PDA

View Full Version : "Mbowe safisha nyumba yako kwanza" - CCM



mwanakijiji
12-25-2008, 10:19 PM
Mwandishi Wetu
Daily News; Wednesday,December 24, 2008 @21:15


Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kujibu tuhuma za ubadhirifu wa fedha unaomkabili ndani ya chama chake na kumwacha Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kwa kuwa ni msafi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda, Richard Tambwe alisema CCM imesikitishwa na maneno yaliyotolewa na Mbowe dhidi ya Rais huyo mstaafu kuwa asiende kwenye kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Mbeya Vijijini, vinginevyo watamchafua.

Tambwe alisema baadhi ya magazeti ya jana yalimnukuu Mbowe akisema kuwa Chadema kitamchafua Mwinyi na kumvunjia heshima ikiwa ni pamoja na kubadilisha msimamo wa chama hicho kwa kile walichokiita kumsamehe Rais Mwinyi kwa makosa aliyofanya huko nyuma.

?Tumesikitishwa na kauli hii ambayo inathibitisha upungufu mkubwa wa Mbowe na chama chake ambacho siku zote kimekuwa mstari wa mbele kuchafua majina ya watu bila ya kuwa na ushahidi au ukweli wowote,? alisema Tambwe.

?Mbowe ambaye ni kijana mdogo sana asiyekaribia hata kidogo kwa umri wa baadhi ya watoto wa Rais Mwinyi, alipaswa kuonyesha heshima na adabu kwake kwa kuzingatia kwamba ni kama baba yake,? aliongeza Tambwe.

Alisema badala ya kujiandaa kutaka kumchafua Mzee Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa, jambo ambalo halitafanikiwa kutokana na rekodi yake safi iliyotukuka ya kulitumikia taifa, ni vyema Mbowe na chama chake wakatoa majibu ya tuhuma zinazowakabili kwanza.

Alizitaja tuhuma hizo ni pamoja na Mbowe kufanya udanganyifu wa matumizi ya fedha zilizotolewa na Taasisi ya Westminister Foundation ya Uingereza kupitia chama cha Conservative kwa ajili ya ununuzi wa pikipiki kwa wilaya zote nchini ikiwa ni msaada kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu uliopita ambazo hazikununuliwa.

?Pikipiki ambazo baadhi ya wanachama wakiongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, marehemu Chacha Wangwe wakati huo na wameendelea kulalamikia kwamba fedha za pikipiki hizo zilitumiwa na watu wachache kwa manufaa yao binafsi,? alisema Tambwe.

Tambwe alizitaja tuhuma nyingine kuwa ni madai ya ukabila uliokithiri ndani ya chama hicho uliopelekea wabunge watano kati ya wote wa viti maalumu kutoka Mkoa wa Kilimanjaro na mmoja aliyetoka Kigoma ni ndugu wa karibu na kiongozi mmoja mwandamizi huku viongozi wengine makao makuu wakiwa wanatoka kwenye familia au ukoo mmoja.

Tuhuma ya tatu Tambwe alisema Mbowe pia anadaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za chama kwa kukidai dola 181,949 sawa na Sh 218,338,546 ambazo hadi Agosti mwaka huu alikwishalipwa Sh milioni 175, akidai kuwa alitumia fedha zake wakati wa uchaguzi na chama kimrudishie wakati hakuna ushahidi wowote jinsi fedha zilivyotumika.

?Ni aibu tena ni kashfa kubwa kwa chama, kwa viongozi wa ngazi yake anayepiga kelele za ufisadi kutofuata taratibu za kitaasisi katika kununua huduma jambo ambalo ni ufisadi mtupu,? alisema Tambwe. Kiongozi huyo aliongeza kuwa Mwinyi atakwenda Mbeya kama alivyopangiwa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kuzindua kampeni hizo za CCM Januari 4, mwakani na chama chake kina uhakika wa kushinda. Aidha, alisema Chadema siyo washindani wa CCM kwa kuwa Uchaguzi Mkuu wa 2005, chama hicho cha Demokrasia na Maendeleo kilishika nafasi ya nne.

My Take:
Je, wapinzani kabla ya kukikonyoshea vidole CCM ni lazima kwanza kabisa wajiangalie wao wenyewe? Kwamba kama kwako kuna matatizo basi usioneshe matatizo ya jirani yako?

Mpita Njia
12-27-2008, 03:36 PM
My Take:
Je, wapinzani kabla ya kukikonyoshea vidole CCM ni lazima kwanza kabisa wajiangalie wao wenyewe? Kwamba kama kwako kuna matatizo basi usioneshe matatizo ya jirani yako?

Pia siamini kuwa mtu wa calibre ya Tambwe ana audacity ya kuwataka wapinzani wajitazame

mwanakijiji
12-27-2008, 06:40 PM
Dk. Slaa achachamaa
? Ashtushwa Tambwe kumshambulia Mbowe

na Kulwa Karedia (Tanzania Daima)




KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema ataanika uozo wa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tambwe Hizza.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana kutokana na kauli iliyotolewa na Hizza juzi dhidi ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, akimhusisha na matumizi mabaya ya fedha ndani ya chama hicho.

?Ndugu mwandishi nakwambia muda wa kumuanika Hizza umefika kutokana na madhambi yake aliyoyafanya akiwa na Chama Cha Wananchi (CUF) kabla ya kuhamia CCM?ametoa wapi jeuri hii?? aliuliza Dk. Slaa.

Alisema kauli ya Hizza juu ya Mbowe haina ukweli wowote kutokana na CHADEMA kukamilisha ukaguzi wa fedha zake kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

?Namwambia Hizza aache uongo wa mchana?kama amechoka ni heri akajitoa CCM na kukaa pembeni badala ya kuudangaya umma wa Watanzania?huyu hana jipya lolote, amesahau kilichomkimbiza CUF!? Alisema Dk. Slaa.

Alisema akiwa CUF, Hizza alituhumiwa kuchota mamilioni ya fedha ambayo hadi leo ameshindwa kuyatolea maelezo wala kukanusha, kitendo ambacho kinaonyesha wazi alihusika na upotevu huo.

?Kama anataka kupambana katika hili, mimi niko tayari kutoa nyaraka zote za hesabu Za CHADEMA na yeye aje na nyaraka zake anazotuhumiwa kuiba fedha CUF tuone nani mkweli kati yangu na yeye?hizi ndiyo hoja alizopeleka Tarime wakati wa uchaguzi, lakini tulifanikiwa kuzijibu,? alisema Dk.Slaa.

Alisema matamshi hayo ya Hizza ni sawa na kutangaza vita ya kisasa na kwamba anamsubiri katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Mbeya Vijijini ili aanze kumshughulikia kikamilifu.

?Muda wa kumshughulikia Tambwe umefika, namngonja kwa hamu kubwa sana Mbeya Vijijini kwenye kampeni zinazotarajiwa kuanza Januari 4; namuomba asikimbie maana amechokoza moto ambao atashindwa kuuzima,? alisema Dk. Slaa.

Alisema Hizza hana hadhi ya kumhoji Mbowe kwa vile wadhifa wake alio nao haulingani na mwenyekiti huyo, hivyo anapaswa kuwa kiongozi mwenye adabu kabla ya kukurupuka.

?Napenda kuuambia umma kwamba huyu Hizza hana hadhi ya kujibizana na mwenyekiti wangu (Mbowe), anapaswa kuwa na adabu kabla ya kukurupuka; Tambwe ni kama sisimizi anayetaka kuangusha mbuyu,? alihoji Dk. Slaa.

Alisema Hizza amekuwa msemaji wa CCM, jambo ambalo linaashiria wazi kwamba anataka kulinda uchafu na ufisadi uliokithiri ndani ya chama hicho.

?Nikiamua kumshughulikia anaweza akapata presha kama alivyowahi kupata wakati aliposhindwa kwenye uchaguzi wa ubunge pale Temeke - akaanguka baada ya kupata presha; sioni sababu ya kumuumiza, lakini pia aache kuilinda CCM na kuwa chaka la ufisadi,? alisema Dk. Slaa.

Hizza ni mmoja wa viongozi wa CCM waliofaidika na fedha za wizi kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Limited kwa vile kitengo chake kilipewa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwadanganya Watanzania.

?Huyu ni mmoja wa watu walionufaika na fedha za Kagoda; sasa atatwambia nini. Alizitumia mno fedha hizo kuwadanganyia Watanzania nadhani naye siku yake ya kushughulikiwa imekaribia,? aliongeza Dk. Slaa.

Kuhusu madai ya CHADEMA kutoshiriki katika vikao vya pamoja vya vyama vya upinzani vya Afrika - Democratic Union of Afrika (DUA) - Dk. Slaa alisema madai hayo hayana ukweli kwa vile viongozi wa juu wa CHADEMA wakiongozwa na Mbowe walihudhuria mkutano huo Accra, Ghana.

?Sijui kwa nini tunakuwa na viongozi wa aina hii jamani, nashangaa kuona anazungumzia suala la DUA ambalo mwenyekiti wetu na maafisa walihudhuria mkutano ule kule Accra, Ghana? sasa haya mambo ya uzushi yanatoka wapi??Aliuliza Dk. Slaa.

Akizungumzia tuhuma za kumshambulia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Dk. Slaa alisema anathamini mchango wake katika taifa na kwamba CHADEMA haina nia ya kumchafua kiongozi huyo.

?Mwinyi ni mzee tunayemheshimu mno, hana madhambi kama yaliyofanywa na Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Benjamin Mkapa?hivyo tunatambua mchango wake, sasa Hizza ndiye amegeuka kuwa msemaji wake?nayasema haya kwa sababu nimetumwa na watu wa Mbeya kuyasema,? alisema Dk. Slaa.

Jumanne wiki hii Hizza aliitisha mkutano na waandishi wa habari, ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam, ambako alisema CCM imesikitishwa na hatua za CHADEMA kuingilia kampeni za chama hicho tawala, zinazotarajiwa kuanza Januari 4 mwakani.

Mbali ya kauli hiyo, Hizza alikishutumu chama hicho kwa kushindwa kutoa hesabu zake za sambamba na kumtuhumu Mbowe, akidai amefanya ubadhilifu kwa kukidai kiasi cha sh 218,338,546 na kwamba hadi Agosti 2008 alikuwa amekwishalipwa sh milioni 175, huku kukiwa hakuna ushahidi wowote wa jinsi fedha hizo zilivyotumika.