PDA

View Full Version : Tume ya maadili ya viongozi imebweteka!



mwabaudi
02-04-2009, 12:14 PM
Nimesoma kijarida maridhawa cha CHECHE ZA FIKRA juzuu 7 toleo 25, awali napenda kusema kwamba bodi ya uhariri imefanya kazi nzuri kuibua vyanzo vinavyoboresha ufahamu wa uma juu ya ufisadi na mstakabali wa nchi yetu, pamoja na mambo mengine taarifa hizi zinatoa taswira ya ulegevu wa Tume ya Maadili ya viongozi wa Uma, Tume inaonekana kwamba ilibweteka kwa muda mrefu badala ya kuwa ndio chachu ya kuhakikisha kwamba maadili ya viongozi yanafuatwa! Inakuwaje basi mtu asitaje mali zake kwa Tume na baada ya Tume kupata taarifa hizi toka vyombo vya habari ilichukua hatua gani?

mwanakijiji
02-04-2009, 05:03 PM
Uzito wa Tuhuma na Utamaduni wa kuwajibika

Na. M. M. Mwanakijiji

Tunapoendelea kujadili suala hili naomba niongeze haya kidogo. Katika nchi ya utawala wa sheria au inayojaribu kujenga misingi ya demokrasia tuhuma dhidi ya kiongozi yeyote yule wa umma (anayechaguliwa au kuteuliwa) zipimwe uzito wake na kwa kuangalia uzito huo na hasa uzito wa ushahidi unaotolewa (preponderous of evidence) ufikie mahali kutosha kumwajibisha mtu.

Mojawapo ya ulaghai wa watawala wetu ni kudai "tusubiri mahakama" au tusimhukumu mtu hadi mahakama ifanye uamuzi. Sasa hilo kwa juu linatosha kuvutia macho lakini ninaamini katika uongozi wa kisiasa au wa umma utamaduni wa kuwajibika utaanza kujikita pale tu ambapo tuhuma nzito haziwezi kuendelea kuvumiliwa.

Katika sakata la Chenge tukumbuke kuwa hakujiuzulu kwa sababu ya tuhuma kuwa anafedha kiasi fulani nje ya nchi. Kilichomtibulia Chenge ni maneno ya kuziita fedha hizo kuwa ni "vijisenti vichache". Watanzania wengi walichukizwa na maneno ya "vijisenti" kuliko fedha alizokutwa nazo au jinsi alivyokutwa nazo. Nina uhakika kama Chenge angefunga mdogo wake na kulia "tusubiri mahakama na uchunguzi uishe" wala asingekwenda popote.

Baada ya aliyekuwa Mkuu wa Tabora Bw. Ditopile Mzuzuri kutuhumiwa kufanya mauaji nilikuwa mtu wa kwanza tena kutaka ajiuzulu mara moja au Rais amsimamishe kazi mara moja. Sikuhitaji mahakama kuniambia kuwa mazingira ya tuhuma zinazotolewa ni nzito mno kiasi kwamba hawezekani kuendelea kuwa mtumishi wa serikali wakati huo huo. Tuhuma za mauaji dhidi yake na uzito wa ushahidi (picha, damu, n.k) vilitosha kabisa kumfanya ajiuzulu dakika inayofuata.

Ndio maana nilichukizwa na kitendo cha Rais kusubiri masaa mengi hadi Dito alipojiuzulu wadhifa huo na hivyo kulinda pensheni yake n.k Cha kushangaza zaidi alionesha maneno ya huruma ambayo naamini yalikuwa na lengo la kuntaint mchakato wa sheria kwa kumwagia huruma kwa Ditopile.

Uzito wa tuhuma dhidi ya Chenge na Dr. Idris ni mkubwa mno. Tuhuma hizi hata hivyo zimekuwepo kwa muda. Inawezekana vipi watu hao wakaendelea kudhaminiwa uongozi wa taifa na hata kupewa nafasi ya Ubunge?

Kwamba Chenge imeshasema hajatoa taarifa ya mali yake kwenye Tume ya Maadili kinyume na sheria ya Maadili ilitosha kabisa kutopata nafasi ya kugombea kule Bariadi. Lakini cha kushangaza ni kuwa alipewa nafasi ya kugombea Ubunge, akateuliwa Waziri mara mbili na mojawapo ya Wizara ambazo alipewa kusimamia ni ile ya Miundo Mbinu (ambayo ilikuwa inahusika na rada!)

Chenge alistahili awe amevuliwa madaraka yake yote mara moja hata kama si kwa mujibu wa utamaduni wa uwajibikaji lakini kwa kuangalia Katiba ya CCM na Mwongozo wa Maadili wa 2002. Katika mwongozo wa maadili CCM yenyewe inasema hivi kuhusu kiongozi wake "Jukumu la Kiongozi wa CCM katika kukijenga na kukilinda Chama ni kubwa. Athari katika Chama za Kiongozi kutenda maovu, au kutotimiza wajibu, ni kubwa kiasi kwamba Maadili yake yakitetereka Chama kitavurugika; na nchi itakwenda mrama."

Je kutetereka kwa uongozi wa CCM na kwenda mrama kwa nchi kumesababishwa na ubovu wa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa CCM na hivyo kuonesha uhusiano wa moja kwa moja wa matendo ya mtu mmoja na hatima ya taifa?

Kwenye suala la Chenge inashangaza zaidi; mtu ambaye anatuhumiwa kupinda sheria, anatuhumiwa kuvunja sheria na ambaye amegubikwa na tuhuma za ufisadi hadi na vyombo vya nje ndiye yeye wakati huo huo anapewa nafasi ya kuongoza Kamati ya Maadili ya CCM ambayo kichama ndiyo inatakiwa kumchunguza hata yeye mwenyewe? Na ndiye huyo huyo aliyepewa nafasi ya kutoa maoni yake kuhusu maadili ya viongozi wengine wakati yeye amezibwa na ukungu mkubwa mweusi wa kashfa!

Dr. Idriss kwa upande wake ni hivyo hivyo. Tuhuma dhidi yake siyo ngeni pia lakini inashangaza kuwa wakati alipopata nafasi ya kujiuzulu na alipotaka kuachia ngazi badala ya kumuacha aondoke angalau aonekane kama shujaa sasa kuna kila dalili ataondoka kwa kashfa.

Haya yote yanatulazimisha kuhoji swali moja kubwa:

Je, yawezekana kuwa ile imani kuwa Usalama wa Taifa wanafanya uchunguzi (vetting) ya viongozi watarajiwa haina msingi wowote katika ukweli? Je yawezekana shughuli hiyo isifanywe na usalama wa taifa bali na tume ya maadili ya viongozi wa umma ambayo inatakiwa iwe huru kutoka mikono ya uteuzi wa Rais na iwajibike moja kwa moja kwa Bunge? Je yawezekana kwa kuwa na mchakato mbovu kabisa wa kupata viongozi wa juu ndivyo vivyo hivyo nchi yetu itaendelea kuwaweka madarakani viongozi, wabadhirifu, walaghai, wenye tamaa na ambao ndani ya mifupa yao chembe za ufisadi zinatengenezwa kila sekunde?

Wakati umefika wa uzito wa tuhuma dhidi ya kiongozi yeyote na hasa ushahidi unaoneshwa mbele vitoshe kabisa kumfanya kiongozi huyo aachie ngazi na hayo ya kisheria au mahakamani yaendelee mbele ya safari.