PDA

View Full Version : Dr. Rashid huku ni kutushikia kisu shingoni!



mwanakijiji
03-10-2009, 09:14 AM
M. M. Mwanakijiji (Tanzania Daima Machi 7, 2009)

KUNA watu wamelewa madaraka. Kuna watu ambao wanaamini bila ya wao Tanzania haiwezi kwenda mahali popote; kwa hakika kuna kundi la watu ambao wanafikiri ya kuwa wao ndio zawadi ya Mungu kwa Watanzania na ya kuwa wao ni warithi wateule waliopakwa mafuta kurithi utajiri wa nchi hii.

Na wapo watu ambao kutokana na vyeo vyao au nafasi zao kijamii, wanaamini kuwa wanaweza kusema au kufanya lolote bila kujali matokeo yake.

Mmoja wao ni Dk. Idris Rashid. Sitaki kuzungumzia masuala yake ya rada au mambo mengine ya huko nyuma. Ninachoangalia leo ni jinsi gani mkurugenzi huyu wa TANESCO amevuka mpaka wa mjadala huru na kuwajibika kama kiongozi, na kuingia katika uwanja wa vitisho na ahadi ya kulihujumu taifa lake.

Katika taarifa yake ya kutangaza kuwa mpango wa TANESCO kununua majenereta ya umeme toka kampuni inayohusishwa na ufisadi na ambayo mmiliki wake hajulikani ya Dowans, Dk. Rashid amesema kitu ambacho kinastahili kumfukuzisha kazi dakika mbili tu baada ya kutoa ujumbe huo.

Ameandika anasema: ?TANESCO inatangaza rasmi kujitoa kwenye nia yake ya kununua mitambo hii. Ni imani yetu kwamba tumeishajieleza na kujenga hoja za kutosha, na wananchi wa Tanzania watafanya maamuzi yao hapo ambapo nchi itakapokuwa imegubikwa na kiza, mahospitali hayatoi huduma, viwanda havizalishi, wanafunzi vyuoni wanashindwa kusoma kwa sababu tulishindwa kufanya maamuzi.?

Kwamba vijenereta hivi vya Dowans vyenye uwezo wa kuzalisha chini ya megawati 200 kutovinunua kutasababisha kiama Tanzania, ni kejeli kwa Watanzania.

Kwamba hali ya umeme Tanzania imefikia pabaya kiasi cha kutegemea Dowans, ni sawa na kutushikia kisu shingoni na kutuambia tusiporuka tutachinjwa. Tatizo ni kuwa tunaambiwa turuke toka kwenye treni liendalo kasi.

Dk. Rashid atambue ya kuwa, Watanzania wako tayari kujaribu bahati yao kuruka toka kwenye treni kuliko kuchinjwa huku wanajiangalia.

Lakini kilichonitibua zaidi ni kuwa, mkurugenzi huyu anazungumza kana kwamba katika sayari nzima ya dunia (hata Zuhura), hakuna chanzo kingine chochote cha umeme, kwamba wataalam wote wa nishati wanakubaliana kuwa Dowans ndiyo ?mwokozi? wa sekta ya umeme. Kwamba hakuna chaguo jingine na hakuna njia nyingine ya kukabiliana na tatizo hili.

Ninachoona ni kuwa, kwa vile tumewakatalia kununua mitambo hii; kwa vile tumewapinga mpango wao huu, kwa vile tumeonyesha kuwa kwa kutulazimisha kununua mitambo ya Dowans wanataka kuwalipa makuwadi wao wa ufisadi, sasa timu yao imejipanga kulipa kisasi. Wamejipanga kuwaonyesha Watanzania kuwa ?tutakiona cha mtema kuni?.

Kama vile yule waziri aliyetuapisha kuwa tule majani ilimradi ndege ya rais inunuliwe. Sasa hivi ni yeye ambaye tumbo lake linamsumbua kila kukicha akifikiria hatima yake.

Ni kwa sababu hiyo tuna ujumbe mmoja tu kwa Dk. Rashid na wapambe wenzake wa vitendo vya kifisadi. Watanzania tumechoka na vitisho, tumechoka na ahadi za kuzimu, na kwa hakika tumechoka na viongozi ambao wanafikiri kuwa wanaweza kufanya lolote alimradi wana tai zinawaning?inia shingoni.

Tunamkatalia nguvu hizo, tunamkatalia nafasi hiyo na yeye na wenzake waamue kujiuzulu. Hawawezi kuendelea na nafasi zao wakati wametushikia kisu shingoni. Hawawezi kusimamia sekta ya nishati wakati wameshatuambia kuwa kiama chaja.

Waamue kujiuzulu au wafukuzwe kazi. Vinginevyo tutaitisha maandamano nchi nzima kupinga uongozi wao na wajue ya kuwa Watanzania si ?mabwege?.

Kwamba, ukimya na utulivu wetu si hulka tuliyozaliwa nayo, bali ni uamuzi tuliochukua tukiweka maslahi ya jamii yetu mbele. Wasifikiri kuwa Watanzania hawawezi kupatwa na hasira na kufanya vurugu kama tunavyoziona nchi nyingine.

Wasitulazimishe tufikie huko, wasitusukume hadi kujiona kama paka wanaopigwa wamefungiwa ndani ya nyumba. Wasituchezee kama wanaotuona ni mbwa koko. Kuna wakati tutasimama na kupigania haki yetu ya kuwa huru na kuheshimiwa. Tutasimama na kuwaambia ?sasa yatosha. Hamuwezi kutusukuma tena, hamuwezi kutupiga tena, hamuwezi kututisha tena.?

Kwani, mwaka huu si mwaka wa mafisadi. ?Hamuwezi kututawala mpendavyo.? Dk. Rashid na watetezi wenzako wa majenereta ya Dowans, kama hamuwezi kusimamia TANESCO na kuhakikisha hakuna tatizo la umeme siku za karibuni, basi muachie ngazi kwa hiari yenu kabla hatujawalazimisha kwa maandamano.

Kama hamuwezi kufikiri njia nyingine bora, za gharama nafuu kuliko majenereta ya Dowans kutumika kuondoa upungufu wa umeme, basi mmeshindwa kuongoza. Hamuwezi kutishia nchi, mkaendelea na madaraka yenu. Hamuwezi.