PDA

View Full Version : Pinda amepoteza sifa ya kuwa kiongozi!



mwanakijiji
01-29-2009, 04:57 PM
Na. M. M. Mwanakijiji

Mwanzoni sikutaka kuamini kuwa Waziri Mkuu amesema alichodaiwa kusema. Sikutaka kukubali kuwa Mwanasheria na Mwanausalama wa taifa kama yeye anaweza kusema hicho alichosema. Sikutaka kudhania kuwa Waziri wetu Mkuu kwa sababu ya janga la mauaji ya Albino yuko tayari kutangaza uvunjwa wa makusudi wa sheria, uvunjaji ambao hauna uwezo wa kugeuzwa. Unapotoa kibali cha mtu kuua ?papo hapo? bila kufuata mkondo wa sheria umetoa kibali cha utawala wa sheria ya mwituni.

Kwa vile ameyarudia maneno hayo tena kwenye gazeti la ?The Citizen? la jana bila utata wowote na kuonesha kuwa anayamaanisha, basi kama tulivyompinga aliyemtangulia, natumia nafasi hii kuyakataa mara moja, daima na milele maamuzi yake hayo kuwa ni ya hatari, yanatishia maisha ya watu, ya kichochezi na kwa hakika kabisa hayawezi kamwe kukomesha mauaji ya dada na kaka zetu maalbino.

Anapolia Bungeni kuonesha uchungu wake, kunathibitisha jambo moja tu, uchungu alionao umemtia kiza katika utashi wake kama kiongozi na hivyo kumfanya kuwa ni mtu wa hatari sana katika madaraka. Mtu mwenye uchungu usimpe nafasi ya kulipiza kisasi. Hivyo hadi pale atakapoyakana maneno, kuyafuta na kutetea utawala wa sheria na Katiba ni jukumu la kila Mtanzania kumpinga na ni uzalendo kufanya hivyo.

Kwanini?

Kwanza kabisa, ni kwa sababu huwezi kuzuia mauaji, kwa kuhalalisha mauaji mengine. Waziri Mkuu wa Nchi anaposimama na kuwaambia watu bila majuto tena kwa fahari kuwa watu wauane kwa sababu serikali yake imeshindwa kusimamia utawala wa sheria anapoteza sifa ya kuendelea kuwa Waziri Mkuu. Waziri Mkuu anapotangaza hadharani kuwa ni vyema tena ni haki kuvunja sheria zetu ati kwa sababu ya adha ya maalbino anachofanya ni kumwagia mafuta kwenye moto ambao tayari unawaka na kuunguza.

La pili na kubwa zaidi ni kuwa karibu mwaka mmoja uliopita Wakati anaapishwa pale Dodoma (na ninayo video ya kuapishwa kwake) nimeangalia jinsi alivyoapa. Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda aliapa huku ameshika Biblia kuwa atailinda na kuhifadhi hisia zake! Aliapa kuwa kwa nafasi anayoingia atalinda na kutetea vionjo vyake na machungu yake! Aliapa kuwa endapo mgongano utatokea kati ya sheria na huzuni, sheria na hasira, sheria na kisasi yeye atachagua huzuni, hasira na kisasi!

Hapana hakufanya hivyo. Hata hivyo inaonekana ameshasahau kiapo chake. Waziri Mkuu wetu aliapa kuilinda, kuitetea na kuitunza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hicho ndicho kiapo chake. Hakuapa kulinda hisia za Watanzania, hakuapa kulinda na kutetea huzuni za Watanzania. Aliapa kulinda Katiba yetu.

Kwa vile amesahau hata Katiba inasema nini naomba nimkumbushe. Ibara ya 13 inazungumzia juu ya usawa mbele ya sheria. Kifungu cha 1 kinasema hivi ?Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.? Kwa vile Waziri wetu amesahau kifungu hicho naomba niweke msisitizo kwenye neno ?WOTE?. Katiba inaposema kuwa watu wote ni sawa maana yake ni kuwa inapokuja sheria Albino ni sawa na mtu yeyote mwingine asiye na ulemavu. Kichaa ana haki sawa na timamu, mwanamke ana haki sawa na mwanamme na fisadi ana haki sawa na asiye fisadi.

Wote hawa ?wanayo haki bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria?. Waziri Mkuu kwa maelezo yake aliyoyatoa ametangaza wazi kuwa Katiba yetu haina maana na yeye kwa kushindwa kuitetea hata wakati huu hana budi kujiuzulu.

Kifungu kinachofuatia pia ni kikubwa zaidi nacho kinasema ?Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.? Katika kifungu hicho msisitizo uko kwenye neno ?KILA MTU NA JUMUIYA YA WATU?. Ina maana ya kwamba hata yule ambaye amekutwa na mkono wa Albino, damu inatiririka, anakimbizwa na kukamatwa pale anapokamatwa ibara hiyo inasimama!

Siyo kwamba hatusikii uchungu, siyo kwamba hatuoni unyama huo, siyo kwamba hatutambui ubaya wa tendo ambalo tunamshuku au tumeona akilifanya tendo hilo. Tunapomkamata na kumpeleka Polisi, na ushahidi tuliomkuta nao, tunatoa nafasi kwa sheria kufuata mkondo. Maana yake, atapelekwa mbele ya mahakama, atahojiwa, wataitwa mashahidi, ushahidi utapimwa, atapewa nafasi ya kuwahoji mashahidi na mwisho sheria itasema kama ana hatia au la. Sheria ikisema ana hatia na ikatoa hukumu ya kunyongwa na akaenda kunyongwa basi hakuna atakaye lalamika.

Hii ina maana hata kama watakamatwa watu 1000 ambao wamefuata mkondo wa sheria na wote wakanyongwa au kupigwa risasi au kunyweshwa sumu au vyovyote vile tutakuwa tumefuata sheria zetu.

Kifungu cha sita cha ibara hiyo hiyo kinaeleza zaidi juu ya usawa huu mbele ya sheria. Sehemu yake inasema hivi: ?wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa nahaki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya
kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kingenecho kinachohusika? Huu ndiyo utawala wa sheria. Ukinituhumu mimi hata kama umeniona nimeshika kiberiti na kutaka kuchoma nyumba, unipe nafasi ya kusikilizwa utetezi wangu hata kama ni wa kijinga kiasi gani!

Tukikubali kufuata mapendekezo ya Waziri Mkuu, tunavunja kabisa dhana nzima ya mahakama na utawala wa sheria! Kama yeye ameshindwa kulinda ibara hiyo kama alivyoapa ajiuzulu!

Hatari ya kukubali hoja ya Waziri Mkuu.
Kinachonisumbua hasa na kama nikifuata mantiki ya Waziri Mkuu ni kuwa gharama ya kutekeleza uvunjaji huo wa sheria unaopendekezwa na Waziri Mkuu ni kubwa mno ukilinganisha na gharama ya kufuata sheria zilizopo. Hivi ukimkuta mtu ana mkono wa mtu, ametapakaa damu, anakimbia, na mkono ule unaonekana ni wa Albino, ukaanza kumkimbiza ukamkamata, unajuaje kuwa kwamba yeye ni muuaji?

Mwanasheria makini hatokurupuka kujibu swali hilo. Waziri Mkuu hata hivyo anasema usimpe nafasi kujieleza, ?umekuta ana mkono, damu, anakimbia basi muueni papo hapo? anapendekeza. Kweli? Vipi kama muuaji ni mwingine ambaye alipoona atashtukiwa akakutana na mtu akamtishia kwa mtutu wa bunduni kumbebea kiungo hicho na alipoona watu wanakuja alimuacha huyo bwana? Yule mtu alipoona kuwa watu wanakuja ana uamuzi gani? Akae atoe maelezo kuwa alitekwa n.k au akimbie? Kwa maelezo ya Waziri Mkuu mtu huyo hana nafasi hiyo kwani akikutwa na ?ushahidi? wote basi auawe papo hapo!

Hili nalikataa, maisha siyo rahisi namna hiyo.

Naamini kabisa kuwa Waziri Mkuu amesema haya yote kwa nia njema akisukumwa kweli na uchungu wa adha (plight) ya ndugu zetu maalbino ambao wamegeuzwa mawindo katika taifa lao. Yote hayo hata hivyo hayaondoi ukweli kuwa tukikubali kuwa watu waanze kuchukua hatua hizi mikononi tutakuwa tumehalalisha uvunjaji mkubwa wa sheria nchini.

Tukikubali kuwa watu wajichukulie sheria mikononi kwa sababu wamechoshwa na kero ya uhalifu fulani tutakuwa na tofauti gani na wale wanaokamata vibaka Kariakoo na kuwatia viberiti kwa sababu na wenye wamechoshwa na kero na adha ya kusumbuliwa na vibaka? Tutakuwa na tofauti gani na wale ambao wanamkamata mwizi wa kuku na kumpiga hadi kumuua wakati kituo cha Polisi kipo karibu? Kama ni halali kuwapiga watuhumiwa wa mauaji na kuwaua kwa vile tumewakuta na ushahidi kuna ubaya gani mtu akimkuta mgoni wake amtie risasi, akikasirishwa na mtu kwenye basi amtie kisu, n.k?

Je mawazo haya si yanatukumbusha kiongozi fulani ambaye baada ya kuchomekewa akajikuta kuwa hakuna haja ya mahakama, hakuna haja ya polisi, alisahau Katiba aliyoapa kuilinda akachomoa bunduki yake na kumtwanga mtu risasi? Kwanini tulimpeleka mahakamani yule? Kwanini tulimpa nafasi ya kujitetea mbele ya mahakama? Ina maana hakukuwa na watu wenye uchungu wa kifo cha kinyama cha kijana yule? Ina maana hakukuwa na watu ambao na wenyewe wangependa kumpa fundisho mheshimiwa yule ?papo hapo?. Tulifuata mahakama kwa sababu hatukuwa tayari kuacha watu wajichukulie sheria mkononi. Kwanini tuanze leo?

Ndiyo Waziri Mkuu anataka tuamini kuwa hatujui machungu ya ndugu zetu kuuawa kinyama. Kweli? Kwamba yeye mwenzetu ndiye pekee anayebeba machungu ya taifa na yeye pekee ndiye anayeumwa na mauaji haya? Hapana, Waziri Mkuu wengi wetu tunafahamu kwa karibu machungu haya kwani yametishia ndugu na rafiki zetu, tunafahamu ubaya huu na tumejaribu kufanya kila tunaloweza kushiriki katika kukomesha mauaji haya. Katika hayo yote hatujafikiria kuvunja sheria zetu. Kwa sababu kama tukitaka kukomesha kwa staili ya Baghdad, Waisraeli na Hamas, au mtindo wa Congo, Somalia na LRA wapo watu wanaweza. Sungusungu ambao yeye amesema kuwa ?anawahusudu? wanakumbukwa kwa vitendo vyao vya miaka ya themanini. Hapana, Waziri Mkuu ametetea uvunjaji wa Katiba tena kwa kiburi, akiamini kuwa yeye yuko nje ya sheria nay a kuwa kwa vile anazungukwa na ving?ora na saluti basi anaweza kuamua kutangaza kuwa nchi yetu haina sheria tena na kila mtu na lwake. Hili tunamkatalia. Kama hawezi au hayuko tayari kufuata sheria na Katiba aliyoapa kuilinda kwa sababu ana uchungu mno, au kwa sababu ya uchungu huo ametiwa kiza cha kuona uzito wa kauli yake. Basi ajiuzulu ampishe mtu mwingine kusimamia na kulinda sheria zetu.

Tunapotaka watu waheshimu utawala wa sheria hatuna maana wawe na hiari ya kuheshimu utawala wa sheria. Katika nchi ya kidemokrasia (au inayojaribu kujenga demokrasia kama ya kwetu) sheria ndiye dikteta! Pinda kama vile alivyo James na kama vile alivyo Zeituni wote wanabanwa na sheria. Haiwezekani yeye mwenzetu kutoa maagizo ambayo anafikiri ana uwezo wa kuyatoa kwa sababu yuko ?nje? ya sheria. Hili ni la kupinga.

Mtu mwingine anaweza kuchukulia kuwa mwanakijiji aone mauaji haya ndivyo atajua kwanini hatuwezi kuchezea suala hili. Ukweli ni kuwa mimi ni miongoni mwa watu ambao kwa mwaka mzima tumetoa mapendekezo kadha wa kadha ambayo hayajatekelezwa, mapendekezo ambayo naamini yanaweza kabisa kupunguza na kutokomeza mauaji haya. Nimeandika tena kwenye gazeti la Tanzania Daima la jana na kutoa mapendekezo ya jinsi gani kama taifa tunaweza kupambana na aibu hii kwa mtazamo wangu. Nina uhakika kuna watu wengine wana mawazo yaliyo bora zaidi pia.

La mwisho ambalo pia ni la kupinga ni kauli ya Waziri Mkuu kutaka UVCCM kushiriki kama ?jeshi? kupambana na mauaji ya Albino. Kwa vile hadi sasa Waziri Mkuu hajafuta kauli hizo naamini kabisa kuwa ni za kweli. UVCCM siyo jeshi na wao kushiriki kufanya kazi ya jeshi au kwa namna yeyote ile kujichukulia sheria mikononi ni makosa ambayo natumaini DPP hatochochelewa kuyafuatilia.

Hata kuwaagiza Sungusungu ambao kwa watu wa kanda ya ziwa wanajua sifa yao ni kuchezea maisha ya wote. Hawa Sungusungu hawana mafunzo yoyote ya kipolisi au ya masuala ya haki za binadamu. Endapo Sungusungu hawa wakitekeleza maagizo ya Waziri Mkuu wakafanya mauaji makubwa huko tunajua wazi ni nani wa kumlaumu. Haitoshi kutuambia kuwa Waziri Mkuu ?alimaanisha? nini, wakati wale waliomsikia wanajua ni nini hasa alimaanisha.

Kama tumeshindwa na Polisi, tumeshindwa na JWTZ, tumeshindwa na TISS na vyombo vingine vya usalama, kama kweli tumeshindwa kutokomeza mauaji haya kwa kutumia mbinu za kisasa na sasa tumekimbilia ulinzi wa jadi (wakati waganga wa jadi tumewafutia leseni) hatuna budi kujiuliza kama tunaongozwa na akili zetu au hisia zetu. Kama Waganga wa Jadi tumewafutia leseni, hawa Sungusungu tunaowapa jukumu la kuingilia hata uhai wa watu wana leseni gani ya ulinzi? Ni maafisa wa jeshi gani hawa? Je wakifanya makosa watashtakiwa kwa ?police code? gani?

Ninachosema ni kuwa kauli hizi za Waziri Mkuu siyo za kupuuzwa au kuzichukulia kwa urahisi ni kauli za kulaani na za kuweza (kwenye nchi zinazoheshimu kweli utawala wa sheria) kumlazimisha hata Waziri Mkuu kujiuzulu. Waziri Mkuu aombe radhi kwa kauli hizi na kama anazisimamia basi aachie ngazi ili mtu mwenye kutaka kulinda kweli sheria zetu ashike nafasi yake.

Kwa mtindo huu wa kujaribu kuongozwa na jaribu na matatizo ya wakati fulani na hivyo kulazimika kufanya vitu nje ya sheria inanikumbusha Waziri Mkuu mwingine ambaye naye alikuja na kisingizio hicho hicho na kuamua kufanya vitu nje ya sheria. Sasa hivi na yuko nje ya serikali. Nitasikitika kama Pinda naye ameingia kwenye mtego huu wa kuanza kulewa madaraka au kulewa uchungu.

Niandikie: mwanakijiji@mwanakijiji.com

dickabudi
01-30-2009, 03:15 PM
Mwanakijiji ukimwona jambazi anauawa na polisi au halaiki unasemaje? Waziri Mkuu anasema ukimwaona mtu anamuua Albino basi nae auawe hasemi ukikisia kuwa hawa watu wanaua Albino waueni

Pia unasemaje unaposikia vijana wetu wa Blue Guard jitokezeni kwa bidii kuandamana hata ikibidi kufa kwa kutetea maslahi ya chama chetu kuweni tayari kufa nini maana yake katika mkusanyiko wa mkutano wa kisiasa

Naomba tuangalie kauli za mikutano ya hadhara na matamko rasmi ya serikali yaliyosainiwa kwa taratibu za kiserikali tusikuze mambo

mfumwa
01-30-2009, 04:24 PM
Naomba tuangalie kauli za mikutano ya hadhara na matamko rasmi ya serikali yaliyosainiwa kwa taratibu za kiserikali tusikuze mambo

Unafahamu tamko la kiongozi kama Waziri Mkuu (WM), akisema kuwa uwekwe ndani ni mpaka isainiwe?. Tamko la kiongozi linakuwa la kiofisi, mfano ukiambiwa na Rais ama Waziri Mkuu nimekuvua madaraka, pale alipotamka ndio madaraka yako yameisha. Rais anapovunja Baraza la Mawaziri hutamka tu, kama barua baadae.

Sasa WM anaposema kuwa wanaoua Albino wauawe na wewe unashabikia ni jambo la kushangaza. Yeye keshaomba msamaha kwa hilo. Huwezi linganisha Polisi wanapoua jambazi na wananchi wanaochukua sheria mkononi. Polisi kwanza wamefunzwa kwa hiyo kazi, na huwa hawaui tu, mpaka hao majambazi watakapoonekana wana silaha nzito, ama wamewazidi nguvu. Sasa kuruhusu wananchi wachukue sheria mkononi mahakama ziwe za nini?, na kama muuaji Albino auliwe na wananchi vipi wauaji wa vikongwe nk?.

Kama WM anavunja katiba, nani aisimamie?

dickabudi
01-30-2009, 04:58 PM
Ninachosema na anachosema WM ni kwamba alimanisha nini kwenye ule mkutano wa hadhara soma NIPASHE

Pia tunachotetea ni kwamba ameomba msamaha kwa waliomuelewa vibaya kwamba si mtaaluma amekurupuka na anachochea uvunjwaji wa sheria na si kwamba alichochea uvunjwaji wa sheria

pia ameelezea adha na matatizo wanayoyapat Ndugu zetu Albino, ametoa mfano wa mtoto yule wa Tabora aliyekatwa mkono, jiulize angekuwa mwanao unapambana na watu kama hao ungewafunga kamba na kuwapeleka Polisi??? Watu ambao tayari wamekuvamia ana wamekata mkono wa mwanao Albino na wanao

Unaposupport damu imwagike kwa mtu kuibiwa kura ni sawa na mtu kukatwa kiungo na ukangoja utawala wa sheria?

mwanakijiji
01-30-2009, 05:05 PM
Ninachosema na anachosema WM ni kwamba alimanisha nini kwenye ule mkutano wa hadhara soma NIPASHE

Pia tunachotetea ni kwamba ameomba msamaha kwa waliomuelewa vibaya kwamba si mtaaluma amekurupuka na anachochea uvunjwaji wa sheria na si kwamba alichochea uvunjwaji wa sheria

pia ameelezea adha na matatizo wanayoyapat Ndugu zetu Albino, ametoa mfano wa mtoto yule wa Tabora aliyekatwa mkono, jiulize angekuwa mwanao unapambana na watu kama hao ungewafunga kamba na kuwapeleka Polisi??? Watu ambao tayari wamekuvamia ana wamekata mkono wa mwanao Albino na wanao

Unaposupport damu imwagike kwa mtu kuibiwa kura ni sawa na mtu kukatwa kiungo na ukangoja utawala wa sheria?

Hajaomba msamaha kwa kauli yake (sikiliza kwenye podcast tumeweka hotuba yote akijibu swali hilo Bungeni). Na alichosema na kukitetea siyo alicho"maanisha" alimaanisha alichosema.

mfumwa
01-30-2009, 05:53 PM
Ninachosema na anachosema WM ni kwamba alimanisha nini kwenye ule mkutano wa hadhara soma NIPASHE

Pia tunachotetea ni kwamba ameomba msamaha kwa waliomuelewa vibaya kwamba si mtaaluma amekurupuka na anachochea uvunjwaji wa sheria na si kwamba alichochea uvunjwaji wa sheria

pia ameelezea adha na matatizo wanayoyapat Ndugu zetu Albino, ametoa mfano wa mtoto yule wa Tabora aliyekatwa mkono, jiulize angekuwa mwanao unapambana na watu kama hao ungewafunga kamba na kuwapeleka Polisi??? Watu ambao tayari wamekuvamia ana wamekata mkono wa mwanao Albino na wanao

Unaposupport damu imwagike kwa mtu kuibiwa kura ni sawa na mtu kukatwa kiungo na ukangoja utawala wa sheria?

Ndugu yangu, unazungumza aliyosema WM, ama unatoa yako yaliyo moyoni?, sidhani kama hapa kuna haja ya kuendelea na mjadala. Kama unataka unayoyaamini ndio nami niyaamini sitafanya hivyo manake huyo WM nimemsikia kiasi. WM alisema hilo lipo, kuomba msamaha ni jambo jingine. Na kama akiomba kwa kukubali alisema, NAMI NITAMSAMEHE sababu yeye si Malaika, ila asizungushe zungushe. Unadhani kama sio ulegelege wao haya mauaji mpaka sasa yangefikia Albino karibia 43.

Sio mwanangu tu akiuawa, mimi mtu yoyote akiuawa naumia. Binadamu si ng'ombe, siangalii maslahi yangu unapokuja utu. Hivyo vikongwe wanapouliwa kanda ya ziwa, watu wafao kwa ajali, watu wanaokufa sehemu zenye vita (somalia, RDC nk), watu wanaouliwa na wananchi wenye hasira nk. Mimi huwa naumia sana.

Wapi nimesupport damu imwagike kwa mtu kuibiwa kura?

mfumwa
01-30-2009, 06:55 PM
Hajaomba msamaha kwa kauli yake (sikiliza kwenye podcast tumeweka hotuba yote akijibu swali hilo Bungeni). Na alichosema na kukitetea siyo alicho"maanisha" alimaanisha alichosema.

Mwanakijiji, mbona katika podcast naona mengine, hii ya hotuba yake WM akijibu swali Bungeni mbona siioni?.

dude
01-31-2009, 10:01 PM
mwanakijiji pamoja na kwamba huwa nakubaliana na hoja zako moja kwa moja kwa hili la pinda imebidi nitofautiane na wewe,kuna siku nilikuwa naangalia tv katoto kamoja kaalbino kalikoswa koswa kuuwawa chozi lilinitoka honestly.sasa pale katika hali ile ndo namwona mtu aliyetaka kumuua yaani siwezi kufikilia tena sheria inasemaje lazima nimuattack,same thing happened to pinda..kwa pinda tumsupport tu kwani ni kiongozi shupavu na muadilifu,and the good thing with pinda sio mwanasiasa anasema wat he feels lakini angekuwa mwanasiasa pale ndo angeanza kupindisha pindisha maneno..wako viongozi wengi tu waliovurunda na kulitia hasara taifa nafikili tuconcetrate na hao hii kauli ya pinda wala haina impact katika uchumi wetu
aluta continua

dickabudi
02-03-2009, 09:59 AM
Chama cha Albino Tanzania (TAS) Mkoa wa Mwanza, wanaharakati na baadhi ya maaskofu nchini, ?wamemkingia kifua? Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuhusu kauli yake ya kuwalinda albino na kuwataka wabunge na wanasiasa waache kumkebehi.

Mkoani Mwanza katika maandamano ya amani yaliyoandaliwa na TAS jana, Mwenyekiti wa Mkoa, Alfred Kapore, alisema jamii ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini, inasikitika kutokana na maumivu wanayoyapata albino wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla, na kuwashukuru wote ambao wamekuwa bega kwa bega kuwaunga mkono kwenye maisha yao ya kila siku.

"Tumesikitishwa na kauli iliyotolewa na baadhi ya wabunge kwa kupinga hatua zilizochukuliwa na Waziri Mkuu Pinda, dhidi ya watu wanaoua albino. ?Hivi nini majukumu yao ? sisi tumewachagua kutatua matatizo, hatukupendezwa na kauli hiyo. Sisi tunakufa wao wanatetea wauaji kwa kisingizio cha haki za binadamu.

Mbunge aliyetoa kauli hiyo bungeni, atueleze kauli yake ina maana gani kumuuliza Pinda?? alihoji Kapore. Alisema athari za mauaji hayo ni kubwa na zinajenga hofu kiafya, kijamii na kiuchumi na kushindwa kufanya shughuli za uzalishaji, zaidi watoto wa jamii ya albino wamekuwa wakiishi katika mazingira ya kutoroka nyumba zao.

Aliiomba mahakama kuhakikisha inatoa hukumu haraka kwa watu waliokamatwa na watakaokamatwa kwa kujihusisha na mauaji ya albino na vikongwe. Pinda katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu bungeni Alhamisi iliyopita, alitetea kauli yake aliyoitoa katika ziara ya Kanda ya Ziwa, ambapo alieleza uchungu wa mauaji ya albino, kiasi cha kutoa chozi akitetea watu hao wasiuawe, na kwamba Serikali haitavumilia wauaji.

Kaimu Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Sheikh Hamis Almasi, alisema watakaokamatwa kwa mauaji ya albino wauawe hadharani kwa risasi tena mchana, ili watu washuhudie. Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa wa Mkoa wa Mwanza, Askofu Isaya Zenobius, alisema wanaunga hatua inayochukuliwa na serikali ya kupambana na wauaji wa albino kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Jijini Dar es Salaam, wanaharakati wa masuala ya haki za watu wenye ulemavu walishangazwa na Kiongozi wa Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed, kwa kitendo chake cha kumkebehi Pinda na kusema si cha kiungwana. Mmoja wa wanaharakati hao, Josephat Tona, alisema machozi yaliyomtoka Pinda akiwa bungeni yamewagusa wengi kwani alilia kwa sababu ya albino na watu wengine wenye ulemavu wa viungo.

Alisema wanamshangaa Hamad kutaka Pinda atoe ufafanuzi wa kauli yake aliyoitoa kuwa anayeua albino naye afe na kuhoji kuwa hadi sasa albino 43 wamekufa, ?inakuwaje haoni uchungu wa mauaji hayo, badala yake wapinzani wanadai Pinda analilia uwaziri mkuu!? ?Hivi wapinzani wanataka nini ? mauaji ya albino ni ukatili na hayawezi kufumbiwa macho, na Waziri Mkuu alikuwa akililia albino si uwaziri wake.

Hao wapinzani wanaosema hivyo baadhi yao wazazi wao ni walemavu, kwa hiyo hili ni janga la Taifa na tunaandaa siku maalumu kwa ajili ya kukumbuka albino waliokufa,? alisema Tona. Aidha, aliwataka wabunge wanaowakilisha watu wenye ulemavu bungeni kujiuzulu, kwa kushindwa kumuunga mkono Pinda kutokana na mauaji yanayoendelea yanayosababisha baadhi ya albino kukosa viungo.

Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa, alisema kauli ya Pinda inapaswa kuungwa mkono na hakuna sababu ya kumshutumu. Dk. Malasusa alisema pamoja na uchungu alionao Pinda juu ya mauaji ya albino, bado kuna watu wanamsakama kana kwamba vitendo hivyo ni vizuri.

?Tunahitaji kumuunga mkono Waziri Mkuu Pinda ? pia tunahitaji sala na maombi kwa ajili ya jambo hili, kwani hao pia ni ndugu zetu, wana haki zote kama sisi,? alisisitiza. Alisema wanaomshutumu Pinda wanakosea, kwa kuwa adha na vitendo vya unyama na vya kikatili wanavyofanyiwa albino havipaswi kuvumiliwa. Alisema ikiwa Watanzania wote wangeguswa na mauaji hayo ya albino kama alivyoguswa Waziri Mkuu, tatizo hilo lingetoweka, na kwamba kinachohitajika sasa ni wanajamii wote kuungana na kupiga vita mauaji hayo.

?Hali ni mbaya, nasi tuguswe tuchukue hatua za kuwafichua wauaji ? kauli yake ya kutowavumilia wauaji wa albino, alikuwa sahihi na hatuoni sababu yoyote ya msingi ya baadhi ya watu kumshutumu, hasa ukizingatia kuwa ukatili unaofanywa dhidi ya albino ni mkubwa na wa kinyama,? alisema Askofu Malasusa. Hadi sasa idadi ya albino waliouawa ni zaidi ya 50 nchini, ambapo mauaji hayo yamekuwa yakihusishwa na imani za ushirikina ambapo wauaji hunyofoa baadhi ya viungo na kutokomea navyo.