. kikwete angekuwa anania dhabiti ya kupambana na ufisadi tungemsikia akisema, akielekeza na kuwaeleza wananchi hali ya mapambano ilivyo (hasa tumjuavyo Rais wetu hupenda kuongea na wananchi hasa yanapotokea mambo yanayoligusa Taifa). Ile miaka ya vita dhidi ya wahujumu uchumi Mwl. na Sokoine walionekana kuwa makini kusimamia mapambano.
mwanakijiji
12-29-2008, 11:04 PM
Mimi si Mwanasheria ila kwa kuzingatia hoja za Dr. Slaa na Prof. Lipumba zinaleta maana na zinaeleweka zaidi kuliko PCCB na Wanasheria (wasomi wengine) waliolizungumzia suala hili. Hata hivyo sioni kama kunauwezekano wa kumshitaki Mkapa kutokana na kukosekana kwa nia dhabiti ya kupambana na ufisadi pamoja na mafisadi. Hata hii habari ya kupelekwa mahakamani akina Mramba, yona na mgonja unaweza kuona kama ni kujisafisha tu. Unajua katika mapambano lazima awepo kiongozi. sasa katika vita dhidi ya ufisadi inayoendelea sasa inaongozwa na nani? Endapo Mhe. kikwete angekuwa anania dhabiti ya kupambana na ufisadi tungemsikia akisema, akielekeza na kuwaeleza wananchi hali ya mapambano ilivyo (hasa tumjuavyo Rais wetu hupenda kuongea na wananchi hasa yanapotokea mambo yanayoligusa Taifa). Ile miaka ya vita dhidi ya wahujumu uchumi Mwl. na Sokoine walionekana kuwa makini kusimamia mapambano.
Nziku.. nafikiri mojawapo ya vitu ambavyo tutakuwa tumegundua miezi hii michache ya mwisho ni kuwa JK anapenda kutobeba lawama ya moja kwa moja. Uongozi wa aina yake ni ule wa 'hand's off" ambapo yeye akiwa Dodoma mnasikia kitu kinatokea Dar au akiwa Zimbabwe mtasikia jambo linafanyika Dar..
Ni kitu ambacho hataki kuonekana anabebeshwa lawama moja kwa moja. Naamini kama Mkapa atafikishwa mahakamani itakuwa ni kwa sababu ya JK lakini itaonekana siyo yeye...
Powered by vBulletin™ Version 4.0.2 Copyright © 2012 vBulletin Solutions, Inc. All rights reserved.