PDA

View Full Version : Chiligati:"Mafisadi wanaodai kuichangia CCM wajitokeze waseme!"



mwanakijiji
12-23-2008, 05:28 PM
Mwandishi Wetu

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi Kapt. John Zefania Chiligati amesema kuwa kama kuna mtu yeyote kati ya wale wanaotuhumiwa kwa ufisadi ambaye anadai kuichangia CCM mtu huyo ajitokeze na aseme. Akizungumza na Mwanakijiji.com Kapt. Chiligati aliendelea kukanusha kuhusika kwa CCM na wizi wa fedha za EPA. ?Tumekuwa tukisema kuwa CCM haihusiki na wizi huo lakini inaonekana wapinzani hawataki kusikia? alisema Bw. Chiligati. Akifafanua msimamo huo Bw. Chiligati amerudia maneno ambayo amekuwa akiyatoa siku chache zilizopita kwa vyombo mbalimbali vya habari kuwa ?kama kuna mwana CCM aliyehusika na wizi huo, basi mtu huyo alifanya hivyo kwa hiari yake, wala hakutumwa na Chama?.

Alipoulizwa kuhusu kile kinachodaiwa kuwa ni michango ya baadhi ya watuhumiwa wa wizi wa benki Kuu kama Jeetu Patel kwa CCM wakati wa uchaguzi Mkuu wa 2005 yawezekana imetokana na wizi huo wa EPA Bw. Chiligati alitoa msimamo kuwa fedha zilizotumika kwenye uchaguzi mkuu kiasi kikubwa kilitokana na michango ya wanachama na mashabiki wake.

?Sasa kama baadhi ya waliochangia vyanzo vyao vilikuwa na utata, sisi hatuwezi kujua; ni sawa na mtu anapochangia kanisani au msikitini sisi hatuna jinsi ya kujua nani kapata wapi fedha zake? alisema Bw. Chiligati. Aliendelea kusema kuwa ?hata suala la magari yaliyotumika wakati wa uchaguzi, ni michango ya wanachama na hilo tumelisema lakini wapinzani wameweka pamba masikioni?.

Alipoulizwa endapo watuhumiwa wa ufisadi ambao wamesimamishwa kizimbani watasema katika utetezi wao kuwa fedha walizozipata toka Benki Kuu walichangia CCM atasemaje? Bw. Chiligati alijibu kwamba ?kama kuna mtu anadai kuwa alichangia fedha za EPA kwenye CCM basi mtu huyo ajitokeze na aseme. Hadi hivi sasa hakuna mtu aliyejitokeza kusema alichangia fedha hizo CCM?

Tovuti yenu ilimtaka pia kueleza kuwa endapo watuhumiwa hao watasimama na kuitaja CCM kupokea fedha za EPA je CCM itakuwa tayari kurudisha fedha hizo kwa umma? Bw. Chiligati hakujibu moja kwa moja bali alisisitiza kuwa ?hao wanaodai hivyo waseme kwanza halafu sisi tutajua cha kufanya wakati huo; michango ikishapelekwa kanisani au msikitini inarudishwa?? alisema Chiligati.

Alipoulizwa kuhusu gharama ya uchaguzi kwa upande wa CCM kwa mwaka 2005/2006 Bw. Chiligati alisema kuwa wakati huo yeye hakuwa katika nafasi ya kujua na hivyo asingefanya haki kulizungumzia hilo isipokuwa Mweka Hazina wa Chama hicho Bw. Amos Makalla. ?Yeye anaweza kuwa na ?general idea? lakini naye kama mimi hatukuwa kwenye uongozi wakati huo, hata hivyo anaweza kukuambia makadirio tu? alielekeza Bw. Chiligati.

Naye Msajili wa Vyama vya siasa nchini Bw. John Tendwa amesema kuwa hawezi kujua gharama halisi ya uchaguzi mkuu kwani mwenye kuweza kujua hilo ni Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Bw. Kiraivu. Bw. Tendwa aliyasema hayo alipozungumza na tovuti hii ambayo ilitaka kujua juu ya mchanganuo wa mapato na matumizi ya vyama yaliyowasilishwa kwake kwa mwaka 2005/2006.

Bw. Tendwa alitolea mfano wa ukaguzi wa vitabu vya CCM na Chadema na kutumia neno moja tu kuwa uko ?perfect?. ?Hata hivyo sisi tunapewa kwanza ukaguzi wa fedha zile za ruzuku ambazo zinatoka serikalini, na vile vyanzo vingine vya fedha za vyama vya kisiasa tunaletewa taarifa tofauti (separate) ya ukaguzi? alisema Bw. Tendwa na kumwelekeza mwandishi kwa tume ya Uchaguzi kama angetaka kujua zaidi juu ya gharama za uchaguzi mkuu.

Juhudi za kumpata Mweka Hazina wa CCM Bw. Amos Makalla hazikuzaa matunda licha ya simu yake kuita kwa muda mrefu. Tovuti yenu itaendelea kumtafuta ili kuweza kupata habari kutoka kwa wenye habari wenyewe.