
Originally Posted by
mwanakijiji
Ummy Muya (Mwananchi)
WAKILI Simon Mponda ambaye anamtetea Mwanasheria Mkuu wa zamani wa serikali (AG), Andrew Chenge katika kesi ya mauaji ya wasichana wawili amekuja juu na kuita mahakama iharakishe kutoa maelezo ya upande wa mashtaka dhidi ya tuhuma za mteja wake, ili kesi iendelee badala ya kuahirishwa mara kwa mara.
Mponda alisema jana mbele ya Hakimu Kwey Rusema wa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara kutokana na kukosekana maelezo hayo.
"Naomba mahakama iharakishe kutoa maelezo ya upande wa mashtaki ili kuliwezesha shauri hili kuanza kusikilizwa, kwani kila mara tunahudhuria mahakamani lakini huwa linapigwa tarehe kwa kukosa maelezo,"alisema Mponda.
Kesi hiyo ambayo maelezo yake ya awali yalipangwa kuanza kusikilizwa jana ilishindikana hivyo kuahirishwa hadi Aprili 9, mwaka huu kwa sababu mwendesha mashtaka ambaye ni Wakili wa Serikali, Richard Rweyongeza alikuwa kwenye kesi nyingine katika mahakama ya rufaa.
Chenge alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Machi 30 mwaka jana, akikabiliwa na mashtaka matatu kabla ya kuongezea moja na kufikia idadi ya mashtaka manne.
Ilidaiwa mahakamani kuwa Machi 27 mwaka jana, Chenge alisababisha kifo cha Victoria George kwa kuendesha gari kizembe katika Barabara ya Haile Selassie, Wilaya ya Kinondoni akiwa na gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin, kisha kuigonga pikipiki ya matairi matatu aina ya Bajaj na kusababisha kifo cha Victoria ambaye alikuwa abiria(katika Bajaj hiyo).
Shtaka la pili, Chenge anadaiwa kuwa siku na muda huo huo, alisababisha kifo cha Beatrice Constantine kwa kuendesha gari kizembe.
Shtaka la tatu ni kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha uharibifu wa Bajaj ambayo ilikuwa imebeba wanawake hao na la nne ni kuendesha gari bila kuwa na hati ya bima.
Akimsomea mashtaka hayo, Mwendesha Mashtaka Mkuu, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), David Mafwimbo, alidai mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi, Emiliusi Mchaulo, kuwa katika shtaka la kwanza, Chenge anadaiwa kusababisha kifo cha Victoria George kwa uendeshaji wa gari kizembe.
Alidai kuwa Machi 27, mwaka jana, saa 10:30 alfajiri katika Barabara ya Haile Selassie, wilayani Kinondoni, akiwa anaendesha gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin, kwa uzembe na kushindwa kuchukua tahadhari kama inavyotakiwa kwa watumiaji wa barabara, aligonga Bajaj na kusababisha kifo cha Victoria na Beatrice Constantine waliokuwa katika pikipiki hiyo.
Mshtakiwa huyo alikana mashtaka yote na ASP Mafwimbo aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika.
Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Mchaulo, alisema ili mshtakiwa adhaminiwe, lazima awe na mdhamini mmoja ambaye atasaini bondi ya Sh1 milioni.
Chenge alidhaminiwa na Mkurugenzi wa Fedha toka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHCR), Ezekiel Masanja na kesi hiyo ikaahirishwa hadi Aprili 30, mwaka jana.
Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika serikali ya awamu ya tatu na Waziri wa Miundombinu katika serikali ya awamu ya nne, wakati ajali hiyo ikitokea, alikuwa akiendesha gari lake binafsi.
Bookmarks