PDA

View Full Version : Tufunge mjadala wa Dowans - Ngeleja



mwanakijiji
03-15-2009, 07:57 AM
NA JOSEPH BURRA (Uhuru)

SERIKALI imesema nchi haitaingia gizani endapo mitambo ya kufua umeme wa Dowans hautanunuliwa.

Imesema inafanya kila jitihada kuhakikisha hakutakuwa na mgawo wa umeme, hata bila mitambo hiyo.

Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, alisema si nia ya serikali nchi kuingia kwenye mgawo wa umeme.

Ngeleja alisema mikakati inafanyika kukabiliana na tishio la upungufu wa umeme ili kuzuia kutokea kwa hali hiyo.

Waziri Ngeleja alikuwa akizungumzia hali ya upatikanaji umeme nchini na kutoa ufafanuzi wa mijadala iliyojitokeza hivi karibuni kuhusu nia ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kununua mitambo ya Dowans.

"Suala la kununua mitambo si la kisiasa bali la kitaalamu, tunaomba mjadala kuhusu dowans ufungwe, hatuwezi kuendelea na jambo ambalo linawachanganya wananchi... tunafanya kila linalowezekana kukabiliana na upungufu wa umeme, wananchi wasiwe na hofu hakutakuwa na mgawo wa umeme," alisema Ngeleja.

Kauli ya Ngeleja imetofautiana na vitisho vilivyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Idris Rashidi, kwamba nchi ikiingia gizani shirika hilo lisilaumiwe.

Akizungumzia kauli hiyo, Ngeleja alisema ni sahihi kwa kuwa ni Mtendaji wa shirika la umma.

Kwa mujibu wa Ngeleja, mitambo ya Dowans ilikuwa inunuliwe kwa dola za Marekani milioni 59.157 (sh. bilioni 70), gharama ambayo wengi walisema iko juu kuliko mtambo mpya.

Kuhusu madai kuwa TANESCO haikupata idhini ya bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo ilipowasilisha ombi la kununua mitambo hiyo, Ngeleja alisema si kweli.

Alisema wizara ina muhtasari wa kikao cha bodi kilichoruhusu kuomba, isipokuwa ilitoa tahadhari kuwa ifanye kwanza tathmini ya kina kabla ya kununua.

Hata hivyo, Ngeleja alisema hoja ya kununua mitambo iliyotumika si ngeni, kwa kuwa ilishawahi kuungwa mkono mara kadhaa na iliyokuwa Kamati ya Bunge ya Biashara na Uwekezaji mwaka 2007.

Alisema kamati hiyo ilifanya hivyo iliposhauri serikali kuharakisha mchakato wa kununua mitambo ya IPTL na kwamba, wabunge wengi walikubali pamoja na kwamba Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 ilikuwepo.

Alisema nia ya serikali kupitia TANESCO kutaka kununua mitambo ya Dowans ilikuwa kuikoa nchi na hatari ya upungufu wa umeme, kwa kuwa mahitaji ya nishati hiyo yanaongezeka kwa wastani wa asilimia 10 hadi 15 katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012.

Alitaja sababu nyingine kuwa, kuisha kwa mikataba ya mitambo ya kukodi ya Alstom Power Rentals (megawati 40) na Aggreko (megawati 40); kuchelewa kuanza kwa mradi wa umeme wa Kinyerezi wa megawati 240, ambao utakamilika mwaka 2011.

Nyingine ni kuvunjwa kwa mkataba wa kukodi mitambo ya Dowans wa megawati 105, uliokuwa uishe Julai 28, mwaka jana.

Ngeleja alisema upungufu wa nishati hiyo kwa sasa ni megawati 150, ambapo serikali kwa kushirikiana na wahisani ipo katika hatua ya mwisho ya kununua mitambo yenye uwezo huo na kwamba, taarifa rasmi ya lini itawasili itatolewa baadaye.

Mikakati mingine ni kupunguza matumizi ya umeme majumbani na viwandani kwa asilimia 20 (megawati 120) kwa kuleta vifaa vipya visivyotumia umeme mkubwa na kutenga asilimia 15 ya mapato ya TANESCO kwa mwezi kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme nchi nzima.

Wiki iliyopita Dk. Rashidi alitangaza TANESCO kujitoa katika nia ya kununua mitambo ya Dowans.

Mpita Njia
03-16-2009, 01:01 PM
Tunafungaje mjadala wa Dowans wakati bado tuna kesi nao?

edo
03-16-2009, 03:42 PM
Hiki ni kichekesho!! Bado kuna mambo mengi yenye kuhitaji maelezo na kwa sababu watawala wetu ni wahubiri wazuri wa utawala bora na uwajibikaji, ni vyema wangetupatia majibu kabla ya kuufunga mjadala huu kirahisi namna hii kana kwamba hauna maslahi yoyote kwa watanzania.