PDA

View Full Version : CCM yamwambia Liundi: "Taja mamluki wetu!"



mwanakijiji
01-01-2009, 08:21 PM
CCM: Liundi taja mamluki tuliowapandikiza upinzani

2009-01-01 13:44:58
Na Simon Mhina

Chama cha Mapinduzi CCM kimejibu shutuma dhidi yake zilizotolewa hivi karibuni na msajili wa kwanza wa vyama vya siasa, George Liundi kwamba kimepandikiza mamluki katika vyama vya upinzani, na kumtaka awataje kwa majina mamluki hao kama anataka aaminike.

Akizungumza na Nipashe, Katibu Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Kapteni John Chiligati, alisema amestushwa na madai hayo, ambayo kwa kiasi kikubwa yanashangaza.

``Liundi amesema kwamba akisutwa atataja majina ya mamluki waliopandikizwa upinzani na CCM, hilo limetufurahisha. Na sisi bila kuchelewa tumeanza kumsuta.

Tunamtaka atutajie hayo majina ya wapinzani feki tuliowapandikiza kwenye vyama vya siasa nchini,`` alisema Chiligati.

Alisema CCM ni chama imara ambacho hakitegemei kupata nguvu wala msaada wowote kwa mamluki, kwa vile tangu kianzishwe Watanzania wameonekana kukiunga mkono pasipo na shaka yoyote.

Alipoulizwa kwamba CCM itakuwa tayari kuwajibika iwapo Liundi atataja majina hayo, Katibu huyo alisema hawezi kuyataja kwa vile sio jambo la kweli.

Alihoji ni kwa vipi awafumbie macho`mamluki` kwenye vyama vya upinzani wakati wote, wakati yeye alidai kwamba alifanya kazi yake kwa mujibu wa sheria, bila kuyumbishwa na mtu?

Chiligati ambaye pia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema hali inayoonyesha ni kwamba hivi sasa Liundi anayo matatizo makubwa ndiyo yamemsukuma kutoa madai hayo ya uongo.

Alipoulizwa kwamba anafahamu matatizo yanayomkabili Liundi, alisema: ``Anayo matatizo ya kiubinadamu.``

Alisema iwapo Liundi hatotaja majina ya wanasiasa mamluki ndani ya upinzani, watachukulia madai hayo ya Liundi kwamba ni matokeo ya matatizo hayo aliyonayo.

``Yeye amesema akisutwa atawataja, sasa kaandike kwamba tumemsuta kweli kweli, ili awataje,`` alisema Chiligati, ambaye katika siku za karibuni amekuwa akijibu kila kauli inayotolewa kukikosoa chama tawala.

Huko nyuma aliyekuwa mwepesi kujibu alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuph Makamba.

Hivi karibuni, Liundi alikaririwa na gazeti hili katika mahojiano maalum akisema kuwa anawajua mamluki wote waliopandikizwa na CCM kwenye vyama vya upinzani kwa lengo la kuvihujumu.

Liundi alienda mbali zaidi akasema kutokana na CCM kuhofu upinzani, kuna wakati viongozi walichanganyikiwa wakala njama za kuvunja mfumo wa vyama vingi nchini.

Alisema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ndiye aliyezima jaribio hilo baada ya yeye (Liundi) kwenda nyumbani kwake kumlalamikia kuhusu mpango huo.

Mpita Njia
01-21-2009, 03:22 PM
Wanajua ameshapiguika hawezi kufanya kitu, wacha waendelee kumdhihaki mzee wa watu

mwanakijiji
01-21-2009, 05:14 PM
sasa Liundi mwenyewe ameshindwa kuwataja hao mamluki?

Dalali
01-24-2009, 04:48 PM
[I]Kumekuwa na shida nyingi katika vyama vya siasa kupelekea vyama hivi kudumaa kama siyo kupaa halafu kurudi chini kusikookoteka!!
Viongozi wakubwa katika vyama hivi wamekuwa wakijiengua kurudi ccm kwa mbwembwe na madaraka wakisema wasiyo weza kuyaamini kama ni matapishi!
Liundi ni binaadamu na anaweza kukosa uvumilivu kama Warioba alivyofikia hivi karibuni,na kwa vile anajua ni yapi akiwatonesha watapiga kelele na sasa tayari!!
Mzee Liundi tunahitaji ushindani wa dhati katika vyama vya siasa ili tuingie katika mabadiliko ya kweli.Tunaelewa wewe ni hazina katika mambo mengi tupe majina hayo ili vyama viweze kujipanga.
Ulivyotamka kuwa wapo bila kuwataja ni kitendo kinachokusuma kuonekana "mnafiki" na hivi kuunganishwa katika mengi yaliyovipata vyama hivi.
Ninaamini kuwa utatupa mengi zaidi ya majina ila wakati haujafika uliopanga na ambao ni mwafaka kwa kuaminisha wananchi ukweli utakaouma zaidi.
dalali

imbya
01-28-2009, 01:11 PM
Napenda kuipongeza timu nzima ya mwanakijiji kwamambo mengi ambayo yameisaidia jamii kufahamu kwa undani maovu mengi ambayo yanatokea kwenye jamii yetu siku hadi siku. Haswa haya maufisadi yanayofanywa na watu tuliowaamini.

Nsaji Mpoki
02-04-2009, 10:09 AM
Nafikiri si sahihi kumtaka Liundi ataje hao mamluki,ni wajibu wa watanzania wote kutumia ufahamu wao kubaini viongozi wenye muelekeo wa kuhujumu upinzani.Dawa sahihi ni kuwabaini mienendo yao na kutimiza viongozi sahihi wenye muelekeo wa dhati wa kuleta mageuzi.Liwe ni jukumu la kila mtu kutumia fikra zake na kutoa maamuzi sio kila tusubiri kuelekezwa.