mwanakijiji
08-23-2009, 11:34 PM
Habari ambazo zimekuwa zikitiririka kupitia vyanzo mbalimbali vimesema kuwa watoto 14 wamefariki kwa kuunguzwa na moto katika bweni walilokuwa wanalala usiku wa kuamkia leo huko Iringa. Bweni hilo liko katika shule ya Sekondari ya Idodi huko Iringa. Ajali hiyo ni nyingine ya aina yake kutokea nchini Tanzania na hadi hivi sasa chanzo hasa cha moto huo hakijajulikana na uchunguzi unaendelea. Hata hivyo, idadi ya wanafunzi waliokufa yaweza kuwa juu zaidi kutokana na baadhi ya wanafunzi kutojulikana wako wapi.
Ajali kama hii iliwahi pia kutokea huko Kilimanjaro katika shule ya sekondari ya Shauritanga ambapo watoto karibu 40 walikufa katika moto mkali ulioteketeza bweni hilo. Hadi leo ripoti ya uchunguzi wa moto ule haijawahi kuwekwa hadharani na serikali licha ya ahadi kuwa ingelifanya hivyo.
Ach-F
08-25-2009, 01:08 AM
Hivi kweli hakuna wakuwajibishwa hapa. Lakini vifo Tanzania vya walipa kodi ni sawa tu na jinsi ya kuua kuku mtaani hii ni kutokana na uongozi madhubuti wa CCM. Tumeyaona kila baada ya mika kadhaa. lake Victoria mamia waliangamia, Tabora NSSF waliuwa watoto (Corporate manslaughter), Zanzibar juzi juzi tu.
Kweli tuna Uongozi imara wa Chama Cha Mafisadi.
mwanakijiji
08-25-2009, 06:28 AM
Wanafunzi walioteketea kuzikwa kaburi moja leo
na Francis Godwin, Iringa (Tanzania Daima)
WAKATI mazishi ya miili ya wanafunzi 12 yanafanyika leo katika kaburi moja, serikali imetangaza kuifunga Shule ya Sekondari Idodi mkoani Iringa kwa siku 21 kuanzia juzi.
Uamuzi huo wa serikali ulitangazwa jana na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, ikiwa ni siku mbili baada ya janga la moto kutokea shuleni hapo na kuua wanafunzi 12, kuteketeza bweni na kusababisha hasara ya zaidi ya sh milioni 105.
Maghembe ambaye anatarajia kushiriki katika mazishi hayo shuleni hapo, alisema serikali bado inatafakari juu ya kukabiliana na majanga ya moto katika mabweni ya wanafunzi wa shule za sekondari nchini.
Alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda, anatarajiwa kuongoza mazishi ya wanafunzi hao.
Aidha, ofisi yake kupitia kitengo cha maafa imetoa rambirambi ya sh milioni 22.
Hata hivyo, wadau mbalimbali wameanza kutoa misaada yao kwa shule hiyo ikiwemo Kampuni ya Asas Iringa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ledian Mng’ong’o (CCM).
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mohamed Abdulaziz alimweleza mwandishi wa habari hizi jana kuwa tayari Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Iringa imeanza kupokea misaada mbalimbali kutoka kwa wadau hapa nchini.
Alisema misaada iliyopokelewa hadi juzi jioni ni magodoro 159, mablanketi 80, ndoo 50 na kanga doti 126 vyote vikiwa na thamani ya sh 4,032,000 kutoka Kampuni ya Asas.
Nayo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa, ilitoa mashuka 105 yenye thamani ya sh 420,000 na Mfuko wa Pesheni Taifa (PSPF) uliotoa mashuka 100 yenye thamani ya sh 400,000.
Wengine ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Mjini, Abed Kiponza aliyechangia magodoro 16, mablanketi 56, ndoo saba, vikombe vya kunywea maji vitano na galoni moja vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh 500,000.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Mng’ong’o alitoa kanga doti 100 zikiwa na thamani ya sh 320,000 ambapo jumla ya misaada yote iliyopokelewa ni sh 7,846,500.
Abdulaziz alisema misaada hiyo ilikabidhiwa juzi usiku kwa wanafunzi chini ya uangalizi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Raymond Mlasu, alisema wanafunzi wa kike wanaohitaji msaada baada ya vitu vyao kuteketea kwa moto ni zaidi ya 400.
Alisema shule hiyo yenye kidato cha kwanza hadi cha nne, ina jumla ya wanafunzi 1,045, wakiwemo wavulana 561 na wasichana 484 huku wanafunzi wa bweni wakiwa 911.
Hata hivyo, mkuu huyo alisisitiza kuwa chanzo cha moto huo ni mshumaa uliokuwa umeachwa bila kuzimwa na mwanafunzi aliyekuwa anasoma na kupitiwa na usingizi.
Abdulaziz alikanusha na kusema moto huo si hujuma kama ambavyo moja kati ya magazeti ya kila siku (si Tanzania Daima) hapa nchini yalivyoandika jana.
Wakati huo huo, Mjumbe wa Bodi ya shule hiyo, Salum Chota, alisema alikuwa wa kwanza kufika eneo la tukio kuzima moto huo.
Chota alisema uvumi wa kuwa mwanamama mmoja alikuwa akiwazuia wanafunzi kupita mlangoni si kweli, kwani mtu aliyekuwa mlangoni ni mwanafunzi wa kiume ambaye alikuwa akisaidia kuwaokoa wahanga wa tukio hilo.
Alisema ugumu wa wanafunzi hao kutoka katika bweni hilo ulitokana na nondo zilizowekwa katika bweni hilo, hivyo wananchi kulazimika kuvunja madirisha na kubomoa milango ili kuweza kuokoa wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk. Ezekiel Mpuya, alisema hali za majeruhi wa tukio hilo zinaendelea vizuri ukilinganisha na juzi walipofikishwa hospitalini hapo.
Mkuu wa Mkoa, alisema kuwa pamoja na maiti moja kati ya 12 kutambuliwa na ndugu, bado wazazi wote wa wanafunzi waliokufa katika tukio hilo walikubaliana maiti zote kuzikwa katika kaburi moja shuleni hapo.
Wanafunzi waliokufa katika tukio hilo ambao leo watazikwa kaburi moja ni Matrida Mtewele, Adelvina Kwama na Elizaberth Mtavila waliokuwa wanasoma kidato cha kwanza.
Wengine ni Digna Nduguru, Chake Kuyaa, Seciliana John, Lazia Kihwele, Witness Mbilinyi na Stellah Mwigavilo waliokuwa wanasoma kidato cha pili.
Pia wamo Falha Abdallah na Jesca Wissa waliokuwa kidato cha tatu na Maria Ndole wa kidato cha nne ambapo alisema kutokana na marehemu hao kuteketea kiasi cha kutotambulika, wametumia njia zingine kupata majina yao.
Majeruhi waliolazwa hospitalini ni Mwizarubi Eliasi, Lucy Sawani, Faraja Sodike, Anoda Ambali, Lela Mkuya, Prisca Melele, Evamary Carlos na Sabrina Abdulhaman.
Wengine ni Lenna Barugu, Zuhra Mazora, Veronika Nyamule, Theresia Zuvapi, Esther Zayumba, Ando Mamba, Irene Mponzi, Ares Ndaga, Lucy Luvanda, Upendo Nyamadule, Fraja Palinoo na Helena Mapunda.
Powered by vBulletin™ Version 4.0.2 Copyright © 2012 vBulletin Solutions, Inc. All rights reserved.