PDA

View Full Version : Mwakyembe na Wengine 7



mwanakijiji
02-26-2009, 11:13 PM
Nipashe

Yule mbunge machachari aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza mchakato wa zabuni ya mkataba wa kufua umeme uliotolewa kwa kampuni feki ya Richmond na ripoti yake kuzua balaa kubwa, Dr. Harrison Mwakyembe ameibuka na kuelekeza mashambulizi yake kwa mafisadi.

Dr. Mwakyembe ambaye ni Mbunge wa Kyela, aliibuka na hoja mpya mwishoni mwa wiki alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kahama wakati wa uzinduzi wa benki ya wanakijiji ijulikanayo kama VICOBA-Kahama katika ujumbe wa wabunge wanane wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Dk. Mwakyembe alisema kuna kila dalili za kushinda vita dhidi ya mafisadi kwa sababu Rais Jakaya Kikwete pia yuko mstari wa mbele katika vita hivyo.

Alisema ni aibu kubwa kwa mafisadi kuanzisha magazeti, ambayo dhamira yake ni kuchafua na kutukana watu.

?Sasa hivi wameanzisha magazeti, nawaomba muwapuuze na tusonge mbele katika vita yetu hii, ambayo mwisho wake ni kuondoa umaskini nchini? Alisema Dk. Mwakyembe.

Naye Mbunge wa Vunjo Aloyce Kimaro, alisema kuna matajiri wengi hapa nchini, ambao fedha wanazomiliki si za halali na hawathubutu kujitokeza kusaidia maskini.
Alimtaja Mwenyeki wa Makampuni ya IPP (wachapishaji wa Nipashe -MM) Bw. Reginald Mengi , kama mfano mzuri wa kuigwa kwani ni mfanyabiashara tajiri, safi, ambaye fedha anazomiliki ni za halali, na ndiyo maana amekuwa mstari wa mbele kusaidia maskini.

Kimaro alisema Rais Kikwete anachukia rushwa, dhuluma na mafisadi na kwa hiyo, akawataka Watanzania wamuunge mkono ili kutokomeza umaskini. Aliwafananisha wala rushwa na mchwa na kusema kwamba baada ya kuua vyama vya Ushirika na Mashirika ya umma, sasa wamehamia serikalini.

?Umaskini walionaoWatanzania leo unasababishwa na mafisadi, ni lazima tumuunge mkono Rais wetu ili hawa mafisadi walioko ndani ya serikali waondoke? alisema Kimaro

Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii alisema akiwa mmoja wajumbe wa iliyokuwa Kamati Teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa Richmond, anaamini walifanya kazi hiyo bila upendeleo wowote. Hata hivyo, alisema iwapo itathibitika kuna mtu walimuonea watajiuzulu nyadhifa zao za Ubunge.

Selelii alisema wamepata vitisho vingi kutoka kwa mafisadi, lakini walifarijiwa sana na Mengi. Alisema uwapo wa Mengi katika hafla ya uzinduzi wa VICOBA-Kahama, ni ishara tosha ya mwendelezo wa vita dhidi ya mafisadi na umaskini nchini.

Wabunge hao, ni miongoni mwa wabunge majasiri wasiokuwa na tabia ya kuumauma maneno kila wanapopata fursa ya kuzungumzia ufisadi.

Ripoti ya Kamati ya Dk. Mwakyembe ilisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa pamoja na mawaziri wawili , Nazir Karamagi aliyekuwa Nishati na Madini, na Dk. Ibrahim Msabaha aliyekuwa Ushirikiano wa Afika ya Mashariki kujiuzulu.

Kimaro alikuwa ni Mbunge wa kwanza ?kumfunga paka kengele? alipomtaja Rais Mstaafu Benjamin Mkapa bungeni kwamba, alihusika na kashfa ya kujiuzia mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira akiwa madarakani kwa bei ya kutupwa na kwa siri.

Pia Kimaro aliwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka nyumba za serikali, ambazo baadhi ya watumishi wa serikali walijiuzia kinyume na taratibu zirejeshwe. Bunge liliunga mkono hoja hiyo na kupitisha azimio la kurejeshwa nyumba hizo. Baadhi ya nyumba zimerejeshwa serikalini.

Wabunge wengine walioshiriki katika uzinduzi wa VICOBA na kuelezea kuunga mkono vita dhidi ya ufisadi ni Anna Lupembe (Viti Maalum), Aziza Ali (Viti Maalum), James Lembeli (Kahama), Devola Likokola (Viti Maalum) na Faida Bakari (Viti Maalum)