PDA

View Full Version : News Alert: Uingereza yabadili utoaji visa!



mwanakijiji
11-12-2008, 04:55 PM
Nimepokea taarifa ifuatayo toka Ubalozi wa Uingereza kama tangazo kwa vyombo vya habari:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

12 Novemba 2008

Mabadiliko katika huduma ya utoaji viza za Uingereza

Ubalozi wa Uingereza unatoa taarifa mapema juu ya mabadiliko katika huduma yetu ya utoaji viza.

Kama ilivyokuwa hapo awali, waombaji wanapaswa kuanza kushughulikia maombi yao ya viza angalau majuma sita kabla ya siku wanayopanga kusafiri.

Lakini Ubalozi wa Uingereza hautakuwa tena na uwezo wa kuwezesha upatikanaji wa viza, ikiwa mwombaji atatoa taarifa ya muda mfupi.

Kuanzia Desemba mosi mwaka huu, maombi ya viza yatashughulikiwa kama ifuatavyo: -

Hatua ya Kwanza: Tuma maombi yako kwa mtandao na omba kupatiwa miadi (appointment)

Waombaji wote wanashauriwa kutuma maombi ya awali kwa mtandao kupitia: www.visa4uk.fco.gov.uk.

Kama sehemu ya utaratibu huu wa kutuma maombi ya viza kwa mtandao, mwombaji atachagua tarehe na muda wa miadi (appointment) yake Ubalozi wa Uingereza, Dar es Salaam. Kwa kawaida miadi itapangwa ndani ya majuma matatu baada ya mwombaji kutuma maombi yake kwa mtandao. Na waombaji watapata urahisi wa kuchagua muda wa miadi ambao utawafaa kwa kuwa Sehemu ya Viza itakuwa wazi kwa mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa awali: kuanzia saa 1:45 asubuhi mpaka saa 8:00 mchana (Jumatatu mpaka Alhamisi), na saa 1:45 asubuhi mpaka 5:30 asubuhi (Ijumaa).

Waombaji ambao hawataweza kutuma maombi ya awali kwa mtandao wanaweza, badala yake, kuja ubalozini bila ya kuwa na miadi. Lakini waombaji wa aina hii hawatapewa umuhimu wa kwanza ikilinganishwa na wale waliotuma maombi yao ya awali kwa mtandao. Kwa hivyo waombaji wanaweza kutakiwa kurudi ubalozini siku nyingine mbeleni.


Hatua ya Pili: Miadi Ubalozi wa Uingereza

Waombaji wote lazima wafike Ubalozi wa Uingereza Dar es Salaam katika muda wa miadi uliopangwa.

Wakati wa miadi, mwombaji:

? atawasilisha pasipoti yake, nakala halisi ya maombi yake, na nyaraka zinazohusika (tazama www.ukvisas.gov.uk ili kufahamu nyaraka zinazohitajika);
? atachukuliwa alama za vidole; na
? atalipa ada ambayo haitarudishwa (non-refundable).

Ubalozi utamjulisha mwombaji ni siku gani atarudi tena kuchukua pasipoti yake.

Hatua ya Tatu: Tathmini ya Maombi

Pasipoti, maombi na nyaraka zote zinazohusika vitapelekwa Ubalozi wa Uingereza mjini Nairobi ambapo vitafanyiwa tathmini, na hapo pia viza kwa waombaji waliofanikiwa zitatolewa.

Baadaye pasipoti na nyaraka za waombaji zitarejeshwa Ubalozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam.

Kwa kawaida mchakato huu utakuwa umekamilika katika kipindi cha majuma matatu. Kama kutakuwa na ucheleweshaji, Ubalozi utawasiliana na mwombaji na kumpa tarehe nyingine ya kuchukua pasipoti yake.

Hatua ya Nne: Kuchukua Pasipoti

Mwombaji anakuja tena kuchukua pasipoti yake Ubalozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam katika tarehe iliyopangwa.

Mabadiliko haya yanafanya kuwe na umuhimu mkubwa sana kwa mtu kuomba viza mapema kabisa kabla ya safari.

Tumeshapendekeza kwa waombaji wote kwamba ni vema waanze mchakato wa maombi kwa mtandano angalau majuma sita kabla ya muda wa safari zao. Tunaendelea kupendekeza jambo hili. Wale ambao hawatupi majuma sita, kuna uwezekano wakajikuta maombi yao hayashughulikiwi katika muda wanaotarajia.

Maombi ya viza yanaweza kutumwa hata miezi mitatu kabla ya safari yako. Na maalumu kwa watu wanaoomba viza za wanafunzi na za kuhamia Uingereza, tunapendekeza kama ikiwezekana maombi yatumwe miezi mitatu kabla ya muda wa safari kuwadia.

Tafadhali zingatia kwamba baada ya Desemba mosi 2008 Ubalozi wa Uingereza mjini Dar es Salaam hautaweza kushughulikia maombi ya viza kwa kupewa taarifa ya muda mfupi.

Ubalozi unapenda kuwahakikisha wasafiri kwamba Serikali ya Uingereza bado ina nia thabiti ya kuboresha huduma zake kwa wananchi wa Watanzania na watu wengine wanaotaka kwenda Uingereza.
__________________________________________________ ______________

Dondoo kwa Wahariri:

1. Mabadiliko haya ni sehemu ya muundo mpya wa shughuli za viza za Uingereza duniani kote, unaojulikana kama "Hub & Spoke visa processing". Hii itapunguza kwa asilimia 50 idadi ya balozi zitakazotoa viza duniani kote, kufikia kiasi cha balozi 50. Kusini mwa Afrika, kwa mfano, maombi ya viza toka Namibia, Botswana, Mozambique, Lesotho, Swaziland, Malawi, Swaziland, Malawi na Zimbabwe kwa sasa yanashughulikiwa Pretoria. Nairobi tayari imeanza kushughulikia maombi toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Kenya. Na Ulaya, Marekani Kaskazini na Marekani Kusini shughuli za viza zimeondolewa kufanyika katika zaidi ya balozi 50 za Uingereza na sasa zinashughulikiwa na ofisi za kanda.

2. Ada za viza za Uingereza duniani kote hupangwa kwa kuangalia gharama halisi za mlolongo mzima wa ushughulikiaji/utengenezaji viza. Kuunganisha shughuli za viza kutasaidia kupunguza gharama za ushughulikiaji viza, kitu ambacho kwa upande mwingine kitasaidia viwango vya ada za viza vibaki chini.

3. Hapatakuwa na mabadiliko katika aina mbalimbali za huduma za viza zinazotolewa Tanzania. Tutaendelea kutoa huduma za viza zenye ubora wa kiwango cha juu.

4. Huduma ya viza ya mtandao kwa sasa ni njia ya haraka na inayojulikana zaidi kwa wateja wetu katika kupanga miadi ya kuja ubalozini kwa ajili ya viza. Zaidi ya asilimia 80 ya waombaji wote wa Tanzania kwa sasa wanatumia huduma ya mtandao kutuma maombi yao ya viza.

5. Wale wanaoomba viza za kuishi Uingereza kwa miezi 12 au zaidi bado watahitajika kufanya kipimo cha TB katika ofisi ya International Organisation of Migration (IOM) jijini Dar es Salaam, kabla ya kuja kwenye miadi ubalozini. Kama vipimo vya DNA vitahitajika, navyo pia vitaendelea kufanyika nchini Tanzania.

6. Kama mwombaji atahitajika kufanyiwa usaili, mipango itafanywa ili usaili huo ufanyike katika Ubalozi wa Uingereza hapa Dar es Salaam au kwa simu. Usaili utapangwa kwa haraka kadri iwezekanavyo, lakini sio zaidi ya siku 10 za kazi (10 working days) tangu miadi ya kwanza ilipofanyika. Waombaji hawatalazimika kwenda kufanyiwa usaili Nairobi.

7. Hata hivyo, kwa sasa usaili kwa waombaji huwa unafanyika kwa nadra sana. Maombi ya viza hutolewa maamuzi kutokana na maelezo yaliyomo katika fomu ya maombi, nyaraka zinazohusika, na historia yoyote ya uhamiaji Uingereza ya mwombaji ya huko nyuma. Ni muhimu basi kwa waombaji kuleta maelezo ya kutosha kutia nguvu maombi yao. Hii ni pamoja, kwa mfano, kutoa ushahidi kuonesha fedha alizonazo mwombaji kumwezesha kulipia gharama za usafiri na makazi yake nchini Uingereza.

8. Mwombaji atakayetoa nyaraka feki/za kughushi au taarifa za uongo atanyimwa viza, na anaweza kufungiwa asipate viza kwa miaka 10.

9. Watu wanaosafiri mara kwa mara kwenda Uingereza wanaweza kustahili kupewa viza za miaka mitano au kumi. Hii itawapunguzia usumbufu wa kuomba upya viza kila mara. Ada za viza za muda mrefu nazo pia ni nafuu kuliko kuomba mara kwa mara zile za miezi 6. Vile vile, mwenye viza za aina hii huonekana ni mteja anayethaminiwa na kuaminiwa na Uingereza.

10. Ada za viza za Uingereza kwa sasa ni:

Viza ya kutembelea inayodumu kwa miezi sita (unaweza kuingilia zaidi ya mara moja) - Tsh 156,000
Viza za kutembelea zinazodumu kwa muda mrefu zaidi: yaani mwaka mmoja, miaka miwili, mitano na miaka kumi (unaweza kuingilia zaidi ya mara moja); viza za kufanyia kazi wakati wa likizo; ruhusa/hati ya kufanyia kazi; viza maalum kwa ajili ya wafanyakazi wageni wenye vipaji maalumu, viza maalum kwa ajili ya raia wa Uingereza waliobadilisha uraia na kuwa raia wa nchi nyingine (certificate of entitlement) - TSh 492,000
Viza kwa ajili ya matibabu - TSh 156,000
Viza za wanafunzi - TSh 238,000
Viza za kupitia Uingereza (Hazina kibali cha kukuruhusu kutoka nje ya uwanja wa ndege) pamoja na viza za kupita kwa wanaokuja kutembea - TSh 108,000
Viza za makazi pamoja na ndoa - TSh 1,236,000

11. Kila mwaka, Watanzania kati ya 8,000 na 9,000 huomba viza za Uingereza.

12. Maelezo ya ziada yanaweza kupatikana kwenye tovuti yetu:www.ukintanzania.fco.gov.uk.
__________________________________________________ ______________________

Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:

John Bradshaw
Afisa Habari
Ubalozi wa Uingereza, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2110101
Simu ya mkononi: +255 (0)754 764276
Faksi: +255 22 2110102
Barua pepe: john.bradshaw@fco.gov.uk
Tovuti: www.ukintanzania.fco.gov.uk