PDA

View Full Version : Makuwadi wa Ufisadi CCM wameguke!



mwanakijiji
04-08-2009, 05:27 PM
Na. M. M. Mwanakijiji

Kuna kundi la wanasiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi ambalo linatakiwa limeguke kutoka chama hicho mapema iwezekanavyo. Kundi hilo ni la wale watu ambao wamefilisika kisiasa ambao wamebakia kuwa watetezi wa mambo yalivyo (status quo) na ambao hawako tayari kuona mabadiliko ya kweli yanakuja ndani ya Chama cha Mapinduzi. Kundi hili kwa hakika ni la wanasiasa ambao majina yao yameanza kusahauliwa, nafasi yao katika historia kufutika taratibu na ambao kwa hakika muda wao wa kuangaza umeisha na sasa wamebakia kuwa vivuli vyao vya zamani. Kundi hili la wanasiasa wanajaribu kusimama tena na kupaza sauti zao ili nao wasikike! Kundi hili ni la wale wasiopenda mabadiliko ndani ya CCM!

Kundi hili linaongozwa na imani isiyotetereka ya Ibara ya 15:1 ya Katiba ya CCM. Kwa wale wasiojua ibara hiyo ni kuwa inaweka majukumu ya mwana CCM. Ibara hiyo inasema hivi ? 15. Kila Mwanachama atakuwa na wajibu ufuatao:- (1) Kujua kwamba Chama Cha Mapinduzi ndicho chenye nguvu, uwezo na kwamba nguvu hizo zinatokana na umoja wa Wanachama, fikira sahihi za CCM na kukubalika kwake na umma. Kwa hiyo ulinda na kuendeleza mambo hayo ni Wajibu wa kwanza wa kila Mwanachama.? Hivyo hakuna utata kabisa kuwa ni nini jukumu la kwanza la mwana CCM. Kwa sababu ukisoma jukumu la pili (haiwezekani kuwa la kwanza baada ya kusoma kifungu hicho cha kwanza) utaona kuwa jukumu la pili ni ?Kutumikia nchi yake na watu wake wote kwa kutekeleza wajibu wake bila hofu, chuki wala upendeleo wa nafsi yake, rafiki au jamaa.?

Hii ina maana ya kwamba, mwana CCM akiweka nchi yake kwanza na kuitumikia na watu wake wote bila hofu, chuki wala upendeleo wa nafsi yake, rafiki au jamaa mtu huyo atakuwa anafanya mambo kinyume na Katiba ya CCM!

Kwa maneno mengine ukimuona mwana CCM anasimama kutetea maslahi ya Taifa, kutetea haki za wananchi na anapambana dhidi ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka n.k akiongozwa na uzalendo kwa Taifa lake basi tarajia mtu huyo kuonekana adui ndani ya CCM. Kwanini? Angalia Ibara ya 15:1

Hivyo, leo hii kuna mgongano ndani ya CCM ambao msingi wake kwa kweli ni mgongano wa maslahi ya chama na yale ya Taifa. Maslahi ya Chama ni kuendelea kukaa madarakani kwa kushinda chaguzi mbalimbali. Maslahi hayo ya kichama wakati mwingine yanagongana na maslahi ya Taifa na pale inapotokea mgongano huo, basi makundi karibu matatu huwa yanajitokeza.

Kundi la watetezi wa Chama;
Hili ni kundi lenye nguvu mno ndani ya CCM ambalo bado kwa mbali linajiona kama Kamati Kuu ya Nchi ya Kikomunisti ambapo wao nidhamu ya chama ni muhimu sana na ambao haliko tayari kuona chama kinachafuliwa, kinabezwa au kwa namna yoyote ile kinafanywa kuwa duni. Kundi hili kila linaposimama kuzungumza kwao maneno yao yanaanza na ?CCM? na yanaishia na ?CCM?. Kwa wajumbe wa kundi hili CCM haiwezi kufanya makosa; CCM kwao ni safi, CCM haina uchafu wowote (wenyewe wanasema uchafu ni wa mtu siyo chama). Kundi hili kwa kweli haliwezi kabisa kuvumilia mtu yeyote kukinyoshea kidole chama na hasa kama mtu huyo ni mwanachama pia.

Kundi hili halichelewi kuja na mikwara kwa mwanachama yeyote ambaye anaonekana ni mchokozi na mkosoaji. Kwa mtu kama huyo kundi hili halichelewi kujitokeza na kusema watu wa aina hiyo ?wameguke?!

Kundi hili halina maslahi yoyote ya Taifa moyoni bali kujihakikishia uwepo wao kwenye madaraka au uzao wao kuendelea kupata nafasi ya kubakia madarakani. Kwao hawa CCM kuondoka madarakani itakuwa ni mwisho wa nafasi yao ya ulaji na usalama wa mali zao. Kundi hili maslahi yake yamefungamana moja kwa moja na uwepo wa CCM madarakani. Bila CCM madarakani kundi hili halina nafasi baadaye (without CCM in power, this group has no future).

Kundi la Wana CCM ? Mabadiliko
Kundi hili ni jipya na limeanza hasa kujitokeza kwa nguvu zake baada ya sakata la Buzwagi ambapo tuliweza kuona kwa mara ya kwanza uwepo wao na sauti yao kwa iliweza kusikika kwa nguvu zaidi wakati wa mjadala wa Richmond. Kwenye sakata la Buzwagi kundi hili lilijikuta linalazimika kushiriki katika kitendo cha kumfungia Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. Zitto Kabwe katika mazingira ambayo mtu yeyote mwenye akili timamu angeweza kuyaona kuwa ni ya kibabe na yenye mrengo wa kutetea chama (kwa mujibu wa ibara ya 15:1) kuliko maslahi ya Taifa.

Mwitikio wa wananchi baada ya kufungiwa Zitto ndiyo ulionesha mpasuko wa wazi uliomo ndani ya CCM. Kwa mara ya kwanza CCM walijua hawatawali tena fikra za wananchi na ya kuwa Watanzania wanajua uonevu wakiuona, na lile la Zitto lilikuwa ni uonevu wa wazi. Bahati mbaya sana ni wabunge wachache na viongozi wachache waliotambua kosa lile na kuanza kujirudi. Wale wa kundi la kwanza waliendelea kutamba na kuimba kuwa ?hatuzomewi, tunashangiliwa!?.

Lilipokuja suala la Richmond ndipo kwa mara nyingine tena tukaona wazi uwepo wa makundi hayo na ndani yake tukaona kundi jingine lililojificha ambalo maslahi yake si chama wala si taifa!

Kundi la Maslahi
Hili ni kundi la wale ambao utii wao na mapenzi yao ya dhati yako kwenye mifuko yao na matumbo yao. Hawa wanatumia nafasi zao ili kujineemesha wao na familia zao. Kundi hili ni la wanasiasa ambao wanavaa nguo za kijani na nyeusi za CCM lakini ndani yao wako kinyume na kila kitu ambacho CCM inasimamia. Hata hivyo hawawezi kuonesha hivyo na badala yake wanajitokeza kama wafadhili wakubwa wa CCM. Kundi hili lina wafanyabiashara wanasiasa na wanasiasa wafanyabiashara na wale wanaopenda kuwa na sehemu zote mbili.

Kundi hili limejikita katika sera za ubepari na wao neno ujamaa ni kinyaa kwao. Hawa wana nguvu moja kubwa nayo ni pesa. Wana uwezo wa kushawishi mtu yeyote wa makundi yale mawili ya mwanzo na wakiamua kutishia maslahi ya mtu huyo (aidha bungeni au vinginevyo) kundi hilo haliwezi kusita kufanya hivyo. Ni kundi ambalo kwa watu wengine tunaweza kusema ndilo lililoiteka nchi!

Kundi hili haliwezi kukemea ufisadi! Liko kimya wakati fedha zetu zimechotwa Benki kuu, liko kimya wakati vijana wetu wametelekezwa kule Ukraine, liko kimya yanapokuja maslahi ya taifa. Watu wa kundi hili hawawezi kukemea mafisadi na hawawezi kuitisha kwa uchunguzi huru wa Meremeta, Mwananchi, Deep Green, Tangold au jambo jingine lolote. Sababu kubwa ni kuwa ni wao wenyewe waliojikita katika sehemu hizo zote na wanajua kuwa siku akitokea kiongozi wa kweli, shujaa asiyeyumba na jasiri asiyebabaishwa utawala wao wa njozi za kifisadi utakuwa umefikia kikomo!

Hawa ndiyo watu wa hatari sana katika demokrasia yetu, na katika mwelekeo wa taifa letu wametushika kama mali iliyowekwa rehani! Wanatembea wakicheka cheka huku wanajifanya wako kimya hawasemi lolote; kumbe wao ndiyo Tanzania na Tanzania ndio wao. Fikra zao ni za ubepari wa zamani ambao msingi wake ni unyonyaji na ugandamizaji.

Kundi hili la tatu ndilo limeshikilia kundi kubwa kabisa ambalo kimsingi naweza kuliita ?bendera fuata upepo?. Watu wa kundi hilo kubwa ambao mwelekeo wao ni wa kundi la tatu wao ni watu ambao wanauhakika kuwa maslahi yao na ya watoto wao yamefungamana na maslahi ya kundi hilo la tatu. Hivyo, wanachama wa kundi hilo kubwa, ndiyo watetezi wakubwa wa mafisadi nchini!

Hawa hawaoni ubaya wowote uliotokea Benki Kuu! Hawa utawasikia wakitetea na kusema ?mafisadi wote wamefikishwa mahakamani? na wakati mwingine utawasikia wakilia kuwa ?fulani alionewa?.

Makundi yote matatu yana wapambe wao aidha serikalini, kwenye vyombo vya habari, kwenye jumuiya mbalimbali na hata kwenye taasisi za dini. Hivyo utaona kuwa mgongano wa makundi haya matatu unachochewa mara zote na maslahi wanayowakilisha. Ukisoma magazeti yanayotoka kila siku utaona mwelekeo wa makundi hayo.

Utaona magazeti yenye vichwa vya habari vya kuwakandia watu wa kundi moja, na ukinunua gazeti jingine utaona watu wa kundi jingine na wenyewe wakirushiwa madongo. Tatizo kubwa ambalo hata Mzee Malecela aliliona ni kuwa ni wananchi ndiyo wanawafadhili watu wa makundi haya yote. Kama mtu ana akili timamu atanunua magazeti ya kundi lile analojiona yuko upande wao! Mtu afanye hivyo ndiye huitwa mwenye hekima!

Nani ameguke sasa?
Sasa tukirudi kwenye mazungumzo ya mzee Malecela kama kuna kitu ambacho naona kilimkera mzee wetu ni kile alichokielezea kama tishio la watu fulani fulani kutoka CCM. Jambo hilo lilimkera sana mzee kiasi kwamba alirudia mara kadhaa kuwataka wanaotaka kutoka CCM basi watoke.

Kwa maneno yake; ?kama kuna watu wanataka kujimega kutoka CCM na wajimegew sasa hivi tujue moja lakini hii ya kuendelea kutishia tu nyinyi mnaandika CCM itameguka, CCM itameguka?Wasifikiri kwamba (CCM) inaweza kutishwa na kikundi cha watu wachache au hata wawe watu wangapi wameguke, na tutawaacha kwenye mataa?. Swali kubwa msomaji inabidi ujiulize ni kundi gani ambalo unafikiri mzee Malecela alikuwa anamaanisha kuwa limeguke?

Haiwezekani kuwa ni kundi la kwanza ambalo naamini yeye yumo. Kundi hili CCM ndiyo mama yao mzazi na hawako tayari kuona mtu yeyote anachezea au kutishia uhai wake. Hawa ni wale ambao naweza kuwaita vigogo wa chama ambao wametoka na CCM mbali na mioyoni mwao wanajua kabisa bila ya CCM wasingekuwa walipofikia hapo. Hivyo hawa kumeguka haiwezekani kwani hawawezi hata kutishia kumeguka! Kwenye njozi zao wakiota wamemeguka itabidi waende kutoa sadaka na kufanya maungamo!

Nyerere mwenyewe asingeweza kuwa kwenye kundi hilo kwani pamoja na uasisi wake wote wa CCM na Taifa aliweza kusema pasipo kigugumizi ?CCM siyo mama yangu?. Leo hii hakuna kwenye kundi hilo anayewa kufikiria kauli ya namna hiyo acha tu kuisema wazi!

Haiwezekani kuwa ni kundi la tatu ambalo maslahi yake yamefungamana na utawala wa CCM. Kundi hilo la tatu likimeguka CCM itapoteza chanzo kikubwa cha mapato yake. Kwani ni kundi hilo lililoshiriki katika kuifadhili CCM ?by any means necessary? ikiwemo mpango wa kijambazi wa Kagoda na wadogo zake. Kundi hili likimeguka CCM imekwisha. Haliwezi kumeguka kwani na lenyewe likimeguka kutoka CCM litakuwa limekwisha kwani nguvu yake pia inatokana na uhodhi wake wa madaraka.

Kundi ambalo linaweza kumeguka ni lile la wale wanaoonekana ni wasumbufu na wenye kutafuta sifa wa kundi la pili. Hawa ni kama mwiba na kama watu ambao wako kwenye boti na hawaachi kuyumba yumba. Hawa wanaonekana kama yule mtu wa kwenye methali aliyekuwa akikata tawi la mti ambalo yeye mwenyewe amekalia.

Hili ndilo kundi ambalo linatishia maslahi ya makundi yote mawili mengine. Kwa wale wa kundi la kwanza kinachotishiwa ni legacy (yaani historia itawakumbuka vipi). Wengi wa wale walio kwenye kundi la kwanza katika zama zao walikuwa ni watu wenye nguvu na wenye sauti lakini sasa hivi wamebakia kama picha ukutani hawana sauti tena isipokuwa ujiko tu wa nafasi walizowahi kushikilia. Sasa kuna kundi limekuja ambalo linaleta mwamko mpya ndani ya Chama na kwenye taifa, lina sauti na lenye kuthubutu; sasa hawa wafanye nini? Ndiyo maana siku za karibuni tunayasikia majina ya wanasiasa ambao tulishawasahau na wenyewe wakijaribu kurudi kwenye kurasa za magazeti yetu kwani maslahi yao yanatishiwa!

Fikiria kina Ndejembi na Barongo hawajasikika miaka leo wanaibuka kuwa watetezi wa Urais wa Kikwete. Walikuwa kimya zilipoibwa fedha zetu Benki Kuu, wamekuwa kimya kwenye suala la kifisadi la Dowans (ndiyo la kifisadi!) na wamekuwa kimya kwenye masuala mengine muhimu ya Taifa. Lakini linapokuja hili la Mwenyekiti wao kunyimwa nafasi nyingine ya kuwa Rais wamekurupuka toka katika usingizi wao wa muda mrefu na kuanza kupiga kelele! Maslahi yao yanatishiwa!

Hivyo, kundi hili la pili ndilo ambalo wangependa limeguke toka CCM; wangependa watu wake wanyamaze na kuacha malumbano! Kundi hili kwa hakika limeleta mwamko mpya wa chama ndani ya CCM na fikra mpya za mabadiliko. Ni kundi ambalo kwa kila kipimo linaweza kulazimishwa kujimega au kutokana na nguvu ya makundi yale mengine mawili likajikuta ?limemegwa? kama walivyomegwa kina Seif na kina Mloo enzi zile!

Kundi hili likiondoka CCM, basi kutakuwa na amani na kwa mara nyingine tena zitaanza propaganda za yale yaliyomkuta Mrema na wenzake waliojitoa CCM kuingia upinzani!

Hata hivyo, naamini kabisa kuwa endapo kundi hili litajitoa huo ndio utakuwa mwisho wa CCM kama tunavyoijua. Akitoka mtu mmoja inawezai isiwe tatizo lakini likitoka kundi la watu kwa wakati mmoja na watu hao ni wale ambao wamejichotea sifa kwa utetezi wao wa nchi na msimamo wao mkali dhidi ya ufisadi basi kundi kubwa la Watanzania litaungana nao na kusababisha kumeguka kwa CCM!

Litakuwa pigo kubwa kwa Chama kilichoasisiwa na Mwalimu lakini yawezekana ndiyo dawa pekee ya kukiponya chama hicho. Kwani, kwa kila kipimo CCM hii siyo ile ya Mwalimu kwani ilishaacha misingi yake siku nyingi zilizopita. CCM hii siyo ya kijamaa (hakuna kada wake hata mmoja anayeweza kusema ni ya kijamaa); CCM hii haina Azimio la Arusha; CCM haina sera za kujitegemea; CCM haina mwelekeo wa ujenzi wa taifa la watu walio huru na sawa; n.k Hivyo kuondoka kwa kundi hilo yawezekana kutairudisha CCM kwenye njia iliyoiacha.

Wakumeguka siyo hao ni hawa!
Hata hivyo ukiniuliza mimi nitakuambia pasipo utata ni kuwa wa kumeguka ni watu wa kundi la tatu. Tena hawa siyo wa kuachwa kumeguka bali wa kumeguliwa kwa nguvu ya Chama. Kundi hili la tatu kama nilivyosema hapo juu ndilo kundi linalohatarisha maisha ya chama na ni hatari kwa taifa. Kundi hili ndilo ambalo watu kama kina mzee Malecela walitakiwa kulipiga vita ndani ya Chama na kulitaka limeguke!

Hivyo, kwa wale ambao wamelelewa ndani ya CCM na ambao wanajua historia ya kimapinduzi ya chama hicho wale ambeo wamejifunza itikadi ya CCM na kula kiapo cha kutokuwa mnafiki au kwa namna yoyote ile kuvumilia rushwa. Kwa wale ambao bado wanahusudu mfumo ule wa kijamaa na kujitegemea, ujumbe wangu kwa hawa makuwadi wa ufisadi waliojibanza ndani ya CCM ni kuwa saa yenu imefika, na wakati wenu umewadia! MEGUKENI! Kwani, hamuwezi kushiriki katika urithi wa Chama cha Mapinduzi, isipokuwa kama mnataka tuwaachie chama mkiite CCM-U!! Yaani, Chama cha Makuwadi wa Ufisadi!

Niandikie: Mwanakijiji@mwanakijiji.com