PDA

View Full Version : Kuna matatizo Bungeni!



mwanakijiji
02-11-2009, 05:07 PM
Hii ni makala yangu iliyotoka kwenye Tanzania Daima tarehe 11 FEB, 2009


NILIKUWA najaribu kutafuta jinsi ya kuanza makala hii ya leo.

Mifano mbalimbali ambayo ningeweza kuanza nayo naona yote haifai isipokuwa niseme tu moja kwa moja bila utata, kujiuma uma au kubania maneno.

Ndugu zangu Watanzania, tuna tatizo bungeni, tuna tatizo na wabunge, tuna tatizo na mfumo mzima wa bunge hususan linapokuja suala la usalama wa wawakilishi wetu bungeni.

Tunaweza kutafuta maneno ya kupindisha au hoja za kuzungushana lakini kama inavyosemwa katika mithali kuwa ?msema kweli ni mpenzi wa Mungu?, nimejitolea kusema ukweli ambao kila mtu mwenye fikra huru anajua ndivyo ulivyo. Hadi hivi sasa hatujafanya juhudi za kina na za wazi kuhakikisha kuwa wabunge wetu wapo salama na hivyo tumekuwa tukizembeazembea na mara kadhaa tumeshalipa gharama kubwa mno na tumelipa hadi ile gharama kuu ya uhai.

Cha kuudhi hata hivyo si kwamba hatujui tatizo bali tatizo lenyewe hata tukilijua hatuna muda mrefu wa kulifikiria na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Hata tukitaka kutafuta ufumbuzi wa kudumu kumbukumbu zetu ni fupi mno kiasi kwamba kabla hatujafika mahali pa kutafuta ufumbuzi tunakuwa tumeshasahu tatizo lenyewe!

Kifo cha Amina Chifupa

Mojawapo ya mambo ambayo tumekwepa kuyafikiria ni mazingira ya kifo cha Mbunge wa Jamhuri ya Muungano, Amina Chifupa.

Mara baada ya siku ile ambapo Amina alizungumza na vyombo vya habari na kuahidi kuwa atasema ukweli wote juu ya wabaya wake, ni wazi kuwa alikuwa amejiweka katika mazingira magumu.

Je, kulikuwa na uwezekano wowote wa Amina kuzungumza tena hadharani? Jibu langu wakati ule lilikuwa ni ?hapana?.

Tuliposikia kuwa familia imeamua kuwa Amina hatozungumza tena, kengele za tahadhari zililia kwenye kichwa changu na nilikuwa mtu wa kwanza kutaka Amina aachwe aseme alichotaka kusema bila kujali gharama yoyote ile. Kilichonishtua zaidi ni kuwa Amina alionekana amefichwa kwa muda mrefu na hakuna mtu aliyejitokeza kumtetea!!

Mbunge wa Jamhuri ya Muungano ameshikiliwa bila ya mawasiliano na mtu mwingine (incommunicado) na hakuna mtu aliyeshtuka. Si DPP, si DCI, si Spika, si Ikulu, si nani. Ati ni suala la familia, kana kwamba Amina alikuwa ni mtoto mdogo.

Baadaye wanatutangazia kuwa amefariki na pamoja tunatakiwa kukubali ?mapenzi ya Mungu?! Niliandika kwa ukali wakati ule kukemea dhamira zetu zilizopigwa ganzi. Tukanung?unika pembeni, tukasema pembeni. Tukasahau. Tukasubiri tukio jingine.

Kifo cha Mhe. Juma Akukweti

Fikiria kifo cha Mhe. Juma Akukweti kufuatia majeraha yaliyotokana na tukio la ajali ya ndege pale Mbeya.

Akukweti alikwenda pale kuangalia tukio la kuungua kwa Soko la Mwanjelwa na alipokuwa akirudi Dar ndipo alipanda ndege ndogo ambayo ilishindwa kuruka, kuanguka na kuungua.

Mazingira ya kifo hicho na safari hiyo ya ndege yanatufanya tuhoji kama yote yalifanyika kuhakikisha usalama wa mbunge huyo na abiria wengine waliofuatana naye na ambao wengine pia walifariki?

Safari ya kutoka Mbeya hadi Dar ni safari ya masaa machache tu na ni ndani ya siku moja. Kwanini kulikuwa na haraka ya kurudi Dar kiasi cha kuamua kupanda ndege hii ambayo taarifa za awali zilisema ilikuwa imebeba mizigo mingi kuliko uwezo wake?

Rais Kikwete alipomtembelea Mhe. Akukweti pale hospitali alizungumza na kusema: ?Nimesikitishwa sana na ajali hii, na yote yaliyotokea pamoja na kupotea kwa maisha ya watu wawili, lakini haya yote ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu.?

Sasa sina mashaka katika yeye kusikitishwa, lakini kweli tunaweza kusema ni mapenzi ya Mungu? Tukanung?unika pembeni, tukasemea pembeni. Tukasahau. Tukasubiri tukio jingine.

Kifo cha Mhe. Salome Mbatia

Mbunge mwingine aliyefariki dunia katika mazingira ya ajabu na yenye kuhoji uwezo wetu wa kulinda viongozi wetu ni Mhe. Salome Mbatia ambaye hadi kufa kwake alikuwa ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.

Kifo chake kilitokea baada ya gari lake kugongana na lori huko Iringa.

Mojawapo ya vitu ambavyo niliandika wakati ule ni kuwa kwanini mbunge ambaye haendeshi gari mwenyewe (abiria) anakaa kiti cha mbele cha abiria badala ya nyuma kama wanavyofanya majaji au viongozi wengine?

Jibu tuliloambiwa wakati ule na bado sijalielewa-marehemu Mbatia alikuwa na dereva mwingine (si dereva wake wa kawaida) na alikuwa anaendesha gari yake mwenyewe.

Kwa maneno mengine, hakuna utaratibu unaoeleweka wa wabunge kusafiri.

Tukaona picha za ajali, tukasikitika. Tukanung?unika pembeni, tukasema pembeni. Tukasahau. Tukasubiri tukio jingine.

Hadi leo hatujajiuliza yule dereva wa lori alipotelea wapi?

Si bungeni, si vyombo vya habari, si nini! Tumekubali!

Ajali za Wah. Mudhihir Mudhihir, Juma Kapuya na Zainab Vulu.

Wakati tukiwa hatujapoa vizuri au kutulia wabunge wengine wakawa katika ajali zilizotishia maisha yao.

Ile ya Mudhihir Mudhihir ilisababisha apoteza mkono wake mmoja, ya Kapuya kusababisha majeraha makubwa na ya Vulu vivyo hivyo. Tunamshukuru Mungu na jitihada za madaktari kuokoa maisha yao vinginevyo orodha ya wabunge waliotutoka ndani ya miaka hii mitatu katika ajali ingetufanya tuhoji kama yawezekana ubunge ni kazi ya mkosi zaidi!

Tukakubali kuwa ni ?ajali na mapenzi ya Mungu? bila kupima kama yumkini tungeweza kuepusha ajali hizo.

Kifo cha Mhe. Chacha Wangwe

Kama vile katika ajali ya Mbatia, Mhe. Wangwe naye akapanda gari na dereva sijui kutoka wapi na hata sijui alikuwa na sifa gani za kuweza kumwendesha mbunge.

Yaani katika Tanzania mtu yeyote anaweza kumpatia usafiri mbunge na kwenda naye popote bila kujali mtu huyo ni nani!

Ajali ikatokea katika mazingira ya ajabu kabisa na sasa kesi iko mahakamani lakini tunajiuliza, hivi kweli yote yalifanyika kuhakikisha wabunge wetu wako salama? Kweli kama gari lilikuwa bovu au lina matatizo wabunge wanaweza kupeleka magari yao mahali popote pale?

Tuliohoji na tulihoji tena kwa hoja. Lakini, kwa ujumla wetu kama taifa tukakubali yakaisha!

Tukio la ?unga unga? bungeni

Tukiwa tunajaribu kutuliza mawazo likaja tukio la ?ndumba? bungeni ambapo hadi leo hii nina uhakika wananchi tumeuziwa mbuzi kwenye gunia.

Mara tuliambiwa kuna video zimerekodiwa kuonyesha kilichotokea, mara wachunguzi wakaja baada ya masaa kadhaa na baada ya Bunge kutumika wakachukua ?vumbi? kwenda kulichunguza huko Dar. Majibu yakaja na kutuambia hakukuwa na kitu!

Tukaambiwa watu wamepagawa tu na ni washirikina.

Waandishi wakaonywa kutokuandika mambo ya kishirikina sana kwani tutatishia wawekezaji! Tukakubali.

Nina uhakika kama wangekufa wabunge kumi wiki ile wananchi tungelia, tungepigwa na hamaki, na kama watu waliolishwa dawa fulani tungeanza kuimba ?mapenzi ya Mungu!?

Tukio la Dk. Slaa na Dk. Tarab

Sasa kilele cha jinsi tunavyowalinda wabunge wetu kimetokea wiki iliyopita.

Hivi ile Ijumaa kama Watanzania wangeamka na kusikia Dk. Slaa amepatwa na janga hata mauti ni nani angejua juu ya hivyo vifaa?

Vipi kama wote wawili vyumba vyao vingeungua wenyewe wakiwa ndani na baadaye tukaambiwa kulitokea ?shoti ya umeme? na tukaimbiwa hadi kwa machozi kuwa yalikuwa ni mapenzi ya Mungu, kweli tungejua juu ya chupa ya mvinyo na vidubwasha vya kielektroniki vilivyokutwa kwenye vitanda vyao?

Sasa kwa vile wanatufikiria sisi hamnazo, kuna watu wanataka tuamini ati wabunge hawa walijiwekea vifaa hivyo wao wenyewe ili kutafuta sifa au kujipa ujiko. Na kuna mtu mwingine amekuja na nadharia kuwa ati wake zao kutokana na wivu walienda kutafuta vifaa hivi na kuviweka kwenye hivyo vyumba! Siwezi kushangaa kuna watu wanaamini porojo hizo!

Cha kushangaza wale wale Polisi walioboronga uchunguzi wa ?unga unga? ndio wale wale ambao leo wanatakiwa kuchunguza vifaa hivi ambavyo wanajaribu kutuambia ati ?vinapatikana kiurahisi?. Lengo ni kutaka tuchukulie kuwa mtu yeyote anaweza kuvipata lakini hakuna anayeuliza kuna usalama gani katika maeneo ambapo wabunge wanalala?

Na hapa sijazungumzia ajali nyingine na matukio mengine ambayo msomaji unaweza kuyafikiria.

Ningeweza kusema mengi, lakini nakataa kusema ninachofikiria zaidi. Nakuomba wewe ufikirie kuwa serikali ya CCM iko tayari kurudia uchaguzi kwa mabilioni ya hela kuliko kuhakikisha ulinzi wa wabunge wetu.

Wamerudia uchaguzi wa Tunduru na Tarime na gharama nyingine nyingi kwa kiasi ambacho naamini kingeweza kabisa kulipia maafisa wa polisi, kampuni za ulinzi au hata madereva wa kudumu wa wabunge hawa!

Na kwa mtindo huu wa kurudia uchaguzi mdogo ni gharama kubwa sana kwa taifa endapo siku moja itatokea kundi kubwa la wabunge wafariki dunia au kwa namna moja washindwe kuendelea na ubunge wao. Hatuwezi kuwalinda wabunge wetu, hatuwezi kulinda Benki Kuu, hatuwezi kulinda maliasili zetu, hatuwezi kulinda watoto wetu, sisi tupotupo tu!

Nina mawazo ya mapendekezo lakini kwenye taifa la wasahaulifu na wasiojali majanga kama la kwetu tuseme nini? Tupendekeze nini bila kuonekana ?wajuaji??

Tutoe ushauri gani kabla hawajatushikia bango na kusema si mrudi nyumbani?

Ninachosema ni kuwa huu ndiyo mwaka mpya, na kama matukio yetu ya usahaulifu huko nyuma ni ishara ya kile kilichoko mbele yetu, basi tujiandae mwaka huu kwa mambo mengine ambayo wengine watasema ni uchuro!

Majanga yatakayotokea mwaka huu ni majanga yanayojulikana na yanaweza kuepukika.

Lakini kwa vile kujiandaa inahitaji kumbukumbu na sisi hatuna kumbukumbu nzuri basi tujiandae kwa machozi!! Tuendelee kusubiri tu hadi yatukute mengine.

Hata hivyo nitatoa pendekezo langu la nini kifanyike. Wiki ijayo, nikikumbuka.