PDA

View Full Version : Mabadiliko upigaji kura za maoni CCM



mwanakijiji
03-09-2009, 05:05 PM
? Mabadiliko makubwa CCM

Na Theodos Mgomba, Dodoma (Uhuru)

HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya CCM imefuta utaratibu wa zamani wa upigaji kura za maoni kuwapata wagombea nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani, ambapo hivi sasa zitapigwa na wanachama wote badala ya wachache.

Utaratibu huo mpya utaanza kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwakani, ambapo kila mwanachama wa CCM atakuwa na haki ya kupiga kura za maoni kupitia Tawi lake, badala ya wajumbe wachache kufanya hivyo kupitia mkutano wa majimbo.

Uamuzi huo wa Halmashauri Kuu unalenga kumwezesha kila mwanachama kugombea uongozi, kuondoa malalamiko na vitendo vya rushwa, vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya wagombea wasiofuata maadili.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati, alisema katika kuhakikisha hilo linafanikiwa, wagombea wote watafanya ziara kwa pamoja na kutumia usafiri ulioandaliwa kwa gharama za Chama.

Alisema kabla ya kura za maoni, wagombea watapata fursa ya kutembelea matawi yote na kukutana na wana CCM kwa lengo la kujitambulisha na kuomba kura. ?Ziara hizi zitaandaliwa na CCM ngazi ya Wilaya na wagombea watasafiri kwa pamoja kwa usafiri ulioandaliwa na kugharamiwa na CCM.

Hatua hii ina lengo la kutoa haki sawa kwa kila mgombea kutembelea matawi yote na kujitambulisha,? alisema Chiligati. Alisema baada ya ziara ya kujitambulisha kukamilika, itapangwa siku moja ambapo wanachama wote watapiga kura kwenye matawi yao, ambapo alisema upigaji kura utaanza saa mbili asubuhi hadi saa nane mchana.

Chiligati alisema: ?Kamati ya Siasa ya Tawi itaweka utaratibu wa kuhakiki zoezi hili. Kura zitahesabiwa katika kituo husika na matokeo kutangazwa siku hiyo hiyo. Nakala ya matokeo itabandikwa hadharani nje ya ofisi ya Tawi, au mahali ambapo kura zitapigiwa ili yawe wazi. Kila mgombea atakuwa na haki ya kuweka wakala wa kusimamia upigaji kura, na zoezi la kuhesabu kura. Wilaya itaweka wasimamizi wa uchaguzi katika kila Tawi?.

Kwa mujibu wa Chiligati, baada ya kura kuhesabiwa katika kituo na matokeo kutangazwa, msimamizi wa kituo atatakiwa kupeleka matokeo hayo kwa Katibu wa CCM wa wilaya kwa njia yoyote ya haraka, kama kwa simu, na kwamba baada ya matokeo kutoka matawi yote kufika wilayani, Katibu huyo akisimamiwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya atajumlisha kura za kila mgombea.

Alisema wakati wa kazi hiyo, kila mgombea atakuwa na haki ya kuwepo mwenyewe au mwakilishi wake na kwamba baada ya kukamilika, vikao vya ngazi ya wilaya, mkoa na taifa vitakaa kuchambua kwa undani zaidi sifa za wagombea na kuzingatia kura za maoni walizopata, na hatimaye kuteua wagombea, ambao majina yao yatawasilishwa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Halmashauri Kuu pia imeagiza Kamati za Usalama na Maadili katika ngazi zote kuwa macho wakati wa kura za maoni, ili kubaini vitendo vya rushwa na kwamba atakayebainika kujihusisha navyo au kukiuka kanuni za uchaguzi, ataenguliwa katika kugombea na atafikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuongeza wabunge/wawakilishi wanawake kufikia lengo la asilimia 50, Chiligati alisema Halmashauri Kuu ya Taifa imependekeza kwa serikali kuwa idadi ya wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano iwe na ukomo wa viti 360.

?Hivyo fomula yoyote ya kuongeza idadi ya wabunge wanawake sharti izingatie ukomo huu? kwamba tuendelee na utaratibu uliopo sasa wa kuwapata wabunge/wawakilishi wa Viti Maalumu Wanawake. Isipokuwa kwamba idadi yao katika kila chombo ipatikane kutokana na asilimia 50 ya wabunge/wWawakilishi wote wa majimbo yaliyopo (hivi sasa yapo 232),? alisema Chiligati.

Alisema kwa kuzingatia kwamba Bunge litakuwa na ukomo wa viti 360 na kwamba idadi ya majimbo ya uchaguzi yaliyopo ni 232, idadi ya wabunge wanawake itakayopatikana itakuwa 116 (asilimia 50 ya wabunge wote wa majimbo) na kwamba, kuna wabunge wanawake saba watapatikana kwa mujibu wa Katiba ya nchi; hivyo kwa utaratibu huo, wanawake 109 ndio watakaopatikana kupitia Viti Maalumu. Akizungumzia kuhusu Zanzibar, alisema Halmashauri Kuu imependekeza kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka ukomo wa idadi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa 86.

?Kwa kuwa hivi sasa Baraza lina viti 50 vinavyotokana na majimbo ya uchaguzi, idadi ya wawakilishi wanawake watakaopatikana kwa njia hii itakuwa 25, yaani asilimia 50 ya wawakilishi wote wa kuchaguliwa katika majimbo yaliyopo, na kwa kuwa wawakilishi wanawake watano watapatikana kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar; hivyo wanawake 20 ndio watakaopatikana kutokana na Viti Maalumu,? alisema.

Alisema katika kuandaa orodha ya wagombea wanawake kwa nafasi 109 za Bunge la Muungano, nafasi 20 za uwakilishi zitakazogombaniwa, watapigiwa kura na vikao vya UWT.

Kwa hiyo wagombea ubunge/uwakilishi watapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa UWT Mkoa. Vivyo hivyo wagombea udiwani wa Viti Maalumu wanawake watapigiwa kura na Mkutano Mkuu wa UWT wa Wilaya.

Kwa upande wa serikali, Chiligati alisema Halmashauri kuu imependekeza kwa Serikali ya Muungano kurekebisha Katiba ya nchi na Sheria ya Uchaguzi ili kuweka ukomo wa idadi ya wabunge katika Bunge kuwa 360, na pia kuhalalisha kisheria utaratibu huo mpya wa kuwapata wabunge wanawake kupitia Viti Maalumu. Alisema: ?Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pia ibadilishe Katiba, na Sheria ya Uchaguzi ili kuweka ukomo wa idadi ya wawakilishi kuwa 86 na pia kuhalalisha kisheria utaratibu mpya wa kuwapata wabunge wanawake kupitia Viti Maalumu.

Ili kuongeza idadi ya wanawake katika Baraza la Wawakilishi, alisema NEC imependekeza Katiba ya Zanzibar ifanyiwe marekebisho ili kumwezesha Rais wa Zanzibar ateue wanawake wasiopungua watano miongoni mwa nafasi 10 alizonazo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar. Tamko kamili la NEC ukurasa wa 22.


Swali:
Fedha za kuwezesha mambo haya yote CCM watakuw wanazitoa wapi?

mohammedzahor
03-10-2009, 11:46 PM
ni hatua kubwa na ya msingi kufikiwa na vikao vya ccm, ila tunahitaji kwenda mbele zaidi ili lutanua wigo wademokrasia ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba kura hizi pia zinapigwa kwa maraisis watarajiwa, na ni vyema tuanze na kwa upande wa zanzibar ili wana ccm wajichagulie kiongozi wao wamtakae badala ya sasa kwamba wachache ndio waamuzi, pia tuhakikishe tunasimamia hili ili ufanisi upatikane, vyenginevyo bado tutakuwa tumetanua wigo wa rushwa tu, maan wako wenye uwezo wa kununua jimbo lote