PDA

View Full Version : News Alert: Mgombea wa Chadema aenguliwa Mbeya Vijijini!



mwanakijiji
12-30-2008, 10:05 AM
(Tanzania Daima)

MSIMAMIZI wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Vijijini, amemfuta katika orodha yake mgombea wa ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Sambwee Shitambala.

Uamuzi wa kumfuta Shitambala umekuja kutokana na pingamizi ambalo mgombea huyo aliwekewa na wagombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mchungaji Luckson Ndaga Mwanjela na yule wa Chama cha Wananchi (CUF), Daud Mponzi. Mgombea mwingine ambaye naye ameondolewa katika kinyang?anyiro hicho ni Ndele Mboma, aliyekuwa amejitokeza kugombea kwa tiketi ya Democratic Party (DP).

Wagombea hao wawili waliwekewa pingamizi na wenzao kutokana na fomu zao za kugombea kubainika kuwa na kasoro za kisheria.

Taarifa kuhusu uamuzi wa msimamizi huyo wa uchaguzi, Juliana Malange, kumuondoa mgombea wa CHADEMA, zilithibitishwa na viongozi wa juu wa chama hicho walioko Mbeya kufuatilia mwenendo wa maandalizi ya kampeni za uchaguzi mdogo zinazotarajiwa kuanza leo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, msimamizi huyo ambaye tayari amekabidhi barua za uamuzi wake kwa vyama husika, anatarajiwa kutoa tangazo rasmi la uamuzi wake huo leo.

Habari zaidi kutoka katika ofisi ya msimamizi huyo zinaeleza kwamba, Shitambala ameng?olewa baada ya fomu zake za kugombea kusainiwa na kampuni moja ya uwakili ya Mbeya, badala ya hakimu, kama sheria za uchaguzi zinavyoelekeza.

Kabla ya uamuzi huo, mgombea huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria, aliwasilisha utetezi wake kwa msimamizi huyo kwa kupinga hoja za wapinzani wake waliodai kuwa, mawakili hawana haki kisheria ya kuapisha kama ilivyo kwa mahakimu.

Shitambala katika utetezi wake, alinukuu baadhi ya vifungu vya sheria kuwa, hakimu anapata uwezo wa kuapisha kisheria kutokana na sheria ya Oaths (Judicial Proceedings) and Statutory Declarations Act 1966), kifungu cha 11 ikisomwa pamoja na sheria ya Notaries Public and Commissioner for Oaths kifungu cha 10, kinachotaja nani anaruhusiwa kuapisha.

Kwa maana hiyo alisema, wakili au hakimu wakati anaapisha, anakuwa na wadhifa wa Notary Public and Commissioner for Oaths na kutajwa hakimu pekee kwenye sheria ya uchaguzi hakuzuii wala kuharamisha wakili kuapisha.

Pia mgombea huyo katika maelezo yake alitupilia mbali madai yote yaliyowasilishwa na wagombea hao wawili wa CCM na CUF, yaliyodai kuwa anatembea na mihuri mfukoni na aliapishwa na kampuni ya uwakili ambayo anafanyia kazi.

Alisema aliapishwa na wakili kutoka Kampuni ya Ernest Mashiba Advocate ambayo hana uhusiano nayo, wala hajaajiriwa hapo.

Kwa maana hiyo, mchuano katika uchaguzi huo, utashirikisha vyama vitatu vya CCM, CUF na SAU.

Hata hivyo habari zilizopatikana baadaye jana kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CHADEMA zilisema kuwa, chama hicho kilikuwa kikikusudia kukata rufaa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupinga uamuzi huo.

Hatua hiyo ilithibitishwa na mgombea mwenyewe Shitambala, ambaye aliiambia Tanzania Daima kuwa msimamizi ameshindwa kutafsiri sheria, hivyo anakusudia kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Wakati CHADEMA ikisubiri uamuzi huo wa NEC, CCM na CUF kwa nyakati tofauti vimepokea kwa furaha uamuzi huo, huku kila chama kikijigamba kuwa njia ya ushindi katika uchaguzi huo ni nyeupe.

Mgombea wa CUF, Mbozi, hakuficha hisia zake kwa kusema kuwa aliamua kuweka pingamizi hilo dhidi ya CHADEMA baada ya chama hicho kilichoibuka na ushindi kwenye uchaguzi mdogo wa Tarime, kukataa kuiachia CUF kwenye uchaguzi huo wa Mbeya Vijijini.

Makada wa CCM waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti waliielezea hatua hiyo ya kung?olewa kwa mgombea wa CHADEMA kuwa yenye manufaa makubwa kwa chama na mgombea wao.

?Mimi nasema ukweli, baada ya CHADEMA kung?olewa, ushindi wa CCM katika jimbo hilo si suala la kujadili tena, ingawa hatufurahi kutokuwa na upinzani tulioutarajia kutoka CHADEMA,? alisema kada mmoja wa CCM ambaye atakwenda kumnadi mgombea wa chama chao.

Hata hivyo, wakati CCM na CUF wakishangilia kuenguliwa kwa mgombea wa CHADEMA, wanachama na wafuasi wa chama hicho, wanatarajia kufanya maandamano katika ofisi za msimamizi wa uchaguzi mjini hapa kupinga uamuzi huo.

Uchaguzi katika jimbo hilo, unafanyika kuziba nafasi ya aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, marehemu Richard Nyaulawa, aliyefariki dunia Novemba 9 jijini Dar es Salaam.