mwanakijiji
05-08-2009, 08:24 PM
Jamani kuna habari ambazo zinatia shaka kwa wana CCM kuwa kuna uwezekano wakashindwa Busanda.. tatizo ni nini? Maana kina Makamba wanataka waachiwe kiti hicho kwani ni "chao"..
CCM yahofia kilio Busanda
Thursday, 07 May 2009 16:40
Na Faida Muyomba, Geita
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Yusuf Makamba amewataka wanachama wa chama hicho kuwa na mshikamano akihofia yaliyotokea Tarime kujirudia jimboni Busanda, Mwanza huku akieleza kuwa alipata aibu kubwa baada ya kushindwa katika uchaguzi huo.
Bw. Makamba aliwaambia wanachama hao kuwa suala la kushindwa ni bora ukalisikia tu kutoka kwa wengine na si wewe mwenyewe kwani ni tukio linalofedhehesha mno na kwamba hata Busanda hapati usingizi kwa kuwa linaweza kujirudia tena.
Alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na wanachama hao katika kile
kinachoonesha ni kuwekana sawa kutokana na ukweli kuwa kuna mpasuko mkubwa
ndani ya chama hicho wilayani Geita, jambo linaloweza kuwanyima ushindi katika Jimbo la Busanda.
"Sasa kama wanalifahamu hilo... mbona hawajalipatia ufumbuzi wa kudumu hii
inatokana na kutosikiliza hoja na kero za wanachama wa kawaida. Badala ya kuarifiwa ukweli wamekuwa wanapotoshwa kwa kuambiwa kuwa wagombea ndio chanzo, madai ambayo ni uongo," alidai mmoja wa wanachama aliyehudhuria kikao hicho nyeti cha CCM.
Dalili za mpasuko huo zimeaanza tayari kujionesha hasa katika siku ya uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika jana Kata ya Kaseme ambapo watu wachache walihudhuria huku msafara wa magari yaliyokuwa na bendera za CCM ulikuwa ukizomewa njiani kama ishara ya kutokubalika kwa mgombea wao.
Uzinduzi wa kampeni za CCM umekuja siku tano baada ya vyama vya upinzani vya CHADEMA na CUF kufanya uzinduzi Mei 2 katika vijiji tofauti vya Katoro na Nyarugusu, mikutano iliyohudhuriwa na mamia ya wananchi licha ya kuvurugwa na mvua.
CUF katika kumnadi mgombea wao Bw. Oscar Primus, ilizindua kampeni zake kupitia kwa Katibu Mkuu wao Bw. Seif Shariff Hamad kwenye kijiji cha Katoro huku CHADEMA wao wakimnadi mgombea wao Mhandisi Finias Magesa katika uzinduzi kwenye Kijiji cha Nyarugusu.
lmllube
05-09-2009, 01:29 PM
Naamini wananchi wameanza kuamka. Nina hakika pia ni suala la muda pale watu wataacha kuchagua kwa kufuata hotuba zinazotolewa majukwaani. Tunataka matendo na si hotuba. Tusichoke ipo siku umma wote utaamka na kuchagua viongozi bora na si bora viongozi.
mwanakijiji
05-09-2009, 10:17 PM
Na Frederick Katulanda, Busanda
WAKATI joto la uchaguzi mdogo wa Jimbo la Busanda likizidi kuongezeka, vyama vya siasa vinavyowania kiti hicho vimebadili mbinu za kampeni, ikiwa ni pamoja na kuwaita wabunge na viongozi wake wa kitaifa ili kujiimarisha.
Kwa upande wa CCM mbali ya kumtumia aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, John Malecela wamelazimika kumwondoa mjumbe wake wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Anthony Diallo ili kuliingiza kundi la mmoja wa wagombea aliyeshindwa kura za maoni kwa nia ya kuziba mpasuko unaokisumbua chama hicho.
Habari za ndani ya CCM zimeeleza kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kampeni zao kupata upinzani mkali ikiwa ni pamoja na kuzomewa na watu wachache kujitokeza kwenye mikutano yao; wameamua kuunganisha makundi yanayohasimiana kwa kumuita aliyeibuka mshindi wa pili, Doanard Max ili asaidie kumnadi mgombea wao.
Diallo ametajwa kuwa hasimu mkubwa wa Max kutokana na kudaiwa kumsaidia mmoja wa wagombea kwa nia ya kumuengua (Max), jambo ambalo liligawa kura zake na kumfanya mgombea wa sasa kuibuka wa kwanza. Max alishika nafasi ya pili huku Sostenes Kulwa anayedaiwa kuungwa mkono na Diallo kuambulia nafasi ya tatu.
Sambamba na hatua hiyo, pia CCM imeamua kuwaita wabunge wake wote wa Mkoa wa Mwanza kwenda jimboni humo kusaidia kampeni za uchaguzi huo na wamepangiwa kata mbalimbali za jimbo hilo.
Mbali na wabunge hao pia CCM katika kuhakikisha inalikomboa jimbo lililoachwa na aliyekuwa mbunge wake, Kabuzi Rwilomba, imepunguza mikutano ya kampeni ya nje na kuimarisha ile ya ndani ili kuepuka kuzomewa.
Lakini Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza, Rajabu Kundya amekanusha kuondolewa kwa Diallo ili kumuita Max, bali ameondoka Busanda baada ya kutumwa Dar es salaam kwa ‘masuala mengine ya kichama’.
Kundya alisema chama chake kimewapangia kazi wabunge wake katika jimbo hilo na kufafanua kuwa kila mbunge amepangiwa kata kusimamia kampeni hadi wakati wa upigaji kura.
Hayo yakijiri, kampeni za wapinzani wa chama hicho, hasa Chadema, zinazidi kunoga na mikutano yake kupata idadi kubwa ya watu, ikilinganishwa na chama hicho kikongwe.
Kama CCM, pia inaelekea mambo ni mazito kwa chama cha CUF, kwa kuwa nacho kimeweka mkakati wa kuongeza nguvu kwenye kampeni zake kwa kuwaita wabunge wake kwa ajili ya kusaidia kumnadi mgombe wake, Oscar Ndalawah.
Katibu wa timu ya uchaguzi ya CUF, Maole Kuchilungulo aliwataja wabunge kuwa ni Magreth Sakaya, Savelina Mwijage, Nuru Bafadhiri na Zaharani Mwanakwetu, wote wakiwa wa viti maalumu. Wengine ni Omari Ally Mzee, Salum Abdallah na Mohamed Mnyaa wote wa Pemba.
Kwa mujibu wa katibu huyo, lengo la kuwaita wabunge hao ni kusimamia kampeni katika kila kata kwa kile alichosema, baada ya kubaini kuwa CCM imeleta wabunge wake na kuwatawanya kila kata kufanya hujuma ambayo hata hivyo hakuitaja.
“Awali CCM walitudharau, walijua kuwa mshindani wao ni Chadema, lakini baada ya kufanya mikutano wamegundua kuwa mgombea wetu ana nguvu zaidi ya kwao na wa Chadema; wamepanga mkakati wa kutuhujumu na baada ya kubaini hilo tumeamua kuwaita wabunge wetu ili kuja kuchuana na wenzao wa CCM katika kila kata,” alieleza.
Chadema
Kwa upande wa Chadema wakiwa bado wanaendelea na kampeni za nje na zile za ndani walisema wameamua kumuita Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe kwa ajili ya kuongeza mashambulizi ya hoja na kufafanua kwa nini jimbo hilo limekuwa nyuma kimaendeleo.
Afisa Habari wa Chandema, David Kafulila alisema wao wamejipanga na kwamba kwa kuanza wameamua kumuita Kabwe ambaye atawasha moto katika kampeni hizo na baadaye kufuatiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
“Hatuna wasiwasi, tuna mikakati mingi lakini naweza kusema tu tumeamua kumuita Zitto Kabwe ambaye sasa atakuwa akiambatana na mgombea katika mikutano hiyo kumnadi kwa wapiga kura,” alieleza.
Green Guird’ walilia posho
Katika hatua nyingine, Vijana 24 wa kikundi cha ulinzi cha CCM (Green Guard), wamelalamikia kupunjwa posho zao na kulipwa Sh800 kwa siku badala ya Sh2,000 walizoahidiwa.
Barua yao ya Mei 5,mwaka huu iliyoandikwa na kusainiwa na David Azaria ilieleza kuwa posho ambayo walistaili kulipwa jumla ya vijana 30 ni Sh 5,000 kwa wageni na Sh2,000 kwa wenyeji wa wilaya hiyo lakini wote wamekuwa wakilipwa Sh800 huku wakielezwa kuwa pesa hakuna.
“Maisha katika mji wa Geita ni magumu, lakini unalipwa Sh800, wanasema chakula tutakula huko. Hivi sasa hali ya maisha yetu ni ngumu sana, lakini tumejaribu kulalamika kwa Katibu wa CCM wilaya amesema tupokee na wasiotaka waondoke,” alieleza mmoja wa vijana hao ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Akijibu malalamiko hayo, Kundya alisema tatizo hilo kwa sasa limemalizika baada ya yeye kufika na watu wote waliopo katika kampeni wanalipwa kulingana na taratibu za fedha za chama.
“Tatizo hilo halipo, kuanzia nilipowasili wanalipwa kwa staili na taratibu za chama,” alieleza Kundya.
Misimamizi wa uchaguzi
Vile vile CUF kimemtaka Msimamizi wa Uchaguzi kufuta zoezi la kuajiri makarani wa uchaguzi kutokana na kuchelewesha kutoa tangazo lake.
Afisa Uchaguzi wa CUF, Hussein Mmasi alisema kuwa tayari chama chake kimemlima barua msimamizi huyo kikieleza kuwa zoezi hilo limegubikwa na utata mkubwa, jambo ambalo linaonyesha wazi kuwa limefanywa makusudi kwa ajili ya kuisaidia CCM.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi jimboni hapa, Jackson Sombe amekiri kupokea malalamiko yao, lakini alikanusha kuwa matangazo hayo yalibandikwa siku ya mwisho.
“Nimepata malalamiko yao, lakini siwezi kubatilisha zoezi hilo, kwa sababu matangazo hayo hayakutolewa siku ya mwisho kama wanavyoeleza wao; yalibandikwa mapema kabisa, nimewaomba kwa kuwaandikia waje hapa ofisini kwangu kuhakiki majina ya makarani hao ili kama kuna mtu wana mashaka naye waseme aondolewe hawajaja,” alisema Sombe.
Katika hatua nyingine, msimamizi msaidizi wa uchaguzi imevionya vyama vyote vya siasa kujiepusha na uvunjifu wa amani katika mikutano yao ili kuepuka vurugu kama za Tarime.
Sombe alisema vyama vote vinapaswa kuzingatia muda wa kuanza mikutano na kumaliza na kufuata ratiba ya mikutano ili kuepuka migongano.
“Niwaombe tu viongozi wa vyama kuzingatia haya, muda wa kufanya mikutano na kumaliza na kuwazuia wanachama wao kuwazomea wengine na kurushiana maneno,” alieleza.
Uchaguzi wa Busanda unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Faustine Kabuzi Rwilomba.
Katika uchaguzi huo vyama ambavyo vimeweka wagombea ni CCM, Chadema, CUF na UDP lakini mchuano mkali umekuwa kati ya wagombea wawili wa CCM na Chadema.
CCM wasitafute mchawi, wachawi ni wao wenyewe ahadi yao ya 2005 maisha bora kwa kila Mtanzania wameshindwa kuitekeleza sasa hivi hata waiite kamati nzima hamna kitu, wananchi wa busanda wameamka. i wish ingekuwa hivo nchi nzima mwakani
mugerezi
05-11-2009, 10:46 AM
Hakuna kubweteka mambo bado mabichi kabisa. Huko Busanda iwe mfano ili 2010 kuwe hakuna kazi. Kama mlivyosikia jamaa anawaambia wanaCCM kuwa kushindwa siyo kuzuri JE HIYO NDIYO SERA? Hapa inatakiwa sera zinadiwe ili watu wachague jamaa analeta NGONJERA. INABIDI BAADA YA HUU UCHAGUZI OPERATION SANGARA IPITE TENA ILI WATU WASISAHAU MACHUNGU YANAYOLETWA NA CHAMA CHA MAFISADI.
flein
05-13-2009, 05:44 PM
Ukisikia mtu mzima analia??--ujue KUNA JAMBO. Hapo ndipo walipofika CCM tena kwa kutaka wakifanya ujinga wetu watanzania mtaji wao wa kufanya ufisadi. Lazima tuamke na kuwamwaga ipasavyo. Nitafurahi na kula chakula kizuri CCM wakimwagwa Busanda halafu mwakani tunawasubir kwenye majimbo yetu 5 mbeya na kilimanjaro na kanda ya ziwa kama kawa bila kusahau DSM. Inabidi hata mzee pinda akae vema maana kuna mguu wa chadema mpanda na lazima tuuhuishe upinzani dhidi ya Chama cha mafisadi.
USHINDI DAIMA
Powered by vBulletin™ Version 4.0.2 Copyright © 2012 vBulletin Solutions, Inc. All rights reserved.